TANGAZO


Monday, September 16, 2013

Wadau watoa wito wa kuendeleza Kilimo cha Pamba kwa mafanikio

 Shamba la Pamba likiwa limenawiri pamoja na mazao yake.
Pamba ikiwa kwenye kikonyo chake.

Na Mwandishi Wetu Dar es Salaa 
Wataalamu wa sekta ya pamba nchini wamesema kwamba iwapo wakulima wa pamba watasaidiwa kuendeleza Kilimo cha Mkataba na kuwa endelevu, kilimo hicho kitabadilisha maisha yao.
Mkaguzi wa pamba wa kutoka katika wilaya ya Bunda, Bw Igore Manonga, amesema hivi karibuni kuwa kuanzishwa kwa Kilimo cha Mkataba takribani miaka mitano iliyopita imekuwa faida kwa wakulima hivyo kuna haja ya kuendeleza na kuzifanyia kazi changamoto zilizopo.
Kiasi cha wakazi wa vijijini wapatao takribani 500,000 wanategemea maisha yao moja kwa moja kwenye sekta hiyo ya pamba.
“Kwa mfano uzalishaji wa pamba wilayani Bunda, umeongezeka kutoka wastani wa kati ya kilo 250 na kilogramu 300 kwa ekari moja kabla ya kuanzishwa kwa Kilimo cha Mkataba lakini kwa msimu wa soko mwaka 2010 –uzalishaji uliongezeka zaidi kutoka kilo 300 hadi kufikia kilo 600  kwa ekari moja,” anasema Bw. Manonga na kuongeza kuwa kuna baadhi ya wakulima ambao huzalisha hadi kilo 1,000 kwa ekari kutokana na mpango huo wa Kilimo cha Mkataba.
Aidha, kwa mujibu wa mkaguzi wa pamba toka wilayani Butiama, Bw Alphone Ngewagale, anasema kuwa karibu kila wilaya ambapo mradi wa awali wa Kilimo cha Mkataba ulipokuwa unafanyika, uzalishaji wa pamba kwa ekari umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kimsingi, Kilimo cha Mkataba kinahusu uzalishaji wa kilimo unaofanywa kulingana na makubaliano kati ya mnunuzi na wakulima.
Mkataba huu wa Kilimo cha Mkataba unaanzisha masharti kwa ajili ya uzalishaji na masoko ya pamba ambapo wanunuzi - ambao mafadhalani kwa Tanzania ni Wasindikaji wa pamba - huwapatia wakulima mikopo kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo za kilimo (mbegu na madawa ya kuulia wadudu ) kama vile ushauri wa kitaalamu. Kwa upande mwingine wakulima huuza pamba yao kwa wasindikaji.
Hata hivyo, Bw. Manonga, anasema kuwa kuna changamoto nyingi ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka.
Aidha anasema kuwa moja ya masuala ambayo wanakabiliana nayo ni kwamba wakati mwingine , wasindikaji hushindwa kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa wakati.
“Kwa mfano, wakulima wanatakiwa kupokea mbegu za pamba kutoka kwa wasindikaji Oktoba 15 lakini kwa nyakati fulani hupokea mbegu mwezi Desemba ..... vivyo hivyo, wakulima wanatakiwa kupokea madawa ya kuulia wadudu mwezi Januari 15, tumeshayasikia matukio kuwa wasindikaji huleta dawa zikiwa zimchelewa na kufika mwezi Februari na wakati mwingine hata Machi .... kuna haja ya kulifanyia kazi suala hili,” anasema Bw. Manonga.
Kwa mijibu wa taarifa ya kila mwezi ya uchumi inayotolewa na Benki Kuu nchini kwa mwezi Julai 2013 –Tanzania ilipata kiasi cha Shilingi bilioni 254.4 (dola za kimarekani Milioni 159.3) kutokana na mauzo ya pamba kwa mwezi Juni mwaka 2013.
Hivi sasa, Tanzania ni nchi ya nne barani Afrika kwa uzalishaji wa pamba baada ya nchi ya Mali, Burkina Faso na Misri –ambazo zinaongoza kwa kilimo cha zao hilo duniani hii ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO).

Kuna zaidi ya makampuni 40 ya usindikaji wa pamba sambamba na takribani watu zaidi ya milioni 14 ambao wameajiriwa kwenye sekta hiyo, na hivyo kuna haja kwa serikali kuimarisha uwepo wa Kilimo hicho cha Mkataba kama ilivyo kwenye nchi za; Zambia, Msumbiji na Zimbabwe.

No comments:

Post a Comment