TANGAZO


Saturday, August 17, 2013

NSSF yawapiga msasa wafanyakazi wa Sekta isiyo rasmi jijini Dar es Salaam

Ofisa Uendeshaji Mwandamizi wa Sekta Isiyo Rasmi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Salim Khalfan akifafanua jambo kuhusu huduma wanazotoa wakati wa uzinduzi wa Ushirikiano wa Kikazi kati ya Umoja wa Wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi, NSSF, Equity Bank na Sanitas Hospital uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mlezi wa umoja huo, Ramadhani Madabida na Meneja wa Huduma za Wateja wadogo wa benki ya Equity, Janeth Zoya. (Picha na habari kwa hisani ya Habari Mseto Blog)
Baadhi ya Maofisa wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakiwa katika uzinduzi huo.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo, wakisikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa.

DAR ES SALAAM, Tanzania

SHIRIKA La Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limeupongeza Umoja wa Wafanyakazi wa Sekta Zisizo Rasmi (Informo Sector Workers Union -ISWU), huku likiwataka kutumia vema fursa itokanayo na unganiko la kikazi baina ya umoja huo, NSSF, Equity Bank na Sanitas Hospital.

Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Ofisa Mwandamizi Mkuu wa Sekta Zisizo Rasmi wa NSSF, Salim Khalfan, alipokuwa akizungumza na wanachama wa ISWU walioshiriki semina na uzinduzi wa ushirikiano huo chini ya programu ya ‘Community Cooparetive Micro Insuarance (CCMI).’ 

Khalfani aliuambia umoja huo kuwa, NSSF inampongeza Mkurugenzi wa Umoja wa Wafanyakazi wa Sekta Zisizo Rasmi, Dauda Wadauda kwa kuratibu umoja huo na kwamba shirika lake liko tayari kusaidiana katika kuwawezesha kufikia malengo yao kibiashara.

Aliongeza kuwa, uwezo mkubwa wa kusaidia harakati za afya na matibabu kwa wajasiriamali iliyonao shirika lake  ulikuwa unakosa nguvu ya kuwafikia mmoja mmoja miongoni mwa wajasiriamali na kwamba kuungana kwao kunarahisisha NSSF kuwafikia na kuwawezesha.

“Wanachama, mnapaswa kutumia fursa hii kwa kuwekeza kadri muwezavyo pesa zenu katika shirika letu, ili kunufaika na huduma za NSSF, ambayo kwa kushirikiana na Equity Bank na Sanitas Hospital, iko tayari kukabili changamoto zenu za ndani na nje ya ujasiriamali.

Kwa upande wake, Mlezi wa ISWU, Ramadhani Madabida, aliishukuru NSSF kwa kukubali kuungana katika vita dhidi ya umaskini ambao aliutaja kama moja ya vyanzo vinavyochangia ukosefu wa amani katika nchi yoyote duniani na kwamba amani ni uwezo wa kukabiliana na changamoto.

Mkurugenzi wa ISWU, Dauda Wadauda, aliwataka wajasiriamali hao kutumia vema elimu waliyopata katika semina hiyo na kuwataka wawe mabalozi wazuri kwa wajasiriamali walio nje ya umoja huo ili kuongeza idadi yao na kuwa na nguvu ya pamoja.

No comments:

Post a Comment