Wajumbe wa Sekretarieti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kutoka kushoto, Mbaraka Saleh, Ahmed Saadat na Kailima Kombwey, wakiwa katika mkutano huo.
Na Mwandishi
Wetu
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi kuhusu
hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa usiku wa mwaka mpya na kuzungumzia
mchakato wa Katiba unaoendelea na kusema Rais hapaswi kulalamikiwa kwani yote
aliyosema yamo ndani ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Jaji
Warioba alitoa ufafanuzi huo leo (Jumamosi, Januari 5, 2013) katika mkutano
wake na Waandishi wa Habari wakati akizungumzia tathmini ya kazi ya kukusanya
maoni binafsi ya wananchi kupitia mikutano iliyomalizika tarehe 19 Disemba
mwaka jana (2012).
“Kuna
kitu gani kipya alichosema Rais? Yote aliyosema yapo kwenye Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na mimi katika mikutano yangu yote nanyi nimeyaeleza na
hakuna asiyejua,” alisema Jaji Warioba ambaye ameshawahi kuwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.
“Rais
alielezea mchakato wote kuanzia kukusanya maoni, kuandaa rasimu, kufanyika kwa
Mabaraza ya Katiba, Bunge Maalum la Katiba na kura ya maoni…haya yote yapo
kwenye sheria ambayo Wabunge waliipitisha,” alisema Jaji Warioba wakati akijibu
swali la Mwandishi wa Habari Jabir Idrissa aliyetaka kujua kauli ya Tume kuhusu
maoni ya baadhi ya wanasiasa kuwa Rais aliingilia kazi za Tume.
“Hivi
ingekuwaje kama Rais angetoa salam za Mwaka Mpya bila kuzungumzia mchakato
muhimu kwa nchi kama huu wa Katiba,” alihoji Jaji Warioba.
Akizungumzia
mikutano ya kukusanya maoni iliyomalizika mwezi uliopita, Jaji Warioba alisema kazi
ya kukusanya maoni ilianza tarehe 2 Julai mwaka jana na Tume yake imetembelea
na kufanya mikutano 1,776 katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa
mujibu wa Jaji Warioba, jumla ya wananchi 1,365,337 walihudhuria mikutano hiyo
na kati yao, wananchi 64,737 walitoa maoni kwa kuzungumza katika mikutano na
wengine 253,486 walitoa maoni yao kwa maandishi katika mikutano hiyo.
Kwa
mujibu wa maelezo ya Jaji Warioba, takwimu hizi hazijumuishi maoni
yanayoendelea kukusanywa na Tume yake kupitia posta, totuvi ya Tume, mitandao
ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za mkononi ambao hadi kufikia jana (Ijumaa,
Januari 4, 2013) jumla ya ‘sms’ 16,261.
Kuhusu
idadi ya wananchi waliojitokeza mikutanoni na kutoa maoni yao, Mwenyekiti huyo
alisema Tume imeridhika na idadi hiyo na kufafanua kuwa kilichokuwa kinatafutwa
na Tume ni hoja na kwamba haukuwa wakati wa kupiga kura.
“Ilikuwa
ni muhimu kufikia watu wengi iwezekanavyo na ndiyo maana tumefika kila sehemu.
Lakini tangu awali, tulishasema hatutaweza kumfikia kila mtu,” alisema na
kuongeza kuwa Tume yake imeridhika na idadi na maoni yaliyotolewa na wananchi
na kutoa mfano wa Tume ya Nyalali ambayo alisema ilipokea maoni ya wananchi
21,000 lakini Ripoti ya Tume hiyo ilisheheni mambo muhimu kwa taifa.
Jaji
Warioba alifafanua kuwa katika awamu zote nne za mikutano ya kukusanya maoni, wananchi
wametoa maoni kuhusu maeneo yote muhimu kama utawala, haki, maadili na mamlaka
yao na mengineyo.
Aliongeza
kuwa mikutano ya Tume ya kukusanya maoni ililelenga kupata hoja za msingi ili
Tume iweze kuandaa Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa katika mikutano ya
Mabaraza ya katiba itakayofanyika kila wilaya.
Akizungumzia hatua inayofuata, Jaji Warioba alisema kuwa
kuanzia keshokutwa (Jumatatu, tarehe 7 Januari, 2013), Tume hiyo itaanza
kukutana na makundi mbalimbali kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba
Mpya. Makundi hayo ni Vyama vya Siasa; Vyama vya Kitaaluma; Asasi za Kiraia;
Taasisi za Kidini, Vyama vya Wafanyakazi, Wakulima na Wafanyabiashara na
makundi mengine mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Tume yake imeshawasiliana na
makundi hayo na imeandaa utaratibu wa kukutana na wawakilishi wao katika ofisi
za Tume na baadhi ya kumbi jijini Dar es Salaam na Zanzibar.
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi rasmi Mei 2 mwaka jana (2012) na kazi ya
kukusanya maoni kupitia mikutano imefanyakika kwa awamu nne. Awamu ya kwanza
ilifanyika kati ya Julai 2 – 30, 2012 wakati awamu ya pili ilifanyika kuanzia
tarehe 27 Agosti – 28 Septemba, 2012. Awamu ya tatu iliyofanyika kati ya terehe
8 Oktoba, 2012 na tarehe 6 Novemba, 2012 na awamu ya nne na ya mwisho
ilifanyika kati ya tarehe 19 Novemba – 19 Disemba mwaka jana (2012).
|
No comments:
Post a Comment