Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Alexander Songorwa akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari juu ya umuhimu wa uhifadhi wa wanyama pori na faida za ushirikishwaji wa wananchi katika kuzuia ujangili. Kulia ni Ofisa Habari wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara hiyo, Yustina Mallya.
Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Kuzuia Ujangili kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, John Muya, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu faida za ushirikishwaji wa wananchi katika kuzuia ujangili, kwenye mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa. (Picha zote na Hassan Silayo-MAELEZO)
MCHANGO WA UHIFADHI KATIKA KUKUZA UCHUMI
WA NCHI NA UMUHIMU WA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA KUZUIA UJANGILI.
Wizara ya Maliasili na Utalii inawajulisha
wananchi kuwa ingawaje kumekuwa na taarifa za kuongezeka kwa ujangili
nchini na hasa mauaji ya kinyama ya tembo na usafirishaji haramu wa
wanyamaporihai na meno ya tembo, Wizara inajitahidi kupambana na uhalifu huu
kulingana na rasilimali watu na fedha zilizopo. Kwa mfano, mwaka 2012/13 pekee
(kufikia Machi 2013) watuhumiwa 1,215 walikamatwa kwa makosa mbalimbali wakiwa
na jumla ya bunduki 85 na risasi 215 za aina mbalimbali.
Kesi 670 zilifunguliwa katika mahakama
mbalimbali nchini. Kati ya hizo, kesi 272 zimemalizika kwa washitakiwa 247
kulipa faini ya jumla ya shilingi 175,002,420/= na washitakiwa 71 kupewa adhabu
ya vifungo vya jumla ya miaka 99. Aidha, kesi 398 zenye jumla ya washitakiwa
897 bado zinaendelea katika mahakama mbalimbali nchini.
Vita dhidi ya ujangili ni ngumu hasa
ukizingatia kuwa, baadhi ya Watanzania wanaamini kuwa jukumu hili ni la
serikali pekee na hasa maafisa na askari wanyamapori. Dhana hii ni potofu
kwani, uzuiaji ujangili kamwe hautafanikiwa kama wananchi na wadau wengine
walioko ndani na nje ya nchi yetu wataendelea kubakia watazamaji tu.
Wizara inaomba sote tuitafakari na
kuitekeleza dhana ya Jeshi la Polisi ya Ulinzi Shirikishi. Ni muhimu kila
mwananchi mzalendo wa nchi hii ashiriki kikamilifu kudumisha amani na ulinzi wa
nchi na rasilimali zake zote. Hivyo basi, wananchi wanaweza kutoa taarifa za
kina na uhakika zitakazopelekea kukamatwa majangili na/au wafadhili wao.
Yeyote mwenye taarifa azitoe ama kwa Afisa
Wanyamapori aliye karibu yake, Makao Makuu ya Idara ya Wanyamapori, TANAPA,
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro au Kituo cha Polisi kilichokaribu. Pia
unaweza kupiga simu kwenye namba zilizoambatanishwa kwenye taarifa hii.
Aidha, ikumbukwe kuwa hapa nchini, zaidi ya
asilimia 90 utalii unategemea wanyamapori. Watalii wengi huja kuwaona, kuwapiga
picha na kuondoka. Wachache huja kuwawinda kisheria na kuchukua nyara.
Wanyamapori ndio wamebeba utalii katika Tanzania na kwa maana hiyo ndio, kwa
kiasi kikubwa, wamebeba uchumi wa nchi hii – ndio wanatununulia dawa, vitabu
mashuleni na kutujengea barabara.
Wizara inatoa wito kwa Watanzania kuwa
tuache kumtazama fisi kama mnyama mwenye sura mbaya na anayenuka; na tuache
kumtazama tembo kama kero kwa wakulima na kwa hiyo kufurahia kuuawa kwao.
Badala yake tuwatazame wanyamapori kama benki kubwa na kama mkombozi wa nchi
yetu kiuchumi.
Wanyamapori kama ilivyo viumbe hai,
huzaliana. Hivyo, kama tutashirikiana kuwalinda na kuwatumia kiendelevu si
miaka mingi tangu sasa watakuwa namba moja katika kuchangia pato la Taifa letu.
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
17 Julai 2013
Namba za simu: 0754877019; 0787491600;
0713350405; 0784483599; 0754756585 Barua pepe: dw@mnrt.go.tz
au ps@mnrt.go.tz
No comments:
Post a Comment