Hili ni jedweli la tathmani ya utabiri wa mvua za Masika kwa mwaka 2012.
Dk. Kijazi akielezea tathmini ya mvua hizo za Masika zilivyokuwa kwa mwaka 2012.
Juu na chini Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Kijazi akielezea tathmini ya mvua za Masika zilivyokuwa kwa mwaka 2012.
Dk. Kijazi akielezea kuhusu hali ya joto la bahari kwa kipindi cha miezi ya Septemba hadi Oktoba kwa mwaka 2012, hali inayosababisha upatikanaji wa mvua kama hakutokuwa na mgandamizo hali ya juu wa maji, suala ambalo hukimbiza mvua hizo.
Picha hii na ya chini, Dk. Kijazi akielezea kuhusu mgadamizo huo wa maji kwa bahari za Indian Ocean, Pacific na Medditerenian, ambazo zimelizunguka bara la Afrika, ambamo Tanzania imo.
Hapa Dk. Kijazi akiwaelezea waandishi wa habari, kuhusu utabiri wa Hali ya Hewa kwa mwezi huu wa Januari 2013.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Kijazi akielezea tathmini hizo mbele ya waandishi wa habari.
Waandishi wa habari wakinukuu taarifa iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Kijazi.
Wapigapicha wa televisheni nao wakichukua taarifa hiyo, iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk. Agnes Kijazi.
TAARIFA KWA UMMA
TATHMINI NA MWELEKEO WA MVUA NCHINI KWA KIPINDI
CHA JANUARI HADI
MACHI, 2013
Taarifa hii inatoa tathmini ya mvua kwa
msimu wa Oktoba hadi Disemba ,
2012 na mwelekeo wa mifumo ya hali
ya hewa na mvua kwa kipindi cha miezi ya Januari hadi Machi, 2013.
A: MUHTASARI
Utabiri wa mvua kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2012
Katika msimu wa Oktoba
hadi Disemba, 2012 maeneo mengi ya nchi yalitarajiwa kupata mvua za wastani
hadi juu ya wastani. Hata hivyo
utabiri huu ulihusu zaidi maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka yaani
kanda ya Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Pwani ya
Kaskazini.
Katika maeneo hayo mvua
zilitarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu ya mwezi Septemba hadi wiki ya pili ya
mwezi Oktoba, 2012. Katika maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, mvua
zilitarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi Oktoba hadi wiki ya nne ya mwezi
Novemba, 2012.
Mifumo ya hali ya hewa iliyotarajiwa kwa kipindi cha
Oktoba hadi Disemba, 2012
Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2012 hali ya joto la bahari ukanda
wa tropikali wa Bahari ya Pasifiki, lilitarajiwa kuwa juu ya wastani hali
iliyoshiria El-NiƱo hafifu. Hali ya joto la wastani hadi juu ya wastani
iliyokuwepo magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika-mashariki) sambamba
na joto la chini kidogo ya wastani
mashariki mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Indonesia) ilitarajiwa kusababisha
upepo kuvuma kutoka mashariki. Aidha, ongezeko la joto la bahari lililotarajiwa
katika kipindi cha Disemba, 2012 kwenye maeneo ya kusini magharibi mwa Bahari
ya Hindi, lingeweza kusababisha matukio ya vimbunga na kuvuma kwa upepo kutoka
magharibi kuelekea Bahari ya
Hindi, na hivyo kuongeza mvua katika maeneo mengi ya nchi kutokana na
unyevunyevu toka misitu ya Kongo.
(i) TATHMINI YA KUANZA KUNYESHA
(ONSET) MVUA KATIKA KIPINDI
CHA OKTOBA - DISEMBA 2012
Tathmini ya kuanza kwa mvua za Vuli katika
kipindi cha mwezi wa Septemba hadi Oktoba, 2012 katika baadhi ya maeneo
yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka inaonesha kuwa mvua zilianza kunyesha kati
ya wiki ya pili ya mwezi Oktoba hadi wiki ya kwanza ya mwezi Novemba 2012.
Katika maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, mvua zilianza kunyesha kati
ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Disemba 2012.
(ii) TATHMINI YA MVUA KATIKA KIPINDI
CHA OKTOBA –DISEMBA, 2012
Tathmini ya mvua za Vuli, katika
kipindi cha mwezi wa Oktoba hadi Disemba, 2012 katika maeneo yanayopata mvua
mara mbili kwa mwaka inaonesha kuwa mvua zimenyesha kwa kiwango cha kuridhisha
katika baadhi ya maeneo. Hata
hivyo, mtawanyiko wake haukuwa
mzuri. Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2012 maeneo ya
Ukanda wa Ziwa Viktoria hususani
Mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara na Geita pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa
wa Kigoma yamepata mvua za wastani hadi juu ya wastani pamoja na vipindi vya
mvua kubwa. Aidha, maeneo ya mikoa ya Shinyanga na Simiyu yamepata mvua za
chini ya wastani.
