TANGAZO


Friday, August 15, 2014

Ukraine kukagua misaada kutoka Urusi





Lori la Urusi lililobeba msaada kwenda Ukraine likikaguliwa

Ukraine imesema walinzi wake wa mpakani watakagua malori ya Urusi yaliyobeba misaada yenye kulitiliwa mashaka kwenda Uraine. Malori hayo yameegeshwa katika eneo la mpaka wa nchi hizo.
Maafisa wa Ukraine wamesema wakaguzi wamewasili katika eneo hilo kukagua mizigo inayotarajiwa kupelekwa katika miji ya mashariki ya Ukraine inayoshikiliwa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi.
Ukraine ina wasiwasi kuwa msafara wa malori hayo huenda yakabeba silaha kwa ajili ya waasi, tuhuma ambazo Urusi imezikataa.
Alhamisi, waandishi wa habari wawili walisema waliyaona magari ya kijeshi ya Urusi yakielekea Ukraine, katika eneo linaloshikiliwa na waasi.
Maafisa usalama wa Ukraine wamesema wameona watu wenye silaha na malori ya kijeshi yakiingia Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Carl Bildt, akiwa mjini Brussels, Ubelgiji kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, ameitaja hatua hiyo kama "ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa".


Lori lililo katika msafara wa kupeleka msaada Ukraine
Serikali ya Urusi imezidi kukanusha kutoa silaha na mafunzo kwa waasi, ambao walisababisha mgogoro mwezi Aprili wakati walipotwaa udhibiti wa miji kadha mashariki mwa Ukraine.
Maafisa wa Ukraine wamesema kuwa msaada huo utapelekwa Luhansk baada ya kukaguliwa na timu ya wakaguzi wa forodha 80 na walinzi wa mpaka.
Luhansk, mji ulio ngome ya waasi, umeshuhudia mapigano makali Alhamisi, kama ilivyokuwa kwa mji wa Donetsk, ambao pia unashikiliwa na waasi.
Hata hivyo Mkuu wa Operesheni ya Usambazaji misaada wa Shirika la Msalaba Mwekundu huko Ulaya na Asia ya Kati, Laurent Corbaz, amesema msaada huo hautasambazwa hadi hapo wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu ambao wamepangwa kusambaa misaada hiyo watakapohakikishiwa usalama wao.

No comments:

Post a Comment