Ingawa Abdel Fattah al Sisi, bado hajawa Rais, kiongozi huyo wa zamani wa jeshi anasema kuwa anafahamu kwamba analengwa na kundi la watu wasiompenda.
Katika mahojiano ya kwanza katika runinga alisema kuwa tayari kumekuwa na majaribio mawili ya kumuua.
Hakutoa ushahidi wowote zaidi kuhusiana na majaribio hayo ya kumuua.Alisema kuwa yeye haogopi lolote kwa sababu anaamini kuwa lililopangwa kuwa litakuwa.
Waziri huyo wa zamani wa ulinzi alisema kuwa hana mpango wa kupatana na vuguvugu la Muslim Brotherhood.
Alisema raia wa Misri walishaamua na akaapa kuwa kundi hilo halitaruhusiwa kuwepo nchini humo atakapochaguliwa kuwa Rais.
El Sisi alipata nafasi, kama kiongozi wa jeshi, kukabiliana na vuguvugu la Muslim Botherhood. Viongozi wengi wa kundi hilo hivi sasa wako gerezani.
Amekanusha kuwa alikuwa na lengo la kisiasa aliposhiriki katika kumtimua uongozi Rais aliyeondolewa Mohammed Morsi, Julai mwaka uliopita.
Alisema anagombea Urais ili aweze kupambana na maadui wa Misri walioko nchini na nje.
Mwanajeshi huyo wa muda mrefu amewahakikishia raia wa Misri kuwa akishinda uchaguzi atajitahidi kuwa jeshi halihusiki vyo vyote katika utawala wa taifa hilo.
Kwa kuwa jeshi limekuwa mstari wa mbele katika utawala nchini Misri kwa zaidi ya nusu karne kuna wale wanaomtilia shaka El Sisi anaposema kuwa jeshi halitashirikishwa katika uongozi wake iwapo anashinda uchaguzi.
Taarifa hiyo ya El Sisi ilikatizwa mara kadhaa katika mitaa mingi ya Cairo kutokana na kukatika kwa umeme mara kadhaa.
Akishinda uchaguzi wajibu wake muhimu wa kwanza utakuwa kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kupata umeme bila kukatizwa.
No comments:
Post a Comment