Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Gulatone Masiga akifafanua jambo kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani). Kushoto ni Asbert Sweya kutoka Chuo Kikuu cha Kampala, wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo jijini Dar es Salaam.
TAMKO LA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
SISI wanafunzi wasomi katika Vyuo Vikuu mbalimbali
vilivyoko Dar es Salaam (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); Chuo Kikuu cha
Ardhi (ARU); Dar es Salaam University College of Education (DUCE); USTAWI WA
JAMII; Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (St. John); Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM);
Open University of Tanzania (OUT); Kampala International University (KIU); Dar
es Salaam Institute of Technology (DIT); Institute of Adult Education (IAE);
Tanzania School of Journalism (TSJ); College of Business Education (CBE) na Chuo
cha kumbukumbu ya Mwl JK Nyerere. Sisi sote tunalaani mwenendo uliyojengeka kwa wanasiasa
wanaojiita “UKAWA“ kuvuruga Bunge
Maalum la Katiba kwa sababu ambazo si za msingi. Kwanza walianza kudhalilisha wanazuoni wanaoonekana
kutofautiana nao kimawazo kuhusu msimamo wao wa kutaka serikali tatu. Wanazuoni
ambao wamekuwa wakidhalilishwa na kutungiwa uongo ni pamoja na Profesa Issa Shivji, Profesa Teddy Malyamkono,
Profesa Nehemia Osoro, Dk. Francis Michael, na Dk. Kitila Mkumbo. Tungependa
kuwataarifu kuwa wanataaluma wana uhuru
wa kutoa mawazo yaani academic freedom
na kamwe hawawezi kukaa kimya wanapoona kuna jambo linaloweza kuifanya nchi ikaangamia na kusambaratika. Wanazuoni huamini katika “no research, no data, no right to speak” kwani data zao za
kiuchumi, kihistoria, kisiasa na kidiplomasia zinakataa muundo wa serikali
tatu. Hoja ya kimsingi ni kuwa “UKAWA” imeanza
juzi, je tafiti (research) wamezifanya lini za kuzipa nguvu hoja zao za kutaka
serikali 3?
Tatizo
lingine tunaloliona kwa “UKAWA” ni
kujaribu kuwadhalilisha waasisi wa taifa letu hasa Mwl JK Nyerere na Sheikh
Abeid Aman Karume. Je tusipomuamini Mwl Nyerere na Sheikh Karume tumuamini nani
kati ya hawa ambao hatuna ushahidi wa uzalendo wao? kwani wapo wanasiasa ya
aina yao ambao wametumika na mataifa ya kibeberu kuvuruga nchi zao na mpaka leo
wananchi wao wanataabika mfano
hai ni Misri, Tunisia, Morocco, Sudan Kusini, Somalia, Libya, Mali Na Afrika ya
Kati. Heshima walionayo waasisi wetu Mwl Nyerere na Sheikh Karume
ndani na nje ya Tanzania, sio ya kupuuzwa wala kufananishwa hata kidogo na
yeyote yule miongoni mwa waliounda “UKAWA”
zaidi ya kutumika kama mfano na kielelezo. Tunawashangaa baadhi ya wanasiasa wa “UKAWA” kuwakejeli waasisi wa taifa letu.
Wanasiasa hawa ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Maalim Seif Sharif Hamad, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, Mh. Tundu Lissu na Halima
Mdee kwani wamesoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichoasisiwa na
waasisi wakuu wa taifa letu, Mwl JK Nyerere na Sheikh Karume. Hata wale
wanasiasa wengine ambao hawakupata bahati ya kusoma Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam wamesoma kwenye shule za awali na vyuo vya elimu ya juu ambavyo vina
msingi wa utawala bora wa waasisi hawa wakuu wa taifa letu. Hivyo tunaona sio
busara hata kidogo kukejeli mchango wao katika harakati za kuliendeleza taifa
letu. Tunapenda kuwathibitishia watanzaia kuwa mawazo ya waasisi wa taifa letu hajachakaa na wala hayapitwa na wakati hata mara moja.
Sisi
kwa mtazamo wetu kama vijana wasomi wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu
tunashauri yafuatayo;
- Katiba
bora haiwezi kupatikana kwa kususia vikao halali vya bunge maalum la
katiba na maandamano, hivyo tunawasihi warejee bungeni ili waendelee na
mchakato kutengeneza katiba. Hatua hii ya kurejea bungeni ikishindikana, warejeshe
posho za vikao ambavyo hawajahudhuria.
- Kutofautiana
kimawazo kwa njia ya kujenga hoja ndio demokrasia pevu yenye dhana ya
“wachache wasikilizwe na wengi wapewe” ambayo ni moja ya misingi mikuu ya
demokrasia itakayotupatia “Katiba Bora” ya sasa na vizazi vijavyo.
- Lazima wafahamu kuwa maridhiano ndio njia
pekee ya kupata “Katiba Bora” yenye kuleta “Elimu Bora”; “Kilimo Bora”;
“Afya Bora”; “Uchumi Bora” na “Utawala Bora” kwa maisha bora ya mtanzania
na pia kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu ili kupigiwa
mfano na kuwa kimbilio la waafrika wenzetu wengi wanaotaabika kwa kuzikimbia
nchi zao kwa machafuko yanachochewa na mabeberu wa siasa na uchumi duniani.
- Tunawasihi
wenzetu wazingatie umuhimu wa kulinda, kudumisha, kustawisha na
kuiendeleza amani katika kipindi cha kutengeneza katiba na baada ya
mchakato. Tusipojiangalia tutakuwa kama wenzetu Misri, Tunisia, Morocco,
Sudan Kusini, Somalia, Libya, Mali na Afrika ya Kati. Tunaamini kwa
kuangalia hali za kisiasa za nchi nyingi za Afrika tunaamini kuwa siasa ya
Tanzania ni safi na hakuna haja ya kuhamasisha chuki, uzandiki, uzushi, uongo
maandamano na uasi ambao ni sumu kali ya umoja (muungano), amani na uhai
wa taifa letu tukufu la Tanzania.
- Watanzania
na wanasiasa wafahamu kwamba mataifa kama Marekani na Uingereza yametawala
dunia kwa sababu ya umoja wao. Tunaomba tujifunze kwa yaliyotokea Urusi,
leo hii imeona umuhimu wa kuzirudisha nchi ambazo zilisambaratika kutoka
kwenye serikali ya umoja wa nchi za kijamaa za kisovieti (USSR). Sisi
vijana wa kizazi kipya tunawashauri wenzetu waulinde muungano kwa gharama
yeyote na muungano huwa haupitwi na wakati. Tunajiuliza kwa wenzetu wa
Ulaya na Marekani ambayo miungano yao imedumu kwa karne zaidi ya tano na
sita. Je huko hakuna vijana wa vizazi vipya? Sisi tunaona kuwa wanaodai
Utanganyika na Uzanzibari ni wakabila na wabaguzi wanaotaka kuturudisha
enzi za ukoloni.
- Tunamuomba
Mwenyekiti wa Bunge Maalum azingatie kwamba Bunge Maalum la Katiba si la
“UKAWA” ni la watanzania. Hivyo basi liendelee kwa kasi na ufanisi zaidi
na lisiyumbishwe na hasira za wachache wanaojiita “UKAWA” kutokana na ukweli
kwamba gharama, muda na nguvu kubwa
vimetumika mpaka sasa. Tunaomba bunge liendelee ili kuwapatia watanzania
katiba iliyo bora.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Afrika
Imetolewa na Gulatone
Masiga, Mwanafunzi UDSM
Kwa niaba vijana
wazalendo wa Vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment