TANGAZO


Tuesday, July 23, 2013

WANANCHI NA WADAU WAALIKWA KUTOA MAONI KWA AJILI YA KUANDAA SERA MPYA YA TAIFA YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO KWA MAENDELEO, TAREHE 23 JULAI, 2013

Ofisa Habari Mwandamizi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prisca Ulomi (kushoto), akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu ushiriki wa wananchi na wadau mbalimbali katika utoaji wa maoni kwa ajili ya kuandaa Sera Mpya ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo, kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.
(Picha na Eliphace Marwa-MAELEZO)
  • Mkurugenzi, Idara ya Habari MAELEZO, Bw. Asah Mwambene;
  • Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, Bi. Zamaradi Kawawa;
  • Ndugu Wanahabari;
  • Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Habari za asubuhi.

  1. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote mliofika katika mkutano huu muhimu wenye lengo la kuwaalika wananchi na wadau wa Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)  kutoa maoni yao kwa ajili ya kuandaa Sera mpya ta TEHAMA kwa Maendeleo.  Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia tayari imeanza kuhuisha Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 pamoja na kuandaa mpango wake wa utekelezaji. Mahuisho haya ya Sera ya TEHAMA yanalenga kuiwezesha nchi na Taifa letu kwenda sambamba na ukuaji wa kasi wa Teknolojia  ya Habari na Mawasiliano duniani na matumizi yake kwa wananchi. Pia ukuaji na mabadiliko ya kasi yanayotokea kwenye sekta hii yanahitaji uwekezaji mkubwa na wenye kushirikisha sekta na wadau mbalimbali na hivyo Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia  imeona ni wakati muafaka Sera iliyopo ihuishwe ili Sekta iweze kuendeshwa kwa ufanisi zaidi na hatimaye kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi.





  1. Zoezi hili la uhuishaji wa Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 ni sehemu ya utekelezaji wa  program ya kujenga Jamii Habari na Kuendeleza Sekta ya TEHAMA (TANZICT) inayofadhiliwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Finland katika jitihada za kuendeleza Sayansi, Teknolojia, ubunifu na TEHAMA hapa nchini ili Sekta iweze kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya hapa nchini. Kwa kuwa masuala ya utumiaji wa huduma za TEHAMA na manufaa yake kwa wananchi ni suala mtambuka, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia inashirikisha wadau kutoka katika sekta mbalimbali ili waweze kufahamu na kujenga uelewa wa pamoja mapema na hatimaye kuwa na Sera mpya ya TEHAMA kwa Maendeleo inayotekelezeka na yenye kujibu changamoto zinazowakabili wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa letu.


Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

  1. Ni dhahiri kuwa sekta ya Mawasiliano inakuwa kwa kasi kubwa sana duniani kote na hapa nchini kwetu pia. Lengo la kuhuisha Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 ni kutengeneza Sera itakayochochea maendeleo endelevu ya Kijamii na Kiuchumi hapa nchini; ikiwa ni kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta, kujumuisha masuala ambayo hayakuwepo katika Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 na kujumuisha maendeleo makubwa ya kiteknolojia yaliyotokea katika Sekta ya TEHAMA kwa kipindi cha miaka kumi (10) tangu Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 iliporidhiwa na kuanza kutekelezwa na Serikali.



  1. Dhumuni la zoezi hili ni kupata Sera ya Taifa ya TEHAMA endelevu na kamilifu itakayokidhi mahitaji ya huduma za TEHAMA na inayojibu hoja zinazotokana na mabadiliko ya kasi ya kiteknolojia yanayotokea Duniani kote; Sera itakayotekelezeka katika nyanja za kiuchumi na kijamii kwa kuwa TEHAMA ni suala mtambuka; na kuhakikisha inatoa mchango wake ipasavyo kama kichochezi kikuu cha maendeleo katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa kila siku katika sekta mbalimbali na kurahisisha maisha ya wananchi. Zoezi hili la uhuishaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 linawahusisha wadau na wananchi wote kwa ujumla ili kufanikisha upatikanaji wa Sera shirikishi; jumuishi na itakayomilikiwa na wadau wote kwa ajili ya kuleta ufanisi katika utekelezaji wake.


Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

  1. Sera hii mpya inatarajiwa kujikita katika Nguzo kuu Nane tofauti na Sera ya mwaka 2003 ambayo ilikuwa na jumla ya nguzo kumi. Nguzo ya Kwanza inahusu maendeleo ya rasilimali watu na uongozi katika TEHAMA (ICT Leadership and Human Capital Development) na inalenga Kuwa na Jamii Habari inayoendeshwa na viongozi mahiri wenye ujuzi na uwezo wa hali ya juu katika TEHAMA ili kwenda sambamba na viwango vya Kimataifa katika kufikia malengo ya maendeleo ya Tanzania. Nguzo ya pili inazungumzia upatikanaji wa huduma za mawasiliano na miundombinu ya TEHAMA (ICT Access and Infrastructure) yenye lengo la Kuwa na Jamii Habari inayoendeshwa kupitia upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wote na miundombinu ya TEHAMA yenye uwezo mkubwa. Ya tatu ni maendeleo ya sekta ya TEHAMA (ICT Sector development). Nguzo hii inasisitiza Tanzania kuwa na Sekta mahiri ya TEHAMA katika uzalishaji na uendelezaji wa huduma za kisasa za TEHAMA kuanzia ngazi ya viwanda vidogo vidogo hadi vikubwa.

  1. Nguzo ya nne ni huduma mtandao na uendelezaji wa maudhui ya kitaifa/nyumbani (E-services and local content development) Nguzo hii imejikita katika utoaji huduma za kielektroniki za nyongeza zinazozingatia mahitaji na mazingira ya mtumiaji na zenye ubora wa hali ya juu ambazo zitawezesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Ya tano ni Ulinzi, Usalama na Viwango katika TEHAMA (ICT Safety, Security and Standardization). Nguzo hii inaitaka nchi yetu ya Tanzania kuwa nchi salama kielektroniki; na yenye mifumo na huduma za TEHAMA zinazotegemewa na kuaminiwa ambazo zitawezesha uchumi endelevu. Nguzo ya sita inahusu masuala ya kisheria, udhibiti na mfumo wa uendeshaji TEHAMA  nchini (Legal, regulatory and Institutional framework). Nguzo hii inatoa mwelekeo wa Tanzania kuwa nchi yenye mfumo madhubuti wa kisheria na kiudhibiti katika TEHAMA unaohusisha matumizi bora ya vyombo vya kisheria yanayozingatia utendaji bora Kikanda na Kimataifa katika kuendeleza na kulinda huduma za kielektroniki. Ya saba ni Ushirikiano wa Kitaifa, Kikanda na Kimataifa katika nyanja ya TEHAMA (Local, Regional and International Cooperation). Nguzo hii inaitaka Tanzania kuwa Taifa linaloongoza katika kutambua na kutumia ushirikiano wa kimkakati katika TEHAMA Kitaifa, Kikanda na kimataifa katika kujenga Jamii Habari. Na nguzo ya nane inahusu Sekta za uzalishaji (Productive sectors). Nguzo hii ina lengo la kuifanya Tanzania kuwa na Sekta za uzalishaji madhubuti, zenye ufanisi na ambazo zinashirikiana  ili kuwa na matokeo ya matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi katika sekta hizo kama vile ya madini, nishati, mafuta na gesi, utalii, kilimo, viwanda na biashara, ujasiriamali, na huduma za kifedha.




Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,

  1. Kwa kutambua mchango wa wadau na wanachi kwa ujumla katika kufanikisha ukuaji wa Sekta ya TEHAMA; matumizi yake kwa wanachi katika kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku; na mchango wa Sekta ya TEHAMA katika kuleta maendeleo ya Taifa letu, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia inatoa fursa kwa wadau na wananchi wote kwa ujumla kushirikiana na Wizara kutoa maoni yatakayofanikisha uaandaji wa Sera mpya ya TEHAMA kwa Maendeleo. Wadau na wananchi wote mnaalikwa kutoa maoni yenu kwa kutumia barua pepe ya Wizara ambayo ni mst@mst.go.tz, kutembelea tovuti ya Wizara www.mst.go.tz na kuwasilisha kwa maandishi Wizarani kwa Katibu Mkuu kwa barua kupitia sanduku la Posta 2645, Dar es Salaam. Wizara itapokea maoni hayo kuanzia tarehe 24 Julai, 2013 hadi tarehe 15 Agosti, 2013. Maoni yenu ndugu wananchi na wadau wa Sekta ya TEHAMA yatapokelewa; kuchambuliwa; na kujumuishwa kwenye Sera mpya ya TEHAMA kwa maendeleo (ICT4D).

Ndugu Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana,
  1. Kabla sijamaliza, kwa niaba ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau na wananchi wote wanaoshiriki kwa njia moja au nyingine katika kuandaa Sera hii mpya ya TEHAMA kwa Maendeleo. Natoa wito kwa watanzania na wadau wote kutoa maoni kuhusu Sera hii kuanzia tarehe 24 Julai, 2013 hadi tarehe 15 Agosti, 2013 ili kufanikisha uaandaji wa Sera kwa wakati.
Asanteni kwa kunisikiliza.

Imetolewa na;
Prisca J. Ulomi
Afisa Habari Mwandamizi,

Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

No comments:

Post a Comment