Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akimpa pole mjane wa marehemu Balozi Isaac Sepetu, Mama Miriam Sepetu, alipofika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Mnazi mmoja Mjini Unguja, kuuaga mwili wa marehemu leo asubuhi. (Picha na Ramadhan Othman Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akitia saini kitabu cha maombolezo ya marehemu Balozi Isaac Sepetu, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Mnazi Mmoja, Mjini Unguja leo asubuhi. Marehemu Balozi Sepetu alifariki juzi, jijini Dar es Salaam na kuzikwa Kijiji kwao, Mbuzini, Wilaya Magharibi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akiuaga mwili wa marehemu Balozi Isaac Sepentu, katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo asubuhi. Marehemu alifariki juzi jijini Dar es Salaam na atazikwa Kijiji kwao, Mbuzini Wilaya Magharibi.
Baadhi ya wananchi mbalimbali wakiwa katika sehemu maalum nje ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo, wakisubiri kuuaga mwili wa marehemu Balozi Isaac Sepetu, ambao utazikwa Kijiji kwao, Mbuzini Wilaya Magharibi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa na viongozi wengine akiwemo Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilali katika mazishi ya marehemu Balozi Issac Abraham Sepetu, yaliyofanyika kijijini kwao, Mbuzini Wilaya ya Magharibi Unguja leo.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Balozi Issac Abraham Sepetu, likiwa limebebwa na Askari Polisi na kulifikisha katika kaburi lake yalipofanyika mazishi kijijini kwao, Mbuzini Wilaya ya Magharibi Unguja leo.
Padri wa Kanisa Katoliki la Minara miwili Mjini Zanzibar, Cosmas Amani Shayo, akiuombea mwili wa marehemu Balozi Issac Abraham Sepetu, wakati wa mazishi yake, yaliyofanyika kijijini kwao, Mbuzini Wilaya ya Magharibi Unguja leo.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Balozi Issac Abraham Sepetu, ukiteremshwa katika kaburi wakati wa mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwao Mbuzini Wilaya ya Magharibi Unguja leo.
Na mwandishi wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaongoza viongozi na mamia ya wananchi wa Zanzibar katika mazishi ya mwanasiasa na mwanadiplomasia mkongwe Balozi Issac Abraham Sepetu yaliyofanyika huko kijijini kwake Mbuzini, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi unguja.
Serikali katika salamu zake zilitolewa
na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed imesema
kuwa Marehemu Balozi Sepetu atabaki katika nyoyo za wananchi wa Zanzibar na
Tanzania kwa jumla kutokana na mchango wake katika kulitumikia
Taifa.RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaongoza viongozi na mamia ya wananchi wa Zanzibar katika mazishi ya mwanasiasa na mwanadiplomasia mkongwe Balozi Issac Abraham Sepetu yaliyofanyika huko kijijini kwake Mbuzini, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi unguja.
Waziri Aboud
alimuelezea Balozi Sepetu ambaye katika uhai wake alishika nafasi mbali mbali
katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kuwa mtu aliyeitumika nchi yake kwa uadilifu na uaminifu mkubwa hivyo
msiba huo si wa familia tu bali kwa wananchi wote wa Zanzibar na
Tanzania.
Alisema
Serikali na wananchi wa Zanzibar wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa
hayati Balozi Sepetu na kuwaomba wanafamilia kuwa na moyo wa subira katika
kipindi hiki kigumu cha maombolezi.
Akitoa salamu
za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mazishi hayo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe alisema
Rais Jakaya Mrisho wa Kikwete ameguswa sana na kifo cha Balozi Sepetu ambaye
aliwahi kufanya nae kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje kwa miaka
kumi.
Alisema kifo
chake ni pigo kwa taifa na daima watanzania watamkumbuka sana Balozi Sepetu na
kubaki katika nyoyo zao kutokana na utumishi wake bora kwa
taifa.
Akisoma wasifu
wa Balozi Sepetu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitega Uchumi-ZIPA nchini Khamis
Salum alieleza kuwa maraeehmu Balozi Sepetu alizaliwa tarehe 16 Oktoba, 1943
huko Tabora alipata elimu yake ya msingi na sekondari katika skuli ya Mtakatifu
Joseph mjini Unguja ambayo sasa inaitwa Tumekuja.
Mwaka 1966
alikwenda iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa masomo hadi mwaka 1970 ambapo
alihitimu shahada ya pili katika Uchumi na sayansi ya siasa. Aliporejea nyumbani
aliteuliwa kushika nafasi ya Meneja Msaidizi Mkuu wa Shirika la Shirika la
Biashara Zanzibar BIZANJE.
Kabla ya kwenda
masomoni nchini Ujerumani marehemu alifanyakazi katika Idara ya Habari na
Utangazaji Zanzibar na aliwahi kuwa Mhariri Msaidizi wa Gazeti la Kweupe
ambalo llianzishwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani
Karume.
Balozi wa
Sepetu aliwahi kushika nyadhifa za Naibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa
Habari na Utalii katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi wa
Tanzania katika Shirikisho la nchi za Kisoshalisti la Kisovieti wakati huo na
Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo wakati huo ikiitwa Zaire.
Katika Serikali
ya Zanzibar aliwahi kuwa Kamishna wa Tume ya Mipango, Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango.Mwaka 2000
alichaguliwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki hadi mwaka 2005. Hadi anaaga
dunia Balozi Sepetu alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya ZIPA.Marehemu Balozi Sepetu ameacha wajane wawili, watoto na wajukuu.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na wageni mbalibali kutoka Tanzania bara.
wakati huo huo mamia ya
wakaazi wa mji wa Zanzibar walitoa heshma zao za mwisho kwa mwili wa marehemu
Balozi Issac Abraham Sepetu mapema asubuhi huko katika ukumbi wa zamani wa
Baraza la Wawakilishi uliopo mjini Unguja.
Mwili wa marehemu uliwasili kwa boti mapema
asubuhi ukitokea Dar es Salaam ambako Balozi Sepetu mauti
yalimkuta.
Baadae mwili ulipelekwa katika Kanisa la Roma
la Minara Miwili lililopo Shangani mjini hapa kwa misa.
No comments:
Post a Comment