*Awataka Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kufanya maamuzi yenye maslahi mapana ya Taifa kwa ajili ya kupata Katiba mpya
Makamu wa Rais wa Jahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilal akiwasha Mwenge wa Uhuru ikiwa ni uzinduzi rasmi wa Mbio za mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2014 ambapo kitaifa zimeanzia mjini Bukoba mkoani Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge Taifa Angela Stevene Kasanda tayari kwa kuanza mbio za mwenge mkoani hapo leo.
Wakimbiza Mwenge kitaifa wakikimbiza Mwenge wa Uhuru kuelekea nje ya Uwanja wa Mpira wa Kaitaba tayari kuanza ziara ya kukagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispa ya Bukoba.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Mratibu wa shughuli za Mwenge Kitaifa Bw. James Kajugusi akiteta jambo na mmoja wa Maafisa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo mara baada ya zoezi la uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kukamilika leo mjini Bukoba.
Wasanii wa Kikundi cha Kakau Band wakitumbuiza wakati wa sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge mjini Bukoba leo.
Wasanii wa Kikundi cha Kakau Band wakitumbuiza wakati wa sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge mjini Bukoba leo.
Watoto wa Halaiki wakionyesha michezo mbalimbali wakati wa sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru leo mjini Bukoba.
Watoto wa Halaiki wakionyesha michezo mbalimbali wakati wa sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru leo mjini Bukoba.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Mratibu wa Mbio za Mwenge Kitaifa Bw. James Kajugusi akimsaidi motto wa Halaiki kutengeneza Mwamvuli wakati wa sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge leo mjini Bukoba.
Askari Polisi akiimarisha ulinzi wakati wa sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika leo mjini Bukoba.
Na Aron Msigwa na Frank Shija- MAELEZO
2/5/2014.BUKOBA
MAKAMU wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal ametoa wito kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kufanya maamuzi yanayozingatia maslahi mapana ya Taifa ili kufanikisha upatikanaji wa Katiba itakayokidhi matakwa na matarajio ya wananchi.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi la kupiga kura ya maoni ili kufanikisha upatikanaji wa katiba shirikishi itakayoliongoza taifa kwa kipindi kirefu bila kuhitaji kufanyiwa marekebisho.
Akizindua Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2014 leo katika uwanja wa Kaitaba, manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Dkt. Bilal amesema mchakato unaoendelea wa upatikanaji wa katiba mpya ni jukumu la watanzania wote na kuongeza kuwa kila mwananchi analo jukumu la kuelewa mchango, wajibu na nafasi aliyonayo ili kukamilisha mchakato huu muhimu.
“Bunge Maalum la Katiba linaendelea na kazi kubwa, nachukua fursa hii kulipongeza kwa hatua linayoendelea nayo naamini maamuzi yote yatakayofikiwa yatazingatia maslahi mapana ya nchi yetu na kutoka na katiba inayokidhi matakwa ya wananchi” Amesema.
Amesema mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu zinabeba ujumbe muhimu usemao Katiba ni Sheria Kuu ya nchi chini ya Kauli inayowahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ya maoni ili kuliwezesha taifa kuwa na Katiba mpya.
Dkt. Bilal ameeleza kuwa kila mwaka nchini mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na kauli ya kudumu kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, Rushwa , Dawa za kulevya na Malaria kwa lengo la kuwakumbusha wananchi kuendelea kupambana na chanagamoto hizo na kutafuta mbinu za kujikwamua .
Kuhusu changamoto hizo hususan ugonjwa wa Malaria amefafanua kuwa ni kati ya magonjwa yanayosababisha vifo kwa kiwango kikubwa hasa kwa akina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka 5 na kuongeza kuwa mapambano dhidi ya ugonjwa huo sharti yapewe kipaumbele katika mbio za Mwenge kwa viongozi wa mbio hizo pamoja na mambo mengine kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo katika maeneo yote watakayopita kuanzia mwaka huu na kuendelea.
