TANGAZO


Thursday, June 20, 2013

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu yazungumzia matumizi ya M-pesa

Naibu Mkurugenzi wa Tehama wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini, Cuthbeth Simalenga akimulezea jambo Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Tanzania Salum Mwalim wakati Vodacom ilipotembelea Makamo Makuu ya bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo kwa lengo la kukuza uhusiano baina ya taasisi hizo mbili. Bodi hiyo hutumia huduma ya M-pesa kama njia kuu ya kukusanyia ada ya uombaji mikopo tangu mwaka 2010.
Mkuu wa Idara ya Uendelezaji Biashara ya M-pesa Jackson Kiswaga akionesha jinsi M-pesa inavyoweza kuboreshwa kukidhi mahitaji zaidi ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu ambayo huitumia huduma hiyo, kama njia kuu ya kukusanyia ada ya maombi ya mkopo, tangu mwaka 2010. Wanaomuangalia ni Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom Salum Mwalim (kulia) na Naibu Mkurugenzi wa Tehama wa bodi hiyo, Cuthbeth Simalenga. Vodacom imetembelea Makao Makuu ya bodi hiyo leo kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa taasisi hizo mbili.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano, Habari na Elimu kwa Umma wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Cosmas Mwaisbwa akifafanua jambo wakati wa kikao baina ya bodi na Kampuni ya Vodacom Tanzania kuangalia namna ya kuimarisha na kuboresha zaidi uhusiano wa biashara baina ya taasisi hizo mbili. Wengine pichani kutoka kulia ni Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalim na Naibu Mkurugenzi wa Tehama wa bodi hiyo, Cuthbeth Simalenga.
Mkuu wa Idara ya Uendelezaji Biashara ya M-pesa, Jackson Kiswaga akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati Vodacom ilipotembelea Makao Makuu ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu jijini Dar es Salaam leo kwa lengo la kukuza uhusiano wa biashara baina ya taasisi hizo mbili. Kulia ni Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo wa Bodi, Juma Chagonja na Naibu wa Tehama wa bodi hiyo Cuthbeth Simalenga. Bodi ya mikopo kwa miaka mitatu sasa imekuwa ikiitumia huduma ya M-pesa kama njia kuu ya kukusanyia ada ya mamombi ya mkopo kutoka kwa waombaji wake. 
Mkuu wa Idara ya Uendelezaji Biashara ya M-pesa, Jackson Kiswaga akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati Vodacom ilipotembelea Makao Makuu ya bodi hiyo, jijini Dar es Salaam leo kwa lengo la kukuza uhusiano baina ya taasisi hizo mbili. Bodi hiyo hutumia huduma ya M-pesa kama njia kuu ya kukusanyia ada ya uombaji mikopo tangu mwaka 2010. Kutoka kulia ni Meneja Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom Salum Mwalim na Naibu Mkurugenzi wa Tehama wa bodi hiyo, Cuthbeth Simalenga. (Picha zote na Mpiagapicha wetu)



Na Mwandishi wetu.
Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu nchini - HESLB imesema huduma ya M-pesa inayowawezesha waombaji wa mikopo ya elimu juu kwenye bodi hiyo kulipia ada ya uombaji kwa kiasi kikubwa imesaidia kurahisisha uendeshaji ikwemo usimamizi na ufuatiliaji wa malipo hayo.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini, Cuthbeth Simalenga wakati wa kikao cha urafiki mwema kati ya uongozi wa Bodi na Kampuni ya Vodacom kilichofanyika Makao Makuu ya bodi hiyo, yaliyopo Msasani Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa taasisi hizo.

Simalenga amesema bodi hiyo ilianza kutumia huduma ya M-pesa kwa malipo ya ada ya maombi miaka mitatu iliyopita na kwamba tangu wakati huo huduma hiyo imekuwa ikiimarika na kutoa tija zaidi kwa upande wa uendeshaji wa shughuli za uombaji wa mikopo.

