TANGAZO


Saturday, June 29, 2013

CCM yavuna wananchama wapya 320, 62 kutoka upinzani

.CUF yafananishwa na magugu maji

Katibu wa Tawi la CUF, Wame Kata ya Kilago, wilayani Kahama, Hamisi Mabala akikabidhi bendera na kadi za Chama cha Wananchi (CUF) kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja (wa pili kulia), baada ya kujiunga nacho jana. (Picha na Mpiga picha wetu)

Na Mwandishi wetu, Shinyanga
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na Katibu wa Tawi la Wame, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, amekihama chama chake na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akikifafananisha na magugu maji.

Katibu huyo, Hamisi Mabala alikuwa ni miongoni mwa wanachama 62, kutoka vyama vya CHADEMA, CUF na TLP walioamua kuvihama vyama vyao na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika sherehe za muendelezo wa
maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika katika kata ya Kilago, wilayani Kahama.

Mbali ya wanachama hao 62 pia CCM ilifanikiwa kupata wanachama wapya wengine 258 ambao walikabidhiwa kadi zao na mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, ambazo pia zilihudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya siasa ya Wilaya na Diwani wa kata ya Chato, Ismail Luge.

Akikabidhi kadi na bendera ya CUF kwa mgeni rasmi, Mabala alisema ameamua kuhama katika chama hicho baada ya kubaini kuwa hakina mwelekeo wowote wa kutawala nchi kutokana na kuwa na nguvu upande mmoja wa nchi na kutokuwa na mawasiliano yoyote kati ya viongozi wa ngazi ya juu na wale wa chini.

“Kwa kweli CUF ni chama kinachoelea hewani tu, maana huku katika mashina hakina nguvu kabisa, viongozi wake wa ngazi ya juu hawana mawasiliano kabisa na sisi viongozi wa ngazi ya chini, ni wazi hata kifanye miujiza ya ajabu hakiwezi kufanikiwa kukamata dola, ndiyo maana nimeona nijiunge na CCM,” alieleza Mabala.

Akizungumza katika sherehe hizo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mgeja aliwakaribisha wanachama wote wapya waliojiunga na chama hicho na kusema huko ndiko kwenye ufumbuzi wa matatizo yote ya watanzania na kwamba vyama vya upinzani havina uwezo wowote wa kuwatatulia kero zao.

“CCM daima tunahubiri maendeleo, hatuna matusi, tunapokaa kazi yetu ni kuzungumzia maendeleo ya watanzania, hata hivyo kila mmoja wenu anapaswa afahamu kuwa siri kuu ya utatuzi wa matatizo yetu ni kufanya kazi kwa bidii, kukimbilia vyama vya upinzani ni kupoteza wakati,” alisema Mgeja.

Aidha aliwatahadharisha wana CCM kujiepusha na vita ya kuwania madaraka na kwamba tabia ya watu kuwania madaraka kwa nguvu inataka kujitokeza katika siku za hivi karibuni kiasi cha kuundiana kamati za fitina na kwamba ni muhimu ikaepukwa kwani itapunguza kwa kiasi kikubwa mshikamano waliokuwa nao huko nyuma.

Kwa upande wake mwenyekiti mstaafu wa CCM wilayani Kahama, Edward Msoma aliwaomba wanachama wa CCM kuacha tabia ya kupigana vita wenyewe kwa wenyewe na kwamba wanachohitaji watanzania ni kuondolewa matatizo
yanayowakabili katika maeneo yao na siyo kusikia malumbano.

Wanachama hao wapya 320 wanafikisha idadi ya wanachama zaidi ya 600 waliojiunga na CCM ndani ya kipindi cha wiki mbili wilayani Kahama ambapo mapema wiki iliyopita wanachama wengine 280 katika kata ya Nyanhembe hali inayoashiria chama hicho kuendelea kukubalika na
wananchi.

No comments:

Post a Comment