Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Waziri Mkuu wa Finland, Bw. Jyrki Katainen alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ziara ya siku moja. Mazungumzo yao yaligusia zaidi katika uhusiano na ushirikiano katika nyanja mbali mbali za kijamii.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na Waziri Mkuu wa Finland Bwana Jyrki Katainen na kufanya mazungumzo kuhusu uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na Finland.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Zanzibar Dk. Shein ameishukuru Serikali ya Finland kwa misaada yake mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa kwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Alibainisha kuwa uhusiano mzuri kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Finland imeiwezesha Zanzibar kupokea misaada katika nyanja mbalimbali za maendeleo, huduma za jamii na hifadhi ya mazingira.
Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na uamuzi wa Serikali ya Finland kuendeleza ushirikiano wake na Zanzibar kwa kuendeleza mradi wa uhifadhi wa ardhi na mazingira kwa Awamu ya Pili (SMOLE II) baada ya kumalizika kwa Awamu ya Kwanza.
Alisifu pia uamuzi wa Serikali ya nchi hiyo kusaidia chuo Kikuu cha Taifa SUZA na kueleza kuwa msaada kwa chuo hicho ambacho ni kichanga una umuhimu wa kipekee kwa kuwa unasaidia kukijengea uwezo.
Dk. Shein amekaribisha wazo la kushirikiana na Finland katika kutekeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kutafuta njia mbadala za kupata nishati ya umeme.
Alieleza kuwa ni kweli hivi sasa Zanzibar inapata umeme wa kutosha kupitia mkonga wa umeme toka Tanzania Bara lakini haitakuwa ajabu baada ya miaka michache ijayo kutokana na kasi ya ongezeko la matumizi ya umeme yanayotakana na kasi ya ukuaji wa uchumi kiasi kilichopo sasa kikawa hakitoshi hivyo ni jambo la busara kuwa na mpango mbadala wa kupata nishati hiyo.
Dk. Shein alimueleza Waziri Mkuu wa Finland kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ingependa kuona ushirikiano zaidi katika maeneo mapya hasa utalii kwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na kuongeza kuwa wawekezaji wa nchi hiyo watumie fursa zilizopo kuwekeza katika sekta hiyo ili kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Finland.
Akijibu pongezi kutoka kwa Waziri Mkuu huyo kuhusu mafanikio yake katika kuiongoza Zanzibar chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio hayo yamewezekana kutokana na ushirikiano wa viongozi Serikalini bila kujali tofauti za vyama wanavyotoka.
Halikadhalika alisema hali ya utulivu na amani imeiwezesha Serikali kupata fursa nzuri kutekeleza majukumu yake ya kuleta maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi wake.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Finland Bwana Jyrki Katainen amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mafanikio aliyoyapata katika kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Mfumo Umoja wa Kitaifa.
Amesema mfumo huo unasaidia kuleta maelewano baina ya vyama na uzoefu unaonyesha kuwa utamaduni wa uendeshaji wa Serikali kwa mfumo kama huo na mingine inayofanana na huo unatumika sana hivi sasa.
Alimueleza Dk Shein kuwa amefurahi kuona Zanzibar imeendelea kuwa katika hali ya utulivu hivyo kuvutia wageni wengi kutembelea visiwa hivyo.
Alibainisha kuwa Zanzibar iko katika nafsi nzuri kuendeleza sekta ya utalii sio tu katika kuvutia watalii kutoka nchini kwake bali hata kwa uwekezaji katika sekta hiyo kulingana na jiiografia yake kuwa karibu na Finland kuliko maeneo mengine ya kitaalii nje ya bara la Ulaya.
Bwana Katainen alimueleza Rais kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Zanzibar katika jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na baadhi ya mawaziri wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulwahid Fereji na Waziri wa Nishati na Madini wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Sospeter Muhongo.
No comments:
Post a Comment