TANGAZO


Thursday, July 25, 2013

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA; MAANDALIZI YA SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI

Ofisa Habari toka Wizara ya Katiba na Sheria Farida Khalifan (kushoto), akieleza kwa vyombo vya habari juu ya mpango wa Serikali kupitia Wizara hiyo kuandaa Sheria ya Msaada wa Kisheria kwa wananchi katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo, jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa na kulia ni Afisa Sheria Mwandamizi, Mercy Mrutu.
Mwenyekiti Kikosikazi cha kuandaa sheria, Dk. Kennedy Gaston akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mpango wa Serikali kupitia wizara hiyo, kuandaa Sheria ya Msaada wa Kisheria kwa wananchi katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo, jijini Dar es Salaam. 
Ofisa Sheria Mwandamizi, Mercy Mrutu akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari juu ya maandalizi ya uandaaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari leo, 
Jijini Dar es Salaam.

Ndugu Wanahabari,
Kwa niaba ya Wizara ya Katiba na Sheria, nianze kwa kuwashukuru kwa kuitikia mwaliko wetu. Pia niwashukuru kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuwataarifu wananchi kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa ujumla wake na kwa namna ya pekee zile zinazofanywa na Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zilizo chini yake.

Ndugu Wanahabari,
Leo tumekutana hapa ili kuwafahamisha kuhusu mpango wa Serikali wa kutunga Sheria ya Msaada wa Kisheria ambayo inalenga kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kulipia gharama zinazotozwa na Mawakili wa kujitegemea ambazo ni kubwa.

Ili kutekeleza mpango huu, mwaka 2010, Wizara ya Katiba na Sheria iliunda Kikosi Kazi (Task Force) kilichojumuisha wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Umma na Asasi za Kiraia zinazojishughulisha na utoaji wa msaada wa kisheria ili kufanya utafiti na kutoa mapendekezo kuhusu mfumo bora wa kisheria wa utoaji msaada huu.

Baada ya Kikosi Kazi hiki kuwasilisha mapendekezo yake, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ilianza taratibu za kutunga Sheria itakayojulikana kama ‘Sheria ya Msaada wa Kisheria’.

Ndugu Wanahabari,
Maandalizi ya Sheria hii sasa hivi yapo katika hatua za mwisho ndani ya Serikali kabla ya Muswada wa Sheria hii kuwasilishwa Bungeni. Lengo la Serikali ni kuwa ifikapo mwezi Januari mwaka ujao wa 2014 Sheria hii iwe imekamilika.

Watoa Msaada Kisheria ni Kina nani?
Ndugu Wanahabari,
Sheria itakayotungwa itamtambua Mtoa Msaada wa Kisheria kama ni mtu ambaye siyo Mwanasheria kitaaluma, lakini amepata mafunzo ya muda mfupi ya kisheria na amesajiliwa na chombo huru na kuwa anafanya kazi ya kutoa msaada wa kisheria chini ya Wakili au Taasisi iliyosajiliwa.

Yanayotarajiwa kuwemo katika Sheria
Ndugu Wanahabari,
Sheria itakayotungwa itaunda Chombo Huru kitakachokuwa na majukumu mbalimbali yakiwemo:
i.              Kusajili Taasisi zinazotoa Msaada wa Kisheria nchini kote;
ii.             Kusajili Watoa Msaada wa Kisheria;
iii.            Kuweka viwango vya ubora katika utoaji msaada wa kisheria na kuvisimamia viwango hivyo;
iv.            Kusimamia nidhamu na maadili ya watoa huduma za msaada wa kisheria;
v.             Kutambua Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals);
vi.            Kutafuta fedha ili kutekeleza majukumu yake;


Ndugu Wanahabari,
Maana ya majukumu haya ni kuwa baada ya Sheria kuanza kufanya kazi, watoa msaada wote (individuals) wa kisheria itabidi wasajiliwe katika Taasisi au Asasi ili watambulike na chombo hicho huru. Taasisi au Asasi hizo zitasajiliwa na chombo hicho. Kwa hiyo, hakuna mtoa msaada wa kisheria atakayeruhusiwa kufanya kazi bila kusajiliwa na Taasisi au Asasi.

Aidha, watoa msaada wa kisheria watatakiwa na Sheria kutoa huduma hiyo kupitia vituo vya Msaada wa Kisheria vilivyosajiliwa na kutoa huduma hizo kwa usimamizi wa Mawakili waliosajiliwa ili kusimamia ubora wa huduma zao.

Athari za Kutokuwepo kwa Sheria hii
Ndugu Wanahabari,
Kutokuwepo kwa sheria kama hii wakati mwingine kumesababisha kuwepo kwa watu wasio na taaluma ya sheria maarufu kama Bush Lawyers ambao wamekuwa wakiwarubuni wananchi kuwa wanaweza kuwasaidia kisheria. Watu hawa, mara nyingi wamekuwa wakizalisha migogoro ili wapate fursa ya kuitatua kwa malipo.  Kuwepo kwa sheria hii kwa kiasi kikubwa kutatatua tatizo hilo.

Sheria hii haitabadilisha utaratibu wa mawakili wa kujitegemea wa kutoa huduma zao kwa malipo na pia kama msaada yaani bure.

Wigo wa Msaada wa Kisheria Kupanuka
Mara baada ya sheria hiyo kuanza kutumika, wigo wa wananchi kupata msaada wa kisheria utapanuka kwa sababu taratibu zitakazowekwa na sheria hiyo zitahusisha mashauri ya jinai na mashauri ya madai. Mtakumbuka kuwa, kwa sasa msaada wa kisheria unatolewa kwa baadhi ya mashauri ya jinai tu chini ya Sheria ya (Legal Aid in Criminal Proceedings Act).

Makundi Maalum yatakayofaidika
Ndugu Wanahabari,
Baada ya Sheria hii kuanza kutumika, tunategemea makundi maalum kama watoto, wajane na wote wasio na uwezo watapata haki ya kupata msaada wa kisheria bila malipo. 

Aidha, sheria hii itakataza watoa huduma za msaada wa kisheria kutoza malipo ya aina yoyote wakati wa utoaji wa msaada wa kisheria.

Kutungwa kwa sheria hii kunafuatia kilio cha muda mrefu cha wananchi wasio na uwezo ambao wamekuwa wakipata shida kupata haki kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.

Aidha, sheria hii itaweka utaratibu mzuri wa kusimamia utoaji wa msaada wa kisheria na kuiwezesha Wizara ya Katiba na Sheria kusimamia masuala ya Kisera na Kibajeti na Elimu kwa Umma juu ya msaada wa kisheria badala ya kuhusika moja kwa moja na masuala yanayohusika na utoaji wa msaada wa kisheria.

Asanteni kwa Kunisikiliza


No comments:

Post a Comment