Watu wenye silaha katika mji wa
Benghazi nchini Libya wameshambulia makao makuu ya jeshi la usalama na
kuibua mapigano yalioyosababisha watu watano kuuawa.
Shambulio hilo limefanyika mapema asubuhi ambapo
watu wengine wapatao kumi walijeruhiwa katika mapigano yaliyoendelea
kwa zaidi ya saa moja baadaye.Benghazi imekumbwa na ghasia tangu mwaka 2011 wakati wa vuguvugu la nchi za Kiarabu.
Vuguvugu hilo lilimaliza utawala wa miaka 42 ya aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, lakini serikali ya nchi hiyo tangu wakati huo imekuwa ikihangaika kudhibiti makundi ya wapiganaji na wanamgambo walioshiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na kujaribu kuwapokonya silaha bila mafanikio mpaka sasa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, ni askari watano waliouawa katika vita vya mapema asubuhi, Ijumaa.
Vikosi maalum viliingilia kati ili kuwaondoa wavamizi na mapigano kusambaa katika maeneo kadhaa, limearifu shirika hilo.
Watu hao wenye silaha pia wameshambulia nyumba ya mkuu wa usalama wa Benghazi, Kanali Ramadan al-Wahishi, lakini hakujeruhiwa, afisa usalama mmoja ameiambia Reuters.
Ghasia hizi zimekuja siku tatu baada ya bomu lililotegwa katika gari kulipuka katika lango la kambi ya kijeshi karibu na uwanja wa ndege na kuua askari wawili.
Benghazi ulikuwa kitovu cha uasi dhidi ya Kanali Gaddafi, lakini tangu wakati huo umekuwa kituo cha mashambulio katika taasisi za umma na maafisa wake.
Benghazi ndiyo mji mkubwa kuliko yoye mashariki mwa Libya, ambako baadhi ya makundi na wanamgambo wa Kiislam wanataka madaraka zaidi ya kujiamulia mambo yao wenyewe na kupewa sehemu kubwa zaidi ya mapato yatokanayo na utajiri wa mafuta katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment