Baadhi ya Wasanii maarufu wa filamu nchini Tanzania wakisikiliza hotuba fupi iliyokuwa ikitolewa na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi Joyce Fissoo (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo katika ukumbi wa May Fair Plaza, Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wasanii na wageni waalikwa waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa filamu ya “TABIA” wakiwa wameketi wakiangalia filamu hiyo mara baada ya kuzinduliwa rasmi na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania BI. Joyce Fissoo hivi karibuni katika Ukumbi wa May Fair Plaza uliopo eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wasanii wakibadilishana mawazo na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania, Bi Joyce Fissooeni mara baada ya kuizindua filamu hiyo ukumbi wa May Fair Plaza uliopo eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Na Benedict
Liwenga-MAELEZO.
KATIBU mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo
amezindua rasmi filamu mpya iliyoandaliwa na Kampuni ya Harmony iliyopewa jina
la “TABIA” filamu ambayo imelenga kutoa elimu katika jamii hasa kwa vijana wa
kileo.
Uzinduzi wa filamu hiyo ulifanyika hivi karibuni katika
Ukumbi wa Hoteli ya May Fair Plaza uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Katika unzinduzi wa filamu hiyo, Bi Fissoo amebainisha kuwa
filamu ya TABIA imekaguliwa na Bodi ya Filamu na kupewa daraja 13 yaani filamu
hii inaruhusiwa kutazamwa na watu kuanzia miaka 13 na kuendelea.
“Ni filamu inayoweza kuonwa na wanajamii wengi kwani
imejikita katika kuelimisha kuanzia kwa watoto wetu”. Alisema Bi. Fissoo.
Bi Fissoo alisema kuwa hapa nchini ni filamu chache
zinazojikita katika kundi hilo ambazo zinawasilishwa Bodi ukilinganisha na zile
zinazolenga umri wa miaka 18 na kuendelea.
Aidha, Bi Joyce ameipongeza Kampuni ya Harmony kwa kuthubutu
kwao na ana imani kuwa Kampuni hiyo itaendelea kuzalisha filamu bora zenye
weledi, maadili na zinazoweza kuingia katika soko la ushindani.
Bi Fissoo ameongeza kuwa utamaduni ni utambulisho wa jamii
yoyote duniani hivyo mtu anaweza kutambulishwa kwa utamaduni wake, pia amesisitza
kuwa utandawazi na ukuaji wa teknolojia unaweza kunufaisha ama kuathiri
tamaduni na moja ya eneo rahisi ambalo linaweza kutekwa na utandawazi na ukuaji
wa teknolojia hiyo ni tasnia ya filamu, hivyo ameshauri kutengeneza filamu
nzuri na zenye maadili ya kiutanzania.
Kwa upande mwingine Katibu Mtendaji Bi Joyce Fissoo amewaasa
waandaaji wa filamu na watengenezaji filamu wote nchini kutengeneza filamu
zisizodhalilisha, zisizolenga kuuza tu bali ziwe zinazolinda maadili, zenye
kutumia rasilimali, mandhari na lugha yetu ya Kiswahili katika kutangaza utaifa
na utamaduni wetu.
“Hata majina ya filamu zetu ni vema yawe kwa lugha ya
kiswahili, tupende na kuenzi utamaduni, maadili na lugha yetu”. Alisema Bi Fissoo.
Katika hotuba yake hiyo, Bi Joyce aliwasihi wadau wote wa
filamu kuunga mkono juhudi za Serikali za kurasimisha tasnia za filamu na
muziki kwani nia ya urasimishaji huo ni kurejesha nidhamu na hadhi katika
tasnia hizo na kuondokana na kilio cha muda mrefu cha wasanii wengi nchini
kutonufaika na jasho lao.
“Nia ya Serikali ni kuwa na njia bora itakayomwezesha kila
msanii kunufaika na kazi yake aliyoibuni na kuitengeneza”. Alisema Katibu Mtendaji
huyo.
Bi Fissoo alimalizia kwa kuwasihi wadau wote wa filamu nchini
kuheshimu sheria na kanuni zinazosimamia tasnia ya filamu nchini ambapo kwa
sasa mwitikio wake umekuwa mkubwa.
No comments:
Post a Comment