TANGAZO


Wednesday, April 2, 2014

Shirika la WOINSO kuzindua mpango wa elimu kuhusu athari za magonjwa ya ngono, utoaji mimba na mahusiano mashuleni

Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali WOINSO, Bi. Janeth Sebastian (katikati) akifafanua jambo juu ya kazi mbalimbali zifanywazo na Shirika lake wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Msaidizi wake Bi. Namsifu Singo na kushoto ni Katibu wake Bi. Consolota Simon. (Picha zote na Benedict Liwenga-MAELEZO)
Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali WOINSO, Bi. Janeth Sebastian (kulia) akijibu maswali toka kwa waandishi wa Habari (hawako pichani) wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza toka kushoto ni Mweka Hazina Philipina Raymond na katikati ni Katibu wa Shirika hilo Bi. Consolata Simon. 
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria Mkutano huo, wakisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na mtoa mada ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la WOINSO, Bi. Janeth Sebastian (hayupo pichani), jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria Mkutano huo, wakisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na mtoa mada ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la WOINSO, Bi. Janeth Sebastian (hayupo pichani), jijini Dar es Salaam leo. 

Na Benedict Liwenga-MAELEZO
SHIRIKA lisilo la Kiserikali Women in Society (WOINSO), linatarajia kuzindua mpango wa Elimu juu ya athari ya magonjwa ya ngono, utoaji mimba na mahusiano mashuleni kwa shule za msingi darasa la sita na la saba.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Shirika hilo Bi. Janeth Sebastian wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa Habari Maelezo uliopo jijini Dar es Salaam.

Bi. Janeth amesema kuwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam Shirika lake linazindua mpango huo Kiwilaya na baadae wanatarajia kuzindua pia katika Wilaya ya Ilala na Temeke ikiwemo na mikoa mingine kama Tanga, Morogoro, Pwani, Mbeya na Songea.

Bi. Janeth ameongeza kuwa Elimu itakayotolewa juu ya athari ya magonjwa ya ngono, utoaji mimba na mahusiano mashuleni kwa shule za msingi darasa la sita na la saba na Daktari Mwelimishaji italenga kuwapa uelewa wanafunzi na kuwafanya wajitambue kwa yale watakayofundishwa na hivyo kuwaepusha vijana hao na athari mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza kwao.

“Elimu hiyo watakyopewa wanafunzi wa darasa la Sita na Saba itawawezesha kuwafanya wajitambue kwa yale watakayofundishwa na hivyo kuwaepusha vijana hao na athari kama vile magonjwa yatokanayo na ngono, utoaji mimba unaosababisha vifo na ugumba na mahusiano kabla ya wakati”. Alisema Bi. Janeth.

Aidha, Bi. Janeth amewasisitiza wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kuhudhuria Uzinduzi rasmi utakaofanyika ukumbi wa Shekina Garden uliopo Mbezi Beach Makonde jijini Dar es Salaam siku ya tarehe 3/04/2014 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Meh. Yusuph Mwenda.

WOINSO ni Shirika lisilo la Kiserikali lililosajiliwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto kwa namba 00NGO/00006564 mwaka 2013. Kabla ya usajili mkubwa lilikuwa linaelimisha kwa usajili maalumu na limefanya kazi tokea mwaka 2011 ambapo makao yake makuu yapo Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment