Mchezaji wa timu ya Ofisi ya Rais (Utumishi) Fatuma Machenga (GS) akifunga goli dhidi ya timu ya Alliance One katika mechi ya mashindano ya Mei Mosi mwaka huu iliyofanyika jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mchezaji wa timu ya Ofisi ya
Rais (Utumishi) Mwadawa Twalibu (GA) akitoa pasi kwa Fatuma Machenga (GS)
katika mechi ya mashindano ya Mei Mosi mwaka huu iliyofanyika jana Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro. (Picha zote na Utumishi)
TIMU ya mpira wa Pete ya
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeanza mashindano ya Mei Mosi 2014 kwa
ushindi mnono kwa kuichapa timu ya Alliance
One ya Morogoro magoli 46 kwa 7.
Mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Jamhuri
Siku ya Pasaka uliwachukua Utumishi takribani dakika 10 za mchezo kuwasoma
wapinzani wao na kuanza kufunga ambapo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Alliance
One walishakubali magoli 23 dhidi ya 5.
Wachezaji waliofanikisha
ushindi huo ni Fatuma Machenga (GS) kwa kushirikiana Mwadawa Twalibu (GA),
ambao walifanikiwa kufunga magoli 34 na 12 katika goli la wapinzani wa
Utumishi.
Mara baada ya mchezo huo nahodha
wa timu ya Ofisi ya Rais (Utumishi) Elizabeth Fusi alisema kuwa amefurahishwa
na matokeo hayo na kuahidi kuendelea kuzitimulia vumbi timu pinzani katika
michezo itakayofuata.
“Tumepania kuwa mabingwa
mwaka huu hivyo tutacheza kwa bidii ili kuhakikisha tunatimiza ndoto yetu” Fusi
alisema.
Naye, Mwenyekiti wa timu ya Alliance One Bw. Charles J.
Kung’aro alikiri kuwa timu yake ilizidiwa mbinu
za kimchezo na Utumishi hivyo kuwaweka wachezaji wake katika wakati
mgumu kimchezo hasa wanaposhambuliwa.
“Tuliruhusu wautawale mchezo
hivyo ikawa rahisi kwao kutufunga hivyo tumejipanga kurekebisha makosa yetu ili
tufanye vizuri katika mechi zijazo” Bw. Kung’aro alisema.
Mashindano ya Mei Mosi 2014 kitaifa
yanafanyika mjini Morogoro kwa kuhusisha michezo ya mpira wa miguu, netiboli,
kuvuta kamba, riadha, mbio za baiskeli, karata, bao na drafti.
No comments:
Post a Comment