TANGAZO


Tuesday, July 16, 2013

Bashir arejea nyumbani kutoka Nigeria


Omar al-Bashir akiwa kwenye mkutano wa AU
Rais wa Sudan Omar al-Bashir, ameondoka nchini Nigeria baada ya makundi ya kutetea haki za kibinadam kwenda mahakamani, kushinikiza serikali kumkamata kuhusiana na tuhuma za uhalifu wa kivita.
Afisa mmoja wa kibalozi, katika ubalozi wa Sudan nchini Nigeria, amesema rais Bashir, alirejea nyumbani Jumatatu jioni kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Muungano wa Afrika ambao alikuwa akihudhuria.
Afisa huyo amesema, rais huyo alikuwa na majukumu mengine ambayo yalikuwa yakimsubiri nyumbani na amekanusha madai kuwa aliondoka kwa sababu ya kuongezeka kwa shinikizo za kukamatwa kwake.
Mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC, inamtuhumu Rais Bashir kwa kuhusika na mauaji ya halaiki katika eneo la Darfur nchini Sudan.
Muungano wa Afrika umetoa wito kwa wanachama wake kutotekeleza agizo la mahakama ya ICC ya kumkamata rais huyo wa Sudan.
Viongozi hao wa AU wanasema mahakama hiyo ya ICC imekuwa ikiwalenga viongozi wa nchi za Kiafrika pekee.
Bwana Bashir alikuwa Nigeria kwa mkutano ulioandaliwa na muungano wa Afrika kuhusu afya unaokamailika baadaye leo.
Ubalozi wa Sudan umesema kuwa aliondoka kwa sababu ya majukumu mengine.
Mahakama ya kimataifa ya ICC ilitoa kibali cha kumkamata Bashir mwaka 2009, baada ya kumtuhumu kwa kufanya mauaji ya halaiki wakati wa vita vilivyodumu mwongo mmoja katika jimbo la Darfur.
Sudan haitambui mahakama ya ICC na inaituhumu kwa kuwa chombo cha nchi za kimataifa kutumiwa kukandamiza nchi za Afrika huku Muungano wa Ulaya ukitoa wito kwa nchi za Afrika kutomkamata Bashir.
Aidha Bashir alitarajiwa kutoa hotuba kwenye mkutano huo mjini Abuja, Jumatatu kulingana na vyombo vya habari nchini humo.
Lakini alipoitwa kutoa hotuba yake hakuwepo kwenye ukumbi.
Bashir alipokelewa na gwaride la jeshi Nigeria, alipowasili mjini Abuja Jumamosi. Mkutano huo unatafuta mbinu za kupambana zaidi na magonjwa ya Kifua kikuu, Ukimwi na Malaria.
Viongozi kutoka nchi nane za Afrika wanahudhuria mkutano huo.
Msemaji wa rais wa Nigeria,Reuben Abati, aliambia shirika la habari la AP kuwa Bashir alikuwa mjini Abuja kwa mwaliko wa muungano wa AU wala sio Nigeria.

No comments:

Post a Comment