TANGAZO


Thursday, February 9, 2012

Waziri Mkuu Pinda, Awasimamisha Watendaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki, alipokuwa akizungumzia mgomo wa Madaktari, Dar es Salaam hivi karibuni. (Picha na Kassim Mbarouk)

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa.
Akizungumza katika mkutano na madaktari, leo asubuhi, Hospitali  ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Waziri Mkuