Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Joyce Fissoo akisisitiza jambo wakati wa kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na wadau wa tasnia hiyo nchini.
Na Aron Msigwa - MAELEZO
31/1/2013 –Dar Es Salaam.
WASANII wa Filamu na Michezo ya kuigiza nchini wametakiwa kuzijua kanuni na taratibu zinazoongoza tasnia ya filamu na kuvitumia vyama vyao kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuepuka migogoro inayoweza kuzuilika.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na viongozi wa vyama vya waigizaji nchini (TDFAA) kilichofanyika leo jijini Dar Es salaam kuzungumzia Kanuni na Sheria ya Filamu pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia hiyo kuelekea zoezi la urasimishaji wa kazi za wasanii lenye lengo la kuongeza vipato vya wasanii na kukuza tasnia ya filamu nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa vyama hivyo wamesema kuwa kuna haja ya wasanii wote nchini kuwa makini na kazi wanazozifanya na kutumia muda wao kuzijua sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza tasnia ya filamu na Michezo ya kuigiza nchini hasa sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya mwaka 1976.
Wamesema kwa kipindi kirefu wahusika wa tasnia ya Filamu na Michezo ya kuigiza nchini ambao ni wasanii wamekuwa wakiingia kwenye fani hiyo pasipo kujua miiko na taratibu zinazoongoza tasnia hiyo na kujikuta wakiibua migogoro, kukiuka maadili na wakati mwingine kutonufaika na kazi zao kutokana na kukiuka vipengele vya katiba.
Viongozi hao wamefafanua kuwa ipo haja kwa wasanii kote nchini kujiunga na vyama na mashirikisho yanayoongoza tasnia hiyo ili waweze kusaidiwa wanapopata matatizo kuanzia ngazi ya wilaya mpaka taifa ili kuepusha hali ya sintofahamu waliyonayo wasanii wengi ambao wamejikuta wakikwama wanapotekeleza majukumu yao na kuishia kuilaumu serikali.
Akizungumza kwa msisitizo katika kikao hicho kwa niaba ya viongozi wenzake mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji nchini Tanzania (TDFAA) Bw. Michael Sangu amesema kuwa ipo haja ya wasanii nchini kuvitumia vyama vyao wanapokuwa na changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea katika masuala ambayo yanaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.
Kufuatia hatua hiyo ya kukutana na viongozi wa Wizara hiyo Bw. Michael Sangu amesema kuwa yapo mambo mengi ambayo wao wenyewe walikua hawayajui lakini kupitia vikao mbalimbali vya Wizara husika kupitia Bodi ya Filamu wameyaelewa na kuondoa hali waliyokua nayo ya kuilaumu serikali.
“Ni kweli yapo mambo mengi tulikua hatuyajui hasa sheria yenyewe ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya 1976 na kanuni mbalimbali zinazoongoza tasnia hii, ipo haja kwa sisi kama viongozi wa vyama vya wasanii nchini kuwa vikao vya mara kwa mara na wizara ili tuweze kujadili mambo yetu pale inapobidi ili kuboresha fani hii”, alisema.
Amesema, ipo haja ya vyama vya wasanii kuungana pamoja na kufanya kazi pamoja na serikali ili kuhakikisha kuwa tasnia ya filamu nchini inapendwa, kulindwa na kuheshimiwa na kuiomba Bodi ya Filamu nchini kuendelea kulinda maadili ya kazi za wasanii ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wasanii husika na kuzuia filamu zote zinazokiuka maadili ya mtanzania kuingia sokoni.
“ Nawaomba wasanii tuungane kwa pamoja na wasanii ambao bado hawajajiunga na vyama vyetu wajiunge ili tuwatambue na kuwasaidia kwani Chama cha Waigizaji Tanzania mpaka sasa tuna uongozi katika mikoa 12 na bado tunaendelea na mpango wa kuongeza maeneo ya utendaji nchi nzima ili tuweze kuwafikia wasanii wote ” Alisema Sangu.
Kuhusu Urasimishaji wa kazi za wasanii Bw. Sangu ameishukuru serikali kufuatia zoezi hilo kwani litazuia wizi wa kazi za wasanii kwa kiasi kikubwa na kuiomba serikali kuijengea uwezo bodi ya Filamu kuwa mamlaka kamili ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuweka utaratibu wa kudhibiti uingiaji wa filamu kutoka nje ya nchi ili kulinda soko la filamu za ndani na kuangalia namna ya kuwasaidia kupunguza tozo mbalimbali wanazotozwa wasanii kutokana na kazi zao ili waweze kunufaika kutokana na ugumu wa soko la filamu nchini Tanzania.
Naye Katibu wa Bodi ya Filamu nchini Bi. Joyce Fissoo amesema kuwa Bodi ya Filamu itaendelea kushirikiana na vyama vya wasanii katika kulinda maadili ya kazi za wasanii nchini na kuwaomba wasanii na viongozi wa vyama vyao kuzitumia ofisi za Bodi ya Filamu kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yahusuyo taratibu za upataji wa vibali vya filamu kwa mujibu wa sheria, ufafanuzi wa tozo mbalimbali, taratibu za ukaguzi wa Filamu na kumbi za maonyesho pamoja na mambo ya kuzingatia msanii anapotaka kutengeneza filamu.
Amesema Bodi ya Filamu imekuwa ikishirikiana na wasanii kwa kukutana nao, kuendesha mafunzo mbalimbali kwa waongoza filamu nchini na kutoa miongozo mbalimbali kwa wasanii kuhusu mambo ambayo hawatakiwi kuyafanya kwa mujibu wa sheria.
Amesema kuwa zoezi la urasimishaji wa kazi za wasanii litawajengea wasanii uwezo wa kumiliki kazi zao wenyewe na kuwafanya wanufaike na kuwawezesha kupata mikopo kupitia Benki mbalimbali nchini kwa kuwa watakua wameingia kwenye mfumo rasmi unaotambuliwa wa kuwa na hati miliki ya kazi zao. |
No comments:
Post a Comment