Watu wawili wameambukizwa ugonjwa hatari ya Ebola nchini Liberia ulioenezwa kutoka nchini Guinea ambako umewaua watu 78.
Walioambukizana ugonjwa huo ni madada wawili, mmoja wao akiwa tu ndio amerejea kutoka nchini Guinea.
Ugonjwa wa Ebola, huambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine na huua kati ya 25% na 90% ya waathiriwa.Maafisa wanasema kuna wasiwasi kuwa ugonjwa huo unaendelea kuenea.
Muimbaji mashuhuri Youssou Ndour amelazimika kukatiza ziara yake kwenda mjini Conakry kwa sababu ya mlipuko wa ugonjwa huo.
Ingawa alikuwa amesafiri hadi mji mkuu,aliambia BBC sio wazo zuri kuleta maelfu ya watu katika sehemu moja wakati ugonjwa huo umeanza kuenea kwa kasi.
Mlipuko ulianza nchini Guinea wiki jana na kuenea hadi mji mkuu ambao una watu milioni mbili.
Waziri wa afya nchini Senegal, Awa Marie Coll-Seck, alisema kuwa serikali imeamua kufunga mpaka wake na Guinea, baada ya kuthibitisha kuwa ugonjwa huo umeenea hadi mjini Conakry.
Pia kumekuwa na taarifa ya ugonjwa huo kuwepo nchini Sierra Leone, lakini taarifa hiyo haijathibitishwa.
Ugonjwa wenyewe unaaminika kuenea kutoka kwa Popo wanaoishi mitini na ambao huliwa na watu Kusini Mashariki mwa Guinea.
No comments:
Post a Comment