Ameeleza kuwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu ugonjwa huo zinaonesha kwamba kati ya watu bilioni 3.3 sawa na nusu ya idadi ya watu duniani wako kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo.
Amesema Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika ambazo ugonjwa wa malaria ni moja ya magonjwa yanaoongoza kwa kusababisha vifo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5 na wajawazito imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabilia na tatizo hilo.
“Kwa upande wetu serikali tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuifanya Tanzania bila Malaria iwezekane kwa wataalam wetu kuendelea kutoa ushauri na maelekezo kwa wananchi, kuimarisha upatikanaji wa dawa na huduma za matibabu katika hospitali zetu,kuhimiza matumizi ya vyandarua vyenye dawa, kuhimiza matumizi sahihi ya dawa za kuzuia malaria kwa akina mama wajawazito na watoto walio chini ya miaka 5”
Kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi nchini Dkt. Bilal ameeleza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na jumuiya za kimataifa ili kuhakikisha kuwa maambukizi mapya ya VVU yanapungua na kufikia sifuri ifikapo mwaka 2015.
Akizungumzia mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini amefafanua kuwa jukumu hilo linahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali na wananchi na kueleza kuwa kwa upande wa serikali, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya inaendelea kutekeleza jukumu lake ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama.
“Tunatambua kuwa vita ya dawa za kulevye ni kubwa na inahitaji mchango wa kila mwananchi sote tunatakiwa kuungana na tume ili kuisaidia kutimiza majukumu yake”
Kwa upande wake waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akizungumza kabla ya uzinduzi wa mbio hizo amesema kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa zikiwahamasisha wananchi kuibua, kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo wanayoishi.
Amesema kwa mwaka huu Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwa muda wa siku 165 katika Halmashauri za wilaya zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na zitahitimishwa mwezi Oktoba mwaka huu mkoani Tabora.
Kuhusu ujumbe wa mbio za Mwenge mwaka huu Dkt. Mukangara ameeleza kuwa unalenga kuwahamasisha wananchi popote walipo kushiriki kikamilifu katika mchakato wa katiba mpya ili kupata katiba bora kwa maslahi na mustakabali wa Taifa.
“Kwa kuwa katiba ndiyo sheria kuu ya nchi ni muhimu tukahakikisha kuwa kila mwananchi anatimiza wajibu wake wa kutoa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ,nawahakikishia mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka huu zitafanya kazi hiyo ya kuwahamasisha wananchi kutimiza haki yao kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ”
Naye Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe awali akizungumza wakati wa kuwakaribisha viongozi mbalimbali wa serikali, mabalozi, nchi washirika wa maendeleo na viongozi majirani wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani Kagera zitaweka msisitizo mkubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, Rushwa,Mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, uvunjifu wa amani na kila aina ya chuki na uhasama.
Amesema Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya taifa la Tanzania na kufafanua kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu ni za kipekee kutokana na umuhimu wake katika mkoa wa Kagera.
“Mwenge wa Uhuru ni chachu kubwa ya maendeleo utaleta matumaini, amani na heshima pale palipojaa dharalau na kwa hakika Mwenge huu utamulika na kuwafichua majambazi wenye silaha, wanaoishi nchini bila kufuata sheria, wezi wa mifugo, wanyanyasaji wa kijinsia, washirikina, waharibifu wa mazingira, wanaojichulia sheria mkononi, wavivu na walevi saa za kazi na wale wenye kuchochea migogoro ya dini na kabila” Amesisitiza.
Ameeleza kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2014 mkoani Kagera zitazindua utekeelezaji wa jumla ya miradi 69 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 69.
Amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya 7 za mkoa huo ambazo ni Biharamulo, Bukoba, Karagwe, Kyerwa, Missenyi, Muleba na Ngara kabla ya kukabidhiwa kwa viongozi wa mkoa wa Kigoma.
No comments:
Post a Comment