Maeneo ya nyanda za juu kaskazini
Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) yamepata mvua za wastani
japokuwa mtawanyiko wake haukuwa mzuri. Maeneo
ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Visiwa
vya Unguja na Pemba, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro) yamepata mvua za wastani
hadi chini ya wastani. Aidha,
katika maeneo mengine ya nchi yaliyosalia hususan maeneo yanayopata msimu moja
wa mvua ikiwemo maeneo ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma), magharibi mwa nchi
(mikoa ya Tabora na Kigoma), Nyanda za juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Rukwa,
Katavi, Njombe, Mbeya na Iringa), maeneo ya ukanda wa kusini mwa nchi (Mikoa ya
Mtwara, Lindi na Ruvuma) mvua zimeanza na zinaendelea kunyesha kwa kiwango cha kuridhisha, ingawaje mtawanyiko
wake bado si wa kuridhisha.
(iii) MIFUMO YA HALI YA HEWA
ILIYOKUWEPO KATIKA KIPINDI CHA
OKTOBA HADI DISEMBA, 2012
Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2012, hali
ya joto la bahari katika ukanda wa tropikali ya mashariki mwa bahari ya
Pasifiki iliendelea kushuka kwa kasi kutoka juu ya wastani hadi wastani, hali
hii haiashirii kuwepo kwa aidha La nina au El Nino. Aidha, kuwepo kwa joto la
juu ya wastani katikati mwa bahari ya Hindi na pwani ya Somalia; na mgandamizo
mkubwa wa hewa kusini mashariki mwa pwani ya Tanzania kulisababisha kupungua kuvuma kwa upepo
wenye unyevunyevu kutoka mashariki na kaskazini mashariki kuelekea pwani ya
Tanzania na nyanda za juu kaskazini mashariki. Hali hii ya mabadiliko ya joto
la bahari na mifumo ya hali ya hewa si ya kawaida na haijawahi kutokea katika
miaka iliyopita. Kutokana na mabadiliko hayo Mamlaka ya Hali ya Hewa ilitoa
mrejeo wa utabiri tarehe 24/10/2012.
Aidha kutokana na mabadiliko hayo yasiyokuwa ya kawaida taasisi
zinazohusika na masuala ya hali ya hewa katika Kanda ya Pembe ya Afrika (ICPAC)
na Kanda ya Kusini mwa Afrika (SADC-CSC) kwa mara ya kwanza ziliandaa warsha ya
wataalamu wa hali ya hewa ikiwemo Tanzania, kufanya uchambuzi wa mifumo ya hali
ya hewa na kutoa mrejeo wa mwelekeo wa mvua za msimu katika ukanda huu. Mikutano
hii ilifanyika tarehe 29 hadi 30 Novemba, 2012 Nairobi, Kenya na tarehe 5 hadi
13 Disemba, 2012 Lusaka, Zambia. Baada ya taarifa hiyo ya kikanda, Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania imefanya uchambuzi wa kina wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejeo wa utabiri wa msimu wa
mvua nchini.
Hali ya kuchelewa kuanza kwa msimu wa
mvua pia ilisababishwa na kutokea kwa Kimbunga kiitwacho ANAIS (mwanzoni mwa Oktoba,
2012) katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi (mashariki mwa kisiwa
cha Madagascar) ambacho kilibadilisha mwelekeo wa upepo wenye unyevunyevu
kuvuma kuelekea katikati ya bahari ya Hindi mahali kilipokuwa kimbunga.
Vilevile kuwepo kwa kimbunga MURJAN (katikati ya Oktoba, 2012) katika pembe ya Afrika ambacho kilisababisha
mfumo wa mvua kubaki kaskazini mwa Ikweta, hali iliyosababisha
kupungua kwa mvua katika baadhi ya maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa
nchi. .
(iv) MATUKIO
Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi 28 Disemba, 2012, kumekuwa na vipindi
vya mvua kubwa zilizoambatana na
upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Mwanza, Kigoma, Dodoma,
Mbeya, Iringa na Mara. Hali hiyo
ilisababisha vifo pamoja na uharibifu wa mali yakiwemo makazi ya watu na
mashamba.
