Bunge la Kenya
Wakenya wanakabiliwa na tisho la kufungwa jela mwaka mmoja au kulipa faini ya dola 23,000 kwa kukosa kumuita mbunge 'mheshimiwa' unapozungumza naye.
Sheria hii mpya inayopendekezwa na wabunge wa Kenya inalenga kuhakikisha kila afisaa mkuu wa serikali anapewa heshima anayostahili.
Adhabu hiyo itawakuta wale watakaokosa kumpa Rais heshima zake kwa kumuita 'Mtukufu Rais', naye spika wa bunge atapaswa kuitwa 'Mheshimiwa spika wa bunge'Watakaovunja sheria hiyo watapata adhabu kali.
Mswada huu uliwasilishwa na mbunge mmoja kwa jina Adan Keynan, ambaye amesema kuwa umuhimu wake ni kuonyesha heshima kwa maafisa wa serikali.
"ni muhimu kuonyesha picha nzuri ya nchi, kuhakikisha kuna mpangilio na maadili mema katika mchakato wa utawala, '' alisema bwana Keynan.
Huku mzozo kati ya wabunge na magavana ukiendelea kutokota, mswada huo haujapendekeza chochote kuhusu cheo cha magavana ambao ni wakuu wa majimbo na watakavyoitwa.
Wataendelea kuitwa tu magavana.
Mswada huo pia unapendekeza kuwepo vyeo kwa maafisa wa serikali kulingana na ukubwa wao.
Ikiwa mswada huo utakuwa sheria, cheo cha mbunge kitakuwa juu zaidi kuliko cha gavana , majaji wa mahakama ya juu , marais wa zamani na makamu wa rais.
Kadhalika mswada huo utatumika katika kuweka mpangilio kuhusu ambavyo maafisa wa serikali watakuwa wanaketi katika hafla na mikutano ya serikali.
Maafisa wa serikali watakaojipatia vyeo vingine mbali na vile vitakavyoorodheshwa katika mswada huo watatowa faini ya dola milioni mbili.
No comments:
Post a Comment