Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu kupungua kwa mfumuko wa bei nchini kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali nchini. Kulia ni Meneja wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei.
Na Aron Msigwa – MAELEZO
Imeelezwa kuwa Tanzania inapiga hatua nzuri katika maendeleo ya uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki kutokana na kupungua kwa mfumuko wa bei wa taifa hali inayoleta unafuu wa maisha kwa mlaji.
Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka 2013 kuanzia mwezi Januari mpaka mwezi Desemba umepungua hadi kufikia asilimia 7.9 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 16.0 iliyofikiwa mwaka katika mwaka 2012.
Akitoa tathmini ya hali ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Desemba 2013 na ule wa mwaka mzima kuanzia mwezi Januari 2013, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa kupungua kwa mfumuko wa bei nchini kunatokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali nchini.
Amesema mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Desemba umepungua hadi kufikia asilimia 5.6 kutoka 6.2 za mwezi Novemba 2013 na kubainisha kuwa hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na migahawani umepungua hadi asilimia 6.6 mwezi Desemba 2013 ikilinganishwa na asilimia 7.6 za mwezi Novemba 2013 huku mfumuko wa bei kwa bidhaa zisizo za vyakula umepungua hadi asilimia 5.5 kwa mwezi Desema 2013 kutoka aslimia 5.7 za mwezi Novemba 2013.
Bw. Kwesigabo amefafanua kuwa mwenendo wa bidhaa zote za 224 zinazotumika kupimia mfumuko wa bei nchini unaonesha kuwa bidhaa za vyakula zimechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa mfumuko wa bei.
Akieleza kuhusu matokeo ya mfumuko wa bei unaopimwa kwa kigezo cha mwezi amesema takwimu zinaonyesha ongezeko la asilimia 1.3 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.6 kama ilivyokuwa mwezi Novemba huku fahirisi za bei zikiongezeka hadi kufikia 144.07 mwezi Desemba kutoka 141.23 za mwezi Novemba na kubainisha kuwa ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Amesema baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi kuwa ni pamoja na mchele kwa asilimia 0.2 , vitafunwa kwa asilimia 2.4, mahindi kwa asilimia 1.4, unga wa mahindi kwa asilimia 1.6, unga wa muhogo kwa asilimia 3.0 , kuku wa kienyeji kwa asilimia 1.5 na dagaa kwa asilimia 2.1.
Bidhaa nyingine ni pamoja na nazi kwa asilimia 11.5, mbogamboga kwa asilimia 5.8, nyanya asilimia 8.3, njegere asilimia 12.6, maharage kwa asilimia 3.7 mihogo kwa asilimia 5.1 na viazi vitamu kwa asilimia 7.2 wakati zile zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi ni pamoja na vitambaa vya suruali kwa asilimia 1.2, blauzi asilimia 1.2, huduma za kufua nguo kwa asilimia 3.6, gesi kwa asilimia 3.4, mafuta ya taa asilimia 2.1, mkaa asilimia 4.0, mazulia na vifaa vingine vya kufunikia sakafu kwa asilimia 1.7, mafuta ya dizeli asilimia 1.3, Petroli asilimia 0.2 , huduma za usafi wa nywele pamoja na usafi binafsi kwa asilimia 1.2.
Bw. Kwesigabo ameongeza kuwa mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula kwa mwezi Desemba 2012 na Desemba 2013 mathalani mchele bei imeonyesha kupungua kwa asilimia 26.6 huku bidhaa nyingine kama mahindi zikipungua kwa asilimia 9.3, unga wa mahindi 4.4, viazi mviringo 6.3 na karanga kwa asilimia 9.7.
Aidha ameeleza kuwa thamani ya shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Desemba 2013 umeonyesha kuwa imara kufikia shilingi 69 na senti 41.
“Napenda niwahakikishie kuwa fahirisi za bei za Taifa zimeonyesha kuwa na mwelekeo imara kwa kipindi chote, kwa hiyo uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeonyesha kuwa na mwelekeo imara kwa kufikia shilingi 69 na senti 41 ” amesema.
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umefikia asilimia 7.15 mwezi Desemba kutoka asilimia 7.36 za mwezi Novemba, huku nchini wa Uganda ukifikia asilimia 6.7 kwa mwezi Desemba kutoka asilimia 8.7 za mwezi Novemba.
No comments:
Post a Comment