TANGAZO


Saturday, June 29, 2013

Muungano hautakufa kwa Serikali tatu - Jaji Bomani

Jaji Mkuu mstaafu Mark Bomani

Na Juma Mohammed, Zanzibar
MWANASHERIA Mkuu wa kwanza mzalendo, Tanzania, Jaji mstaafu Mark Bomani amesema Muungano hautakufa kwa kuwa na mfumo wa muundo wa  Serikali tatu.

“Muungano hautakufa kwa kuwa na Serikali tatu (Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano), lakini unaweza kufa kwa sababu ya watu wenye tamaa na maslahi binafsi wasiojali wananchi,” alisema, Jaji Bomani.

Jaji mstaafu Bomani, alikuwa akihutubia kwenye kongamano la siku moja lililofanyika  Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar leo, ambapo alisema kwamba mfumo wa muundo wa Muungano wa Serikali hauna gharama zaidi ya kupunguza gharama ambazo zipo.

“Sikubaliano na hoja ya gharama kama inavyoelezwa na baadhi ya watu, Serikali ya Muungano itakuwa na mambo machache kwa hivyo, hakuna suala la gharama, Bunge lake litakuwa na Wabunge wachache,” alisema Jaji Bomani.

Jaji Bomani, ameendelea kusisitiza kwamba kwa mtazamo wake, mfumo wa kuwa na Serikali tatu ndio mujarab. 

“Mfumo wa Serikali moja hauna uwezekano…hili lilibainisha miaka 50 iliyopita, mfumo wa Serikali, ndiyo hivyo tumejionea matatizo na kero zake na ubishi usiokwisha,” alisema Jaji Bomani.

Alisema serikali tatu zitatoa nafasi kwa kila nchi mwanachama kuendesha mambo yake jinsi wananchi wake wanavyotaka.

Jaji Bomani alisema ni vigumu kuunda mfumo wa muundo wa Muungano ambao utamfanya mdogo kuwa na hofu. 

“Kwa kuondoa shaka hiyo, tuwe na Serikali tatu, ya Zanzibar, ya Tanganyika zote zikiwa na madaraka kamili na kwa kuwa sisi ni wamoja lazima tuwe na kitu kinachotuunganisha, nacho ni Serikali ya Muungano.”

Aidha, alishauri mjadala wa kupata Katiba mpya uwe huru, wananchi wafungue mioyo yao, wasifungwe na mawazo au itikadi fulani na badala yake kila mmoja atoe alichonacho moyoni. 

Alizungumzia pia hoja ya Serikali ya mkataba, alisema 
“Serikali ya mkataba inawezekana ikiwa  watu wanataka  hilo si la ajabu, kitu umuhimu ni watu wakae kitako kuamua nini wanataka, wasiburuzwe au kufungwa mikono”

Jaji Bomani, alirudia suala lake la kupendekeza mjadala huru ili kila upande uweze kutoa dukuduku lake na muafaka huru upatikane. 

Katika kufikia hilo, alipendekeza ama Tume ya Uchaguzi Zanziba( Zec) au hata Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), isimamie mchakato wa kupata maoni huru huku wakiuliza maswali mawili tu.

Ameyataja maswali hayo kuwa ni “je, unautaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar? Na la pili kama jibu lako ni ndiyo, unapendelea Muungano wa mfumo gani, Serikali moja, Serikali mbili, Serikali tatu”.

Kongamano hilo, liliandaliwa na Kamati ya Maridhiano Zanzibar, lilikuwa chini ya Uenyekiti wa Mzee Hassan Nassor Moyo, mshereheshaji alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mansoor Yussuh Himid.

Wajumbe wengine wa Kamati ya maridhiano ni pamoja na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa, Mohammed Riyami na Salim Bimani.


No comments:

Post a Comment