Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabara Mkoa wa Iringa, Salim Asas akiahidi kutoa mafunzo kwa mdereva wa bodaboda wa mjini Iringa wasio na uwezo(hawapo pichani) na kuwapatia pikipiki moja kwa ajili ya ulinzi shirikishi (Picha na Francis Godwin)
Na Francis Godwin, Iringa
MWENYEKITI wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salim Asas ameahidi kutoa msaada wa pikipiki kwa madereva bodaboda mjini Iringa kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano na jeshi la Polisi kupitia dhana ya polisi jamii na ulinzi shirikishi.
Asas ametoa ahadi hiyo jana baada ya kufurahishwa na jitihada zinazofanywa na madereva wa bodaboda mjini Iringa katika kupambana na vitendo vya uhalifu .
Alisema kuwa pikipiki hiyo ataitoa kwa madereva hao kupitia chama chao, Asas alisema kuwa amevutiwa zaidi na umoja uliopo kwa madereva hao boda boda mjini Iringa na kuwa katika kuwauga mkono zaidi ili vijana hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa polisi katika kupambana na vitendo vya uharifu mkoani Iringa atawapatia pikipiki hizo kwa ajili ya kufanya shughuli za ulinzi.
Pia Asas aliahidi kutoa ufadhili wa mafunzo ya udereva kwa madereva wa bodaboda wasio na uwezo baada ya kuelezwa kwamba baadhi yao wameshindwa kushiriki mafunzo hayo kutokana na ukosefu wa fedha.
“Pikipiki hii itakayotumiwa na uongozi wenu wa bodaboda kusaidia shughuli za ulinzi shirikishi ili kuufanya mji wetu na mkoa kuwa salama zaidi"
Kwa upande wake mgeni rasmi katika Hafla hiyo ya ufungaji wa mafunzo ya udereva kwa madereva bodaboda, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa (RPC), Ramadhani Mungi mbali kupongeza jitihada za Asas pia aliagiza askari aliyetajwa kwa jina moja la Chande aondolewe mara moja kwenye kitengo cha askari wa pikipiki wa mjini hapa baada ya kutuhumiwa na madereva boda boda hao kuwa anawasumbua .
Alichukua hatua hiyo baada ya madereva hao kumshitaki askari huyo kwamba anavunja heshima ya askari wenzake na ya jeshi hilo wakimtuhumu kukithiri kwa vitendo vya kudai rushwa.
Tuhuma dhidi ya askari huyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Bodaboda Manispaa ya Iringa, Mwambope Joseph wakati madereva 150 wa bodaboda wakikabidhiwa vyeti vyao vya kumaliza mafunzo ya wiki moja ya udereva wa pikipiki.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Afande Steven Nyandongo kwa kushirikiana na Chuo cha Udereva Iringa (Iringa Driving School) yalihusu sheria za usalama barabarani, alama na michoro ya barabarani, nidhamu ya mdareva, udreva wa kujihami, vyanzo vya ajali na tahadhari na utunzaji wa pikipiki.
Akiwatunuku vyeti vyao, RPC Mungi alisema shughuli ya bodaboda ina sura tatu amabzo ni ajira, biashara na huduma na kwamba uwepo wake unategemea kanuni, taratibu na sheria za nchi.
Akitangaza kukipokea kilio chao alisema “kuanzia leo askari Chande simtaki; apewe kazi nyingine; aondolewe mara moja kwenye kitengo cha askari wa pikipiki, simtaki, simtaki.”
Alisema katika kujenga mahusiano mazuri na madereva wa bodaboda ataendelea kupokea na kuyashughulikia matatizo yao kiungwana.
Alisema katika kuyashughulikia matatizo ya kila siku ya bodaboda, ofisi yake imeanzisha kitengo maalumu cha bodaboda kinachoratibiwa na Afande Zakaria Benard.
Katika taarifa yake kwenye hafla hiyo, Benard alisema kumekuwepo na ongezeko la ajali za bodaboda kutoka nane mwaka jana hadi 26 Septemba mwaka huu.
Alisema vinavyosababishwa na ajali hizo navyo vimeongezeka kutoka saba mwaka jana hadi 23 Septemba mwaka huu.
Alisema baada ya madereva hao kupatiwa mafunzo, tathimini itakuwa ikifanywa kila mwaka ili kuona kama kuna mabadiliko.
|
No comments:
Post a Comment