B: TATHMINI
NA MWELEKEO WA Mifumo ya hali ya hewa
JANUARI HADI MACHI 2013.
Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2013, hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropikali ya
mashariki na magharibi mwa bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuwa ya wastani hadi
chini ya wastani. Hali kadhalika, joto la bahari katikati ya bahari ya Hindi
linatarajiwa kuwa chini ya wastani wakati joto la bahari karibu na pwani ya
Tanzania linatarajiwa kuwa la wastani hadi juu ya wastani. Hali hii inatarajiwa
kusababisha upepo wenye unyevunyevu kuvuma kutoka bahari ya Hindi kuelekea
katika maeneo ya ukanda wa Pwani. Vilevile, joto la bahari katika bahari ya
Atlantiki, kusini magharibi mwa bara la Afrika linatarajiwa kuwa la chini ya
wastani na hivyo kusababisha upepo kutoka magharibi kuvuma kuelekea maeneo ya
kusini magharibi mwa nchi.
C: MWELEKEO WA
MVUA KWA MWEZI JANUARI HADI MACHI , 2013
Mvua kwa
kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2013 zinatarajiwa kuwa za
wastani hadi juu ya wastani, isipokuwa maeneo ya kaskazini magharibi ambayo yanatarajiwa kuwa na mvua za
wastani hadi chini ya wastani. Aidha mchanganuo wake ni kama ifuatavyo;
Maeneo
yanayopata misimu miwili ya mvua (Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini
Mashariki ukanda wa ziwa Victoria):
Baadhi ya maeneo yanayopata mvua mara
mbili kwa mwaka (Mikoa ya Dar es salaam, Tangam Pwani, Arusha, Kilimnjaro,
Manyara, Mwanza, Mara, Geita, Shinyanaga, Kagera na Simiyu) yanatarajiwa kupata
mwendelezo wa mvua (out of season rains) mwezi Januari. Aidha utabiri wa mvua za masika katika
maeneo haya utatolewa mwezi Februari, 2013.
(ii) Mvua za Msimu
Kipindi cha mvua za Msimu Novemba hadi
Aprili ni mahsusi kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka (Kanda ya
Magharibi, Kanda ya kati, Nyanda za juu kusini magharibi, mikoa ya kusini na
pwani ya kusini). Mvua zinaendelea kunyesha na kwa kipindi cha Januari hadi
Machi, 2013 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo;
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya
Tabora, Katavi na Kigoma):
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani.
Kanda ya kati (Mikoa ya
Singida na Dodoma):
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda za juu
Kusini Magharibi: (Mbeya, Rukwa, Iringa na Morogoro-kusini ):
Mvua zinatarajiwa
kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya kusini
na Pwani ya kusini (Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi):
Mvua zinatarajiwa
kuwa za wastani hadi juu wastani.
MUHIMU: Aidha
katika maeneo mengi ya nchi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa viwango vya
mvua ya wastani vinaendelea kushuka, hivyo kufanya mvua za wastani katika
baadhi ya maeneo kutokidhi mahitaji ya shughuli mbali mbali kama vile kilimo,
maji na nishati.
|
Taarifa katika jedwali linaonyesha
‘probability’ kwa mfano maeneo ya kusini uwezekano wa kupata mvua za juu ya
wastani ni asilimia arobaini 40%,
mvua za wastani 35% na mvua za chini ya wastani 25%.
D. ATHARI NA USHAURI
Kipindi cha mvua
kilichobaki ni kifupi hivyo pamoja na matarajio ya mvua za wastani hadi juu ya
wastani katika baadhi ya maeneo ya kati na kusini mwa nchi tunashauri maji
yatumike kwa uangalifu hasa shughuli za umwagiliaji katika maeneo ya mito
inayotiririsha maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ili kuwa na uhakika wa
kupata maji ya kutosha katika mabwawa. Aidha vyanzo vya mito hiyo (cathment areas) vihifadhiwe na
kuhakikisha hakuna uharibifu wa mazingira.
Kuna uwezekano wa kuwa na
vipindi vifupi vya mvua kubwa zinazoambatana na upepo mkali katika kipindi hiki
cha mvua hivyo tahadhari ziendelee kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa
wananchi na mali zao.
Tunashauri pia wafugaji
wajenge tabia ya kuhifadhi malisho kwaajili ya kutumia wakati kunapokuwa na
upungufu wa malisho.
Mamlaka ya hali ya hewa
Tanzania Itaendelea kufuatilia Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na
vimbunga katika bahari ya Hindi na kutoa taarifa kuhusiana na mwelekeo wa mvua
nchini.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
No comments:
Post a Comment