“Kwa miaka mitatu sasa tumekuwa tukitumia huduma ya M-pesa kukusanyia ada za malipo ya maombi ya mikopo, kwa sasa waombaji wote wanatumia huduma hii na tumekuwa tukiboresha mifumo yetu ya ndani mara kwa mara kukabiliana na changamoto za hapa na pale zinazojitokeza.”Alisema Simalenga.

Zaidi ya waombaji 50,000 wakiwemo waombaji wapya na wale wanaaondelea na elimu ya juu hutuma maombi ya mikopo kwenye  bodi hiyo kwa mwaka, na wote kwa sasa wanatumia huduma ya M-pesa kulipia ada ya malipo ya maombi ambayo ni Sh 30,000.

Simalenga amesema changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa katika mfumo huo wa malipo kuwa ni uaminifu wa waombaji hasa wanafunzi ambao baadhi yao hulalamika kushindwa kulipia au na kudai kutaka kurejeshewa fedha zao wakati huohuo wakiwa tayari wameshakamilisha mchakato wa uombaji na fedha hizo kupaswa kutumika kama ada ya uombaji.

“Wamekuwepo baadhi ya waombaji ambao wamekuwa wakisababisha usumbufu wa hapa na pale kwa kutuma maombi na kufanya malipo baadae wanarudi na kupiga simu Vodacom kudai kurejeshewa fedha zao kwa madai kuwa wamebadili mawazo ya kuomba mkopo wakati sio kweli.” Aliongeza Bw. Simalenga.

“Tunaomba waombaji wote na umma kwa ujumla kutambua kuwa mamlaka ya kurejeshewa fedha Sh 30,000 ya ada ya uombaji yapo nje ya Vodacom, hilo ni la Bodi na kwamba sasa tumeweka utaratibu wa kurudisha fedha hizo mwishoni mwa zoezi la uombaji tukizinagtia taratibu za kiuhasibu za bodi baada ya kujiridhsiha kuwa utambulisho wa muamala (Transaction ID) wa mwombaji haijatumika kuendelea na zoezi la uombaji mkopo.”Alifafanua.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuzungumzia uhusiano wa bodi na kampuni ya Vodacom ambao amesema una kila nafasi ya kuwa imara zaidi huku akiishauri Vodacom kuongeza ubunifu zaidi kwenye mfumo wa malipo ya M-pesa ili mfumo huo uweze kuwa na tija zaidi kwa wadau wake hasa wabia wakubwa.

“Vodacom imekuwa karibu na sisi na bado kuna fusra zaidi ya ubunifu kwenye huduma hii itakayotoa tija zaidi kwetu.”Alisema Bw Simalenga na kuongeza “Tunafurahia uhusiano wetu wa kibishara kwa kipindi chote hiki kwani tumepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Vodacom pekee hivyotumejikuta tukiwa na M-Pesa pekee.”

Kwa upande Mkuu wa Idara ya Ukuzaji Biashara ya M-pesa wa Vodacom Bw Jackson Kiswaga amesema kiasi cha Sh. Bilioni Moja na Milioni Mia Nne kinapitia katika mfumo wa M-pesa kama ada ya uombaji wa mikopo kila mwaka.

“Tumekuja kubadilishana uzoefu na wenzetu juu ya uhusiano wetu unaotuunganisha kupitia huduma ya M-pesa, bodi hii imekuwa sehemu muhimu kwetu kibiashara na tunatarajia kuimarisha zaidi huduma hii siku zijazo.”Kiswaga aliwaambia waandishi wa habari wakati wa ziara hiyo.

Kiswaga amewakumbusha waombaji wa mikopo wa bodi hiyo ya elimu ya Juu kuendelea kuitumia huduma ya M-pesa katika kulipia ada ya uombaji kwa kuwa ndio njia rahisi na ya kuaminika zaidi kwao inayowapunguzia gharama za usafiri,muda na usumbufu.  

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo wa Bodi hiyo Bw. Juma Chagonja amesema bado zipo fursa nyingi bodi inazoweza kuzitumia kwenye huduma ya M-pesa na kuwataka wananchi kuvuta subira kuona mambo mazuri zaidi siku chache zijazo.

No comments:

Post a Comment