Meneja wa Kanda ya Mashariki kutoka Mfuko
wa Pensheni wa LAPF Sayi Lulyalya(katikati) akieleza kwa waandishi wa habari
kuhusu Mafao na Miradi mbalimbali inayotekelezwa na mfuko huo,wakati wa mkutano
uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO leo, jijini Dar es
Salaam.Kushoto ni Afisa uhusiano wa Mfuko huo Andrew Kuyeyana na kulia ni Afisa
Habari wa Idara ya Habari Fatma Salum.
(Picha
na Frank Mvungi- Maelezo)
Na Fatma Salum na Hassan Silayo- MAELEZO
Mfuko wa pensheni wa LAPF unatarajia
kutumia kiasi cha shilingi bilioni 35 katika mradi wa kituo cha mabasi eneo la
msamvu Mkoani Morogoro.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo, Meneja wa mfuko huo Kanda ya Mashariki, Sayi
Lulyalya alisema mradi huo ambao ni ubia kati ya Manispaa ya Morogoro na mfuko
wa LAPF unatarajiwa kuanza wakati wowote mwaka huu.
Sayi alisema hatua za awali za utekelezaji
wa mradi huo ambao utakamilika baada ya miezi 18 zimeshaanza kwa kuzungushia
uzio katika eneo la ujenzi wa kituo hicho.
“LAPF imeamua kutenga takriban bilioni 35
za ujenzi wa kituo cha Msamvu na tunashukuru uongozi wa Manispaa ya Morogoro
kwa kutoa eneo la kutosha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na michoro
imeshakamilika na shughuli za zabuni zinaendelea.” Alisema Sayi.
Aidha Sayi aliongeza kuwa mradi huo wa
uwekezaji utahusisha ujenzi wa hoteli yenye hadhi ya nyota tano itakayojengwa
ndani ya eneo la kituo cha mabasi Msamvu ili kusaidia kuongeza mapato ya
serikali.
Mradi wa kituo cha mabasi Msamvu ni
muendelezo wa miradi mingi ya uwekezaji inayotekelezwa na mfuko wa pensheni wa
LAPF ambapo baadhi ya miradi mingine ni ujenzi wa mabweni chuo cha Hombolo,
Kituo cha Afya cha Chuo Kikuu Dodoma, jengo la biashara Mwanza na mradi wa
malori na mabasi wa Mbezi Louis.
No comments:
Post a Comment