TANGAZO


Tuesday, April 1, 2014

SSRA yatoa taarifa kuhusu uandikishwaji wanachama wapya kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini Tanzania

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Ansgar Mushi (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu uandikishwaji wa wanachama wapya wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini Tanzania. Kulia ni Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka hiyo, Ibrahim Ngabo. (Picha zote na Dotto Mwaibale)

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Ansgar Mushi (wa pili kushoto), akisoma taarifa hiyo, kwa waandishi wa habari. Kutoka kulia ni Ofisa Mahusiano na Ushawishi wa SSRA, Stewart Bisanda, Mkurugenzi wa Idara ya Fedha na Utawala, Mohamed Nyasama, Mkurugenzi wa Sheria, Ngabo Ibrahim na Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Ushawishi wa SSRA, Sarah Kibonde.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Ansgar Mushi (kushoto), akisisitiza jambo katika mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari waliokuwepo kwenye mkutano huo, wakichukua taarifa hiyo.
Mkurugenzi wa Sheria wa SSRA, Ibrahim Ngabo (kulia), 
akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu masuala 
mbalimbali ya kisheria katika mkutano huo. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Ushawishi wa SSRA, Sarah Kibonde.


Na Dotto Mwaibale
MAMLAKA ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), imesema haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote anayekiuka sheria za kujiunga na mfuko wowote ulioanzishwa kwa sheria ya Bunge.

Hayo, yalibainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Ansgar Mushi wakati akitoa taarifa kwa umma kupitia kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu uandikishwaji wa wanachama wapya wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini.

*Ifuatayo ni Taarifa kamili kutoka Mamlaka hiyo
1.  UTANGULIZI
Mnamo mwaka 2008 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha  Sheria Na.8 ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.Pamoja na mambo mengine Sheria  hii imeanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii(SSRA).Jukumu kubwa la Mamlaka hii ni kusimamiana kudhibiti shughuli zote za sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini ikiwa ni pamoja na Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii iliyoanzishwa kwa Sheria za Bunge (NSSF,PSPF,PPF, GEPF,LAPF na NHIF).
2.  MAREKEBISHO YA SHERIA ZA MIFUKO
Tunapenda kuutarifu Umma kwamba Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zimefanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Sekta ya Hifadhi ya Jamii,Sheria Na.5 ya mwaka 2012.Moja ya maeneo yaliyofanyiwa  marekebisho na Sheria hiyo Na. 5 ya mwaka 2012 ni pamoja na Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii kuruhusiwa kuandikisha wanachama  wapya wanaoingia kwenye ajira  kwa mara ya kwanza  kutoka sekta rasmi au sekta isiyo rasmi.Ruhusa hiyo pia inahusisha wafanyakazi ambao wako kwenye ajira lakini hawajawahi kuandikishwa na Mfuko wowote.Marekebisho haya ambayo yameondoa ukiritimba katika uandikishaji wa wanachama yamefanyika ili kutimiza matakwa ya kifungu cha 30 cha Sheria  Na. 8 ya mwaka 2008 iliyoanzisha  Mamlaka ambayo inampa uhuru mfanyakazi kujiunga na Mfuko wowote ulioanzishwa kwa Sheria ya Bunge.

3.  UANDIKISHWAJI WA WANACHAMA
Hivi karibuni kumejitokeza malalamiko kuhusiana na uandikishaji wa wafanyakazi wapya wanaojiunga na ajira kwa mara ya kwanza kutoka sekta ya Umma na sekta binafsi. Baadhi ya vitendo vinavyolalamikiwa ni pamoja na:-
·      Mfuko kutengeneza, kutoa na/au kusambaza nyaraka za uwongo kwa madhumuni ya kupotosha umma kuhusu utendaji wa Mifuko mingine ikiwemo afya ya Mfuko kifedha na aina ya mafao yatolewayo kwa lengo la kujipatia wanachama.
·      Mfuko kupotosha hali halisi ili kupata ridhaa ya wafanyakazi, waajiri na wadau wengine.
·      Mfanyakazi kuandikishwa kwenye Mfuko wa lazima (mandatory scheme) wakati amekwishaandikishwa na Mfuko mwingine.
·      Mfanyakazi kulazimishwa au kushurutishwa na mwajiri au Mfuko kujiandikisha na Mfuko fulani.
·      Mwajiri kumchagulia mfanyakazi Mfuko wa kujiunga nao.
·      Mwajiri kuwa na mikataba ya ajira au sera au miongozo ya ajira inayoelekeza wafanyakazi wake kujiunga na Mfuko fulani.
·      Mifuko kutumia njia za usajili zisizofaa kuandikisha wanachama.
Vitendo vyote vilivyoainishwa hapo juu vimeharamishwa chini ya Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 na Miongozo ya Uandikishaji Wanachama {Social Security Schemes (Membership Registration) Guidelines, 2013} iliyotolewa chini ya sheria hiyo. Yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo anavunja sheria na Mamalaka haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria.
Mamlaka inapenda kuikumbusha Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii pamoja na wadau wote wakiwemo waajiri na wafanyakazi kuzingatia matakwa ya Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 pamoja na Miongozo ya Uandikishaji Wanachama ili kulinda uhuru wa mwanachama wa kujiunga na Mfuko anaoupenda.
Imetolewa na;
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
S.L.P 31846 Dar es Salaam
    Tel:+255 222761683/8
      Tovuti: www.ssra.go.tz

No comments:

Post a Comment