Mkuu wa kitengo cha mawasiliano toka Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mkumbwa ally(Kushoto) akieleza kwa waandishi wa habari juu ya Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi katika mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam katikati ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa na kulia ni Mkuu wa Idara ya Asia na Australasia Balozi Mbelwa Kairuki.
Mkuu wa Idara ya Mashariki ya kati toka Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano Balozi Hassan Simba(Kushoto) akiwaeleza waandishi wa habari sababu za kufungua Balozi za Tanzania nchini Brazil na Malasia, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyikaleo Jijini Dar es Salaam kulia ni Mkuu wa kitengo cha mawasiliano toka Wizara hiyo Bw. Mkumbwa Ally.
Mkuu wa Idara ya Asia na Australasia toka Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano Balozi Mbelwa Kairuki(Kulia)akijibu moja ya maswali ya waandishi wa Habari juu ya Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyikaleo Jijini Dar es Salaam kushoto Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.
Picha zote na Hassan Silayo
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imekuwa inatekeleza Sera
Mpya ya Mambo ya Nje iliyoanza kutumika rasmi 2001. Lengo la sera hii ni kufanya
mageuzi katika sera ya awali ya mambo ya nje ya Tanzania ili iendane na
mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yaliyotokea ndani nan je ya nchi.
Sera mpya inaweka kipaumbele kwenye diplomasia ya
uchumi, na kazi kubwa ya Wizara ya Mambo ya Nje ni kuratibu shughuli za wizara
nyingine na Asasi za serikali na binafsi katika kukabiliana na changamoto za
maendeleo kwa kufuata diplomasia ya uchumi madhubuti na endelevu.
Mikakati inayotumika kutekeleza sera ya mambo ya nje
ni pamoja na kujenga mazingira wezeshi ya ndani ya kukuza uchumi; kuimarisha ubia wa kimataifa; kuweka
mbele malengo ya uchumi katika ushirikiano wa pande mbili (bilateral cooperation);
kuimarisha uhusiano wa kimataifa (multilateral cooperation); kukuza ujirani
mwema na kukuza ushirikiano wa kikanda.
Njanja zinazotumiwa kutekeleza malengo ya kukuza
ushirikiano ni mikutano ya pande mbili, tume za pamoja za ushirikiano, mikutano
ya kimataifa, balozi zetu nchi za nje na ziara za viongozi wetu wa kitaifa nchi
za nje na viongozi wa mataifa ya nje hapa nchini.
Wizara imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa
diplomasia ya uchumi, ambayo yamejidhihirisha katika sekta mbali mbali,
zikiwemo za afya, kilimo, nishati, mifugo na uvuvi, viwanda, miundombinu na
uchukuzi.
Baadhi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika
kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2011/12 hadi sasa ni pamoja na yafuatayo:-
Sekta ya Afya
Mwezi Oktoba, 2012, Bloomberg Philanthropies ya
Marekani ilitoa Dola za Marekani milioni nane(US$8,000,000) kwa ajili ya kuboresha vituo vya afya vijijini hapa nchini.
Ufadhili huo ulizinduliwa mjini New York, Marekani, na Mheshimiwa Rais Jakaya
Mrisho Kikwete. Msaada huo utatumika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya za
dharura kwa wanawake wajawazito na kuendesha mafunzo kwa maafisa tabibu
wasaidizi na wakunga.
Sekta ya kilimo
Katika mwaka wa fedha wa 2012, Mradi wa Rais Barack
Obama wa Marekani wa kuendeleza uzalishaji wa chakula katika nchi zinazoendea (Feed
the Future) ulisaidia zaidi ya wakulima 14,000
kutumia mbinu mpya za kilimo katika mashamba yao ya jumla ya hekta 22,430,
chini ya mpango wa Taifa was kukuza kilimo ukanda wa kusini (SAGCOT), wakati
wakulima wengine 13,000 walisaidiwa kuongeza uzalishaji kwa hekta kwa asilimia
46. Mradi huo pia ulifadhili mipango ya lishe iliyofaidia watoto 96,000 nchini.
Aidha, wizara ilifanikiwa kushawishi mamlaka za Chakula za Jamhuri ya Watu
wa China kuruhusu tumbaku inayozalishwa Tanzania kuingia kwenye soko la China.
China peke yake inanunua asilimia 46 ya tumbaku yote duniani na inalipa bei ya
juu kuliko nchi nyingine.
Sekta ya Nishati
Serikali ya China imetoa mkopo wa masharti nafuu
kujenga bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na mitambo ya
kusafishia gesi hiyo. Jumla ya gharama za mradi huu utakaoongeza uzalishaji wa
umeme nchini ni dola za Marekani bilioni 1.2.
Aidha, Tanzania ni kati ya nchi saba za Afrika
zitakazofaidika na mradi wa upanuzi wa uzalishaji wa umeme utakaogharimiwa na
Serikali ya Marekani (dola za Marekani bilioni 7) na Washirika wengine wa maendeleo (dola
bilioni 9).
Sekta ya Mifugo na Uvuvi
Wizara iliratibu ziara ya ujumbe wa wataalam kutoka
serikali ya Oman uliokuja nchini kutafuta fursa za biashara ya nyama na mazao
yake. Mazungumzo yanaendelea kati ya Oman na Kampuni ya Ranchi za Taifa ili
kuwezesha nchi yetu kufaidi9ka na biashara ya mifugo na kuboresha maisha ya
wafugaji.
Sekta ya Viwanda
Wizara imeratibu mipango ya kampuni ya Nitori ya Japan
kuwekeza katika sekta ya viwanda hapa nchini. Nitori itajenga kiwanda cha nguo
katika Ukanda Maalum wa Uwekezaji uliopo Bagamoyo, na tayari imepatiwa eneo la
kulima pamba huko Handeni, Tanga. Uwekezaji huo utatoa ajira kwa maelfu ya
Watanzania.
Wakati huohuo, Wizara kwa kushirikiana na Ubalozi wetu
New Delhi, india, inaratibu mpango wa Serikali ya India kufadhili miradi ya
kuendeleza teknolojia ya viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya Shirika la Viwanda
Vidogo Vidogo (SIDO). India itatoa dola za Marekani milioni 2 ikiwa ni sehemu ya msaada ulioahidiwa na
Waziri Mkuu Dkt. Manmohan Singh alipotembelea Tanzania Mei, 2011.
Sekta ya Miundombinu na Uchukuzi
Wizara imeshiriki kuivutia kampuni ya China
Merchant Holding International kuja kujenga bandari kubwa ya kisasa (4th generation
port) huko Bagamoyo,
ambako pia kampuni hiyo itajenga eneo la ukanda maalum wa uwekezaji (Export
Processing Zone- EPZ), mji
wa kisasa pamoja na miundombinu ya reli na barabara.
Mkataba wa Mwongozo (Framework Agreement) kuhusu
uwekezaji huo ulitiwa saini wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa
China, Mheshimiwa Xi Jinping hapa nchini, Machi, 2013.
Mradi huo mkubwa utatoa ajira za moja kwa moja kwa
maelfu ya Watanzania na kuliingizia taifa mapato kutokana na kodi na mrabaha.
Aidha utasaidia kupunguza foleni na msongamano katika jiji la Dar es Salaam.
Kadhalika, Serikali ya Japan imekubali ombi la
Tanzania kupitia Wizara yetu, kufadhili ujenzi wa barabara za kupita juu (flyovers) katika makutano ya Barabara za Nyerere na
Mandela, eneo la TAZARA jijini Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika mkutano uliofanyika
Arusha Mei, 2012, kati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Rais wa JICA. Mkataba wa makubaliano hayo umetiwa
saini na Serikali ya Japan inafanya maandalizi ya ujenzi.
Sekta ya Maji
Wizara imeweza kushawishi nchi mbali mbali rafiki
kusaidia ujenzi wa miradi ya maji hapa nchini. Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana
na Serikali za Ujerumani na Tanzania, wamegharamia mradi wa maji wa Swaya
mkoani Mbeya, ambao utafaidia wananchi 490,000. EU imechangia shilingi bilioni
36.9, Ujerumani shilingi bilioni 13.5 na Serikali ya Tanzania shilingi bilioni
29.1
Mradi huo ulifunguliwa na Mheshimiwa Rais Kikwete
wakatiwa ziara ya Mheshimiwa Jose Manuel Barroso, Rais wa Kamisheni ya Umoja wa
Ulaya hapa nchini Julai, 2012.
Aidha, Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo
wa Kuwait (Kuwait Fund),
imesaini makubaliano ya kugharamia mradi mkubwa wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe,
utakaofaidia mamia ya maelfu ya wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Mradi huo utatekelezwa mwaka huu wa fedha.
Mafanikio mengine ya Wizara
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNICC). Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya
Jamhuri ya Watu wa China imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Kituo hicho jijini
Dar es Salaam. Kituo hicho kina
uwezo wa kuchukua watu 1600 kwa wakati mmoja na ujenzi wake umegharimu USD
Milioni 15.5.
Ufunguzi wa Balozi mpya: Tangu kipindi cha mwaka 2007 hadi 2013 Tanzania imefungua Balozi mpya nne
ambazo zimefunguliwa katika nchi za Brazil, Malaysia, Uholanzi na Comoro na
kuifanya Tanzania kuwa na jumla ya Balozi 34, Balozi Ndogo 3 na Balozi za
Heshima 17.
Heshima ya Tanzania Kimataifa: Tanzania ilikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa
Afrika mwaka 2008 chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Tanzania sasa ni Mwenyekiti wa Asasi ya Ulinzi, Siasa na
Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC-TROIKA)
kuanzia Agosti 2012 hadi Agosti 2013.
·
Uteuzi wa
Watanzania wengi kushika nyadhifa mbalimbali kimataifa na kikanda:
Mfano ni Dkt. Asha-Rose Migiro, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa na hivi sasa ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja huo katika Masuala
ya UKIMWI Barani Afrika. Mwingine
ni Balozi Liberata Mulamula, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya
Maziwa Makuu (ICGLR), na wengine wengi.
Ziara
za viongozi wa Mataifa Makubwa Duniani
Katika kipindi cha utakelezaji wa Sera Mpya ya Mambo
ya Nje, Tanzania imekuwa mwenyeji wa ziara kadhaa za viongozi wa juu wa mataifa
makubwa duniani. Mwaka huu wa 2013 pekee, nchi yetu imetembelewa na Rais Xi
Jinping wa Jamhuri ya Watu wa China na Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Xi amekuwa kiongozi wa juu wa pili wa China
kutembelea Tanzania ndani ya miaka mitano iliyopita wakati Rais Obama ni Rais
wa tatu wa Marekani aliyeko madarakani kuzuru nchi yetu tangu mwaka 2000. Ziara
hizi ni kilele cha mafanikio ya sera yetu mpya ya mambo ya nje na
zinadhihirisha umaarufu ambao viongozi wetu wameijengea nchi yetu katika uwanja
wa kimataifa.
Aidha, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa
Majadiliano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue), uliohudhuriwa na
Wakuu wa Nchi na Serikali saba. Zaidi ya nchi 20 ziliwakilishwa kwenye mkutano
huo.
Hitimisho
Sera mpya ya Mambo ya Nje inayoweka kipaumbele kwenye
diplomasia ya uchumi, imeleta manufaa makubwa kwa nchi yetu na kuweka wazi
zaidi jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa la kuratibu
na kusukuma juhudi za kukuza uchumi wa taifa.
IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO
WA KIMATAIFA,
DAR ES N
`
SALAAM.
JULAI 28, 2013
No comments:
Post a Comment