Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akitoa tamko la ushirikiano wa Vyama vya upinzani, Dar es Salaam leo, vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kuhusu mustakabali wa mchakato wa Katiba Mpya kufuatia kile walichodai kupitishwa kinyemela kwa muswaada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013. Wanne kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wa tano) na wengine pichani ni baadhi ya viongozi waandamizi wa vyama hivyo. (Picha na Kassim Mbarouk)
Na Claudia Kayombo
VYAMA vya upinzani, vimetoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kutosaini muswada wa marekebisho ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 kwa kuwa utaratibu uliotumika kuupitisha ni kinyume cha dhamira na dhima ya majadiliano aliyofanya na vyama hivyo.
Badala yake vimemtaka arejeshe muswada huo bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuamiana na muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba mpya.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akisoma tamko la pamoja la ushirikiano wa vyama hivyo ambapo licha ya CUF vingine ni NCCR Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano baina yao na wanahabari.
Alisema katika jambo la Katiba Rais Kikwete anatakiwa ahakikishe jambo hilo anaweka mbele maslahi ya taifa na si ya chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Viongozi hao wa vyama hivyo vya upinzani wamemhadhalisha Rais kuwa awe makini katika hilo isije mkono wake ukalitumbukiza taifa katika machafuko.
Profesa Lipumba alitanabaisha kuwa katika hilo wameanza kuunganisha umma kufanya maamuzi ya kunusuru mchakato wa Katiba mpya kuendelea kutekwa na kuhodhiwa na CCM kwa kuzingatia kwamba madaraka na mamlaka yote ni wananchi na Serikali inapaswa kuwajibika kwao.
"Tunapongeza na kuunga mkono hatua ya wabunge wa vyama vyetu kuweka pembeni tofauti zao na kutumia njia za kibunge kutaka mjadala wa muswada huo usiendelee bungeni kwa lengo la kuhakikisha masuala muhimu kwa niaba ya wananchi yanazingatiwa.
"Vyama vyetu vimeamua kuendeleza ushirikiano huo kwa kuweka pembeni tofauti zetu na kuunganisha nguvu za pamoja kunusuru mchakato wa Katiba mpya kwa maslahi ya wananchi na nchi kwa ujumla.
"Tunalani ukiukwaji wa kanuni za Bunge na mila na desturi za kibunge uliofanywa wa kuingiza vifungu vipya kinyemela, kukiuka masharti ya kushughulikia madai ya taarifa za uongo kutolewa bungeni.
"Kuzuiwa kwa wabunge wa upinzani kusema kuhusu masuala na kutoa hoja za kusimamia haki na taratibu za kibunge, kushambuliwa kwa baadhi ya wabunge, pamoja na kudhalilishwa kwa hadhi ya Bunge kwa ujumla,"alisema Pro. Lipumba
Aliongeza kuwa sasa vyama hivyo vimeanza kuunganisha umma kufanya maamuzi ya kunusuru mchakato wa Katiba mpya kuendelea kutekwa na kuhodhi .
Aidha alisema wanakusudia kufanya mkutano wa hadhara wa pamoja kwenye Uwanja wa Jangwani Dar es Salaam Septemba 21 mwaka huu ambao utakuwa ni atua za mwanzo kwenda kwa wananchi.
"Njia zitakazotumika kuunganisha wananchi kuchukua hatua na ratiba ya vyama kuzunguka katika maeneo mengine nchini ni kati ya masuala yatakayoelezwa katika mkutano huo,"alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema madai kuwa vyama vya upinzamni vinalenga kuharibu mchakato wa Katiba Mpya hayana ukweli.
Mbatia alisema hawawezi kufanya hivyo kwa sababu wao ndiyo waliokuwa wakitoa hoja za kuundwa Katiba mpya kutoa mwanzo wa vyama vingi.
Alisema Katiba ni tamko la umma kinachotakiwa Watanzania kuzika tofauti zao na kuandika Katiba yenye maslahi kwa umma wa Watanzania.
"Ndiyo maana tunakiitaka CCM na wadau wengine tuweke tofauti zetu za kiasiasa pembeni tulete maridhiano, ili tupate Katiba mpya itakayodumu miaka 50 hadi 100 ijayo,"alisema Mbatia.
Alisema rasimu ya Katiba ina mambo mazuri ikiwemo haja ya kuwepo Serikali tatu ambayo Cham Cha Mapinduzi inaogopa.
"Tume ya Jaji Warioba imefanya kazi nzuri sana rasimu ni nzuri tunachotakiwa ni kuilinda,"alisema
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa rai kwa wanahabari kuwa wao ni wadau wakubwa mno katika mchakato huo kwa kuwa wanaweza kuchochea Katiba nzuri ya Watanzania.
Alisema wanahabari wanaitikadi zao hata hivyo katika mchakato wanatakiwa kuweka pembeni tofauti zao ili kupatikana Katiba isiyo hodhiwa na chama chochote cha siasa wala taasisi.
Alisema katika hilo Watanzania wakiwemo viongozi wa dini wanapaswa kuwa kitu kimoja na kwamba kwa kuwa ni jambo jema hana shaka Mungu ataliwekea mkono wake litafanikiwa tu.
No comments:
Post a Comment