TANGAZO


Friday, April 25, 2014

Pigo kubwa Chadema Iringa, Katibu na Kamanda wa Mufindi wajiengua na kujiunga CCM


Katibu wa Chadema Jimbo la Mufindi Kusini, Emannuel Ngwalanje akikabidhi vitendea kazi vyake kwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtutura (kushoto ) baada ya kukihama  chama hicho na kujiunga na CCM.
Akiendelea kukabidhi
Akimalizia kukabidhi kadi yake
Hapa akivishwa mavazi mapya ya CCM
Shughuli ikiendelea kwa kuvalishwa kofia
Na ikamalizikia kwa kukabidhiwa kadi mpya ya CCM


Akimwaga sera

Na  Francis Godwin, Iringa
KUTOKANA  na hali  ya mambo ilivyo ndani ya chama cha  Demokrasia na maendeleo (Chadema)  kusimamisha  viongozi  wake wa kitaifa akiwemo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe Katibu wa Chadema Jimbo la Mufindi Kusini, Emannuel Ngwalanje amekihama  chama hicho na kujiunga na CCM.

  Ngwalanje alisema kuwa hajapendezwa na siasa zinazofanywa na Chadema kutokana na migogoro na vurugu zisizo kwisha na hivyo kulazimika kutulia ndani ya chama hicho tawala.

Michael Ngimbusi alisema; “Ngwalanje alikuwa nguzo kuu ya Chadema wilayani Mufindi, aliogopewa na wana CCM, hiyo ikiwa ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kushawishi na kujenga hoja.

Katika kipindi cha zaidi ya miaka minne ambacho Ngwalanje amekuwa Katibu wa Chadema Jimbo la Mufindi Kusini ameweza kushawishi zaidi ya wakazi 600 katika maeneo mbalimbali jimboni humo kujiunga na chama hicho.

Kila kiongozi wa CCM aliyepata fursa ya kuzungumzia hatua ya kiongozi huyo kujitoa Chadema na kujiunga CCM alionesha furaha isiyo kifani na kuahidi kumpa ushirikiano atakaohitaji ili kuimarisha CCM inayojipanga vilivyo katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Baada ya kukabidhi kadi na magwanda ya Chadema kwa uongozi wa CCM wilaya ya Mufindi na baadaye kupewa mavazi na kadi ya CCM jana, Ngwalanje alisema kazi kubwa iliyoko mbele yake ni kuibomoa Chadema wilayani Mufindi.

Katika hafla ya mapokezi yake iliyofanyika kijijini kwake kimilinzowo kata ya Itandula alisema; “Kazi ya kuibomoa Chadema haitaishia katika wilaya ya Mufindi pekee bali nitaiendeleza hadi Jimbo la Iringa Mjini linaloongozwa na Mchungaji Peter Msigwa kupitia Chadema.”

Huku akishangiliwa na mamia ya wakazi wa kijiji hicho waliojitokeza kushuhudia tukio hilo, Ngwalanje alisema utawala mbovu na matumizi mabaya ya fedha za ruzuku  utaisambaratisha Chadema katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema chama hicho kinapata fedha nyingi zinazotokana na ruzuku ya serikali na michango ya wanachama, wafuasi na marafiki wake wa ndani na nje ya nchi lakini zimekuwa zikiwanufaisha wachache.

Alisema wakati kundi kubwa la viongozi wa chama hicho likifanya kazi kwa kujitolea, kundi la wachache walioko makao makuu wamekuwa wakitafuna fedha hizo bila woga huku wakiwatishia wanaohoji.

Alisema demokrasia inayohubiriwa kutafutwa na chama hicho nchini ina walakini kwa kuzingatia kwamba ndani ya chama hicho zipo nafasi za uongozi ambazo kwa wengine ni uaini kuziwania.

Alisema Zitto Kabwe alikuwa ni mmoja wa viongozi tegemeo mwenye ushawishi mkubwa hasa kwa vijana wa vyuo vikuu lakini aliwekwa kikaangoni baada ya kuonekana ana nia ya kuwania uenyekiti wa chama hicho.

“Nimeamua kurudi nyumbani, nyumbani kwa baba yangu na mama yangu CCM, ili nishirikiane na wana Mufindi wenzangu kuleta maendeleo ya taifa,” alisema.

Akionesha furaha yake wakati wa mapokezi yake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia wilaya hiyo, Marcelina Mkini alimpongeza Ngwalanje kwa uamuzi huo aliouita kuwa ni wa ujasiri unaopaswa kuigwa na wana Chadema wengine.

“Milango iko wazi, njooni, tutawapokea na tutawapa ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kushughulikia kero za wananchi wetu,” alisema.

Katibu wa CCM, Wilaya ya Mufindi Miraji Mtataru alisema Mungu ameweka utaratibu wa kuwasamehe watu wanaotubu dhambi zao.
“Na katika siasa watu wanaoamua kumaliza tofauti zao kwa kukubaliana na mazingira na hali halisi ni sawa na wale wanaosamehewa dhambi zao,” alisema.

Alisema CCM ina furaha kubwa kuendelea kuwapokea watanzania waliopotea njia kwa kujiunga na vyama vya upinzani na baadaye kubaini dhambi walizofanya.

Katika mkutano huo wanachama wengine wawili wa Chadema walijitoa na kujiunga na CCM akiwemo kamanda maarufu Bernado Lugenge ambao   wote  walieleza kusikitishwa na viongozi wa juu wa Chadema kujimilikisha chama  hicho .

No comments:

Post a Comment