Rais Omar al-Bashir wa Sudan, katika ziara yake ya kwanza mjini Juba tangu nchi ya Sudan ya Kusini kuwa huru mwaka 2011, ametangaza mipaka kati ya nchi hizo mbili kufunguliwa.
Akizungumza akiwa na rais mwenzake, Salva Kiir, Bw Bashir alitaka pia mataifa hayo mawili kudumisha amani, na kuimarisha uhusiano wa kawaida tena.
Hali ya uhasama iliongezeka kati ya mataifa hayo mawili mwaka jana, huku kukiwa na wasiwasi wa kuzuka vita.
Uhasama huo umepungua, lakini tofauti kuhusiana na mafuta na ardhi bado upo kati ya nchi hizo mbili.
"Nimewaamuru maafisa wa serikali ya Sudan chama cha maslahi ya raia kushirikiana na ndugu zao katika Jamhuri ya Sudan ya Kusini", Bw Bashir alieleza katika hotuba yake katika mji mkuu wa Sudan ya Kusini, Juba.
"Kamwe hatutarudi katika vita," alieleza.
"Mimi na Bw Kiir tulikubaliana kwamba vita vilifanyika kwa muda mrefu mno."
Kwa upande wake, Bw Kiir alieleza kwamba yeye na Bw Bashir wamekubaliana kwamba watatekeleza masharti yote yaliyoafikiwa ya kuimarisha uhusiano kati ya mataifa yao mawili.
No comments:
Post a Comment