TANGAZO


Wednesday, April 2, 2014

Ofisi ya Taifa ya Takwimu yafunga mafunzo ya zoezi la uorodheshwaji wa viwanda nchini

Mkurugenzi wa Utawala na Masoko kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Stanley Mahembe akiwatambulisha wageni walioketi meza kuu (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya Zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda nchini, mafunzo hayo yamefungwa jana mkoani Morogoro.
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera akiwahutubia wasimamizi na Wadadisi (hawapo pichani) muda mchache kabla ya kufunga mafunzo ya zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda nchini, mafunzo hayo yamefungwa jana Mkoani Morogoro.
Baadhi ya Wasimamizi na Wadadisi wa Zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda nchini wakimsikiliza kwa makini Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera (hayupo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya Zoezi hilo jana Mkoani Morogoro.
Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Serikali pamoja na Wasimamizi wa Zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda nchini mara baada ya kufunga mafunzo ya zoezi hilo jana Mkoani Morogoro. (Picha zote na Veronica Kazimoto)

Na Veronica Kazimoto, Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera ametoa wito kwa Wamiliki wa viwanda nchini kutoa ushirikiano kwa Wadadisi na Wasimamizi wa Zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Viwanda inayotarajia kufanyika mwezi Septemba, 2014.

Akiwahutubia Wasimamizi na Wadadisi wakati wa kufunga mafunzo ya  zoezi hilo mkoani Morogoro, Bendera amesema ni muhimu kwa Wamiliki wa viwanda kutoa ushirikiano kwa wadadisi ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata takwimu sahihi ya orodha ya viwanda vilivyopo nchini.

“Natoa wito kwa Wamiliki wote wa viwanda nchini kutoa ushirikiano kwa Wadadisi kwa kuwapatia takwimu sahihi za viwanda vyao, wakifanya hivyo, zoezi hili litafanikiwa kwa ufanisi mkubwa sana” amesema Bendera.

Aidha, Bendera amewatoa wasiwasi Wamiliki wa viwanda kwa kusema kuwa  zoezi hili la Uorodheshaji wa Viwanda halitaathiri  shughuli zozote za viwandani.

Awali, akitoa maelezo ya utangulizi, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morice Oyuke amesema, baadhi ya taarifa zitakazokusanywa  katika zoezi hilo ni pamoja na anuani za viwanda, mahali viwanda vilipo, aina ya umiliki na utaifa wa mmiliki. 

Taarifa nyingine ni gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi, mapato yanayotokana na uzalishaji, mwaka kiwanda kilipoanzishwa, aina ya bidhaa zinazozalishwa, idadi ya wafanyakazi na gharama za uzalishaji.

Zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda linahusu viwanda vidogo, vya kati na vikubwa na litafanyika nchi nzima kwa muda wa miezi miwili kuanzia mwezi huu Aprili mpaka Juni, 2014.

No comments:

Post a Comment