TANGAZO


Wednesday, January 8, 2014

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Sadiki akiongoza Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa jijini leo

 Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmando, akizungumza wakati alipokuwa akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam (RCC), leo. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Sadiki. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Wakuu wa Wilaya, Sophia Mjema- Temeke (kushoto), Jordan Rungimbana (katikati), wa Kinondoni.
Baadhi ya wabunge wa Majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa katika kikao hicho jijini leo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa, Saidi Sadiki, akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, wakati alipokuwa akikifungua kikao chao cha kujadili kero mbalimbali mkoani humo, katika ukumbi wa ofisi yake, Dar es Salaam leo. Kulia ni Naibu Waziri wa Kazi na Mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga na katikati ni Mwenyeiti wa Chama Cha Mapinduzi, mkoani humo, Ramadhani Madabida.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa, Saidi Sadiki, akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, wakati alipokuwa akikifungua kikao chao cha kujadili kero mbalimbali mkoani humo, katika ukumbi wa ofisi yake, Dar es Salaam leo. Kulia ni Naibu Waziri wa Kazi na Mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga na katikati ni Mwenyeiti wa Chama Cha Mapinduzi, mkoani humo, Ramadhani Madabida.
Baadhi ya Wabunge wa Viti Maalum, wakiwa katika kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Dar es Salaam, mara baada ya mkuu wa Mkoa kukifungua kikao cha kamati hiyo leo.
 Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wakiwa katika kikao chao kujadili kesro za jijini leo.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Ushauri, wakiwa katika kikao chao leo.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho, wakiwa katika kikao cha kujadili kero za jiji hilo leo.
 Wajumbe wa kikao cha Kamati hiyo, wakiangalia makabrasha yao kwa ajili ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza leo.
 Baadhi ya wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho jijini leo.
 Mkuu wa Mkoa akikifungua kikao cha Kamati hiyo, jijini leo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meki Sadiki, akizungumza wakati akikifungua jijini leo.
Mkuu wa Mkoa akizungumza na baadhi ya viongozi wa mkoa huo leo.
 Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo jijini leo.
Baadhi ya waandishi wa habari, wakiwa kwenye mkutano wa Kamati ya ushari ya mkoa wa Dar es Salaam leo.
 Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ushauri (RCC), wakiwa kwenye kikao chake jijini leo.
Mbunge wa viti maalum, (CCM), akichangia hoja wakati wa kikao hicho jijini leo. 
 
 Baadhi ya wajume wakiangalia makabrasha yao, ili kubaini makosa katika muhutasari wa vikao vilivyopita vya Kamati hiyo.
 Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu akizungumza wakati akitoa ushauri kwenye kikao cha kamati hiyo jijini leo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa, Saidi Sadiki akikiongoza kikao hicho, wakati wa mkutano wao huo leo.
Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu akizungumza katika kikao cha Kamati hiyo jijini leo.
 
HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM KWENYE UFUNGUZI WA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA MKOA (RCC) TAREHE 08 JANUARI, 2014 KWENYE UKUMBI WA OFISI YA MKUU WA MKOA

Mhe. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa,

Mhe. Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa,

Katibu Tawala wa Mkoa,

Wahe. Wakuu wa Wilaya,

Wahe. Wabunge,

Wahe. Wastahiki Mameya,

Wakurugenzi wa Halmashauri,

Wakuu wa Taasisi,

Wawakilishi wa madhehebu ya dini,

Wawakilishi wa vyama vya siasa,

Maafisa mbalimbali wa Mkoa na Halmashauri

Waandishi wa habari

Waalikwa Wote,

Mabibi na Mabwana.

Ninapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha katika kikao chetu cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na pia kuwatakia Kheri ya Mwaka Mpya wa 2014. Kikao hiki ni muhimu siyo tu kwa vile kipo kwa mujibu wa Sheria bali pia kinatupatia fursa ya kujadili masuala mbalimbali yaliyotekelezwa katika Mpango na Bajeti ya Mkoa wetu kwa mwaka 2012/13 na kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2013/2014.

Kama mnavyofahamu, majukumu ya Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ni pamoja na kutoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali na utekelezaji wa mipango ya maendeleo, bajeti, kupokea na kutathmini taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya Kitaifa, Programu za Maendeleo na shughuli zingine zote zinazohusu Mkoa. RCC pia inalo jukumu la kuratibu masuala yote ya uchumi na maendeleo ya Mkoa na kuhakikisha kuwa yanafanyika ipasavyo.

Ndugu Wajumbe,

Katika kikao hiki tutajadili agenda zilizoandaliwa pamoja na mambo mengine muhimu yatakayojitokeza katika kikao hiki. Lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi ndani ya Mkoa wanapatiwa huduma bora na zinazotosheleza. Kufanya hivyo tutakuwa tumetenda haki kwa wananchi na dhamana tuliyopewa kama viongozi ikiwa tutatimiza wajibu wetu ipasavyo. Aidha, tungependa pia katika kikao hiki tujadili mambo muhimu ambayo ni pamoja na Agenda ya eneo maalumu linalopendekezwa kutengwa kwa ajili ya udhibiti taka na uchafu i.e Usafi Jijini (Smart Area) na Mapendekezo ya kupanua maeneo ya Utawala Mkoani Dar es Salaam. Agenda hizi hazikuweza kuwasilishwa mbele yenu kutokana na kutokamilishwa kwa mchakato na taratibu za kuwasilishwa na kujadiliwa katika Vikao vya ngazi ya Halmashauri zetu.  Mambo hayo ni muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa Mkoa wetu, hivyo Halmashauri zetu kuchelewa kujadili agenda hizo kunaturudisha nyuma katika jitihada za kuwaletea wananchi huduma bora.

Ndugu Wajumbe,

Pamoja na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali, Taasisi na wadau mbalimbali bado tuna changamoto zinazotukabili.  Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na:-

·        Jiji letu la Dar es Salaam bado ni chafu; pamoja na jitihada zinazofanyika bado hali ya usafi hususani katika maeneo ya makazi, masoko, biashara, machinjio na vituo vya mabasi hairidhishi.

·        Uwepo wa watoto wanaoishi mitaani na katika mazingira hatarishi; hii ni pamoja na ombaomba.  Makundi haya yana athari ya uchafuzi wa mazingiara na hadhi ya Jiji.

·        Uwepo wa wafanya biashara ndogo ndogo wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi ni chanzo cha ukwepaji kodi na pia ni wachafuzi wakuu wa Jiji na kero kwa wenye biashara rasmi na kufanya Jiji kukosa ustaarabu.

·        Miundombinu isiyotosheleza utoaji wa huduma za Maji, elimu, afya na Usafiri changamoto imeongeza malalamiko kwa Serikali kutofanya vizuri.

·        Kuendelea kuwapo kwa vifo vya akina mama na watoto na maambukizi ya VVU/UKIMWI.

·        Kasi ya ongezeko la idadi ya watu lisiloenda sambamba na kasi ya upanuzi wa huduma za kijamii kama vile Elimu, Afya, Viwanja vya makazi na shughuli nyinginezo.
Ndugu Wajumbe,
Changamoto nilizozieleza ni baadhi tu kati ya nyingi na zimekuwa ni kikwazo kwa  Ustawi wa Jamii yetu, hivyo  zinapaswa kutafutiwa majawabu ya kuziondoa ili kuifanya Jamii iweze kuwa na maisha bora. 

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Mkoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa wakishirikiana na wadau wengine wamekuwa wakiandaa mipango na bajeti katika mtazamo wa kukabiliana nazo na hatimaye kuziondoa changamoto hizi. Miongoni mwa taarifa zitakazowasilishwa leo ni pamoja na mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2012/13 na utekelezaji wa Robo ya I mwaka 2013/14.  Ni matumaini yangu kwamba, wajumbe watapata fursa ya kutathmini ni kwa kiwango gani tutafanikiwa katika kukabiliana na baadhi ya changamoto na hatimaye kutoa ushauri pale panapohitaji kuboreshwa zaidi. Pia tutapokea na kujadili vipaumbele vya mpango na bajeti kwa mwaka 2014/15 ambavyo vitatupa mwelekeo wa makadirio ya mpango na Bajeti kwa mwaka 2014/15 ambayo yatawasilishwa baada ya kupata Ukomo wa bajeti (Ceilings), kukamilisha vitabu na kupitishwa kwa mipango na bajeti hizo katika vikao vya kisheria vya Halmashauri.

Ndugu wajumbe,
Nafasi tuliyopewa kama Kamati ya Ushauri ya Mkoa ni dhamana kubwa na hivyo hatuna budi kujadili na kufanya maamuzi yenye tija kwa Jamii.  Aidha katika kikao hiki pia kitapokea taarifa ya huduma ya maji safi na taka, huduma za Mama na Mtoto Mkoani kwetu, taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), taarifa ya ukaguzi wa shule, Mikakati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ndani ya Mkoa katika kuwapatia nafasi wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2014 pamoja na taarifa ya utekelezaji wa mkakati wa kupunguza msongamano katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Ni matarajio yangu kwamba wajumbe watapokea na kuchambua taarifa hizi na pia kutoa ushauri pale panapohitajika.
 
Aidha nichukue nafasi hii kuwapongeza sana walimu, wazazi na walezi kwa jitihada walizofanya kuwasimamia wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi mwaka 2013 ambapo ufaulu wa Mkoa ulikuwa 75.19% na kuchukua nafasi ya kwanza Kitaifa.  Kwa ufaulu huo tunayo changamoto ya kuwapatia nafasi za Sekondari wanafunzi wote waliofaulu.
Ndugu wajumbe,
Mipango mizuri bila utekelezaji mzuri haina maana, hivyo natoa wito kwa kila mmoja wetu na kwa nafasi na dhamana aliyonayo kwa Jamii kuhakikisha kwamba anatimiza wajibu wake kikamilifu.
Mwisho napenda kuwatakia majadiliano mema katika kikao hiki. Sasa natamka rasmi kuwa kikao kimefunguliwa.
Asanteni,

No comments:

Post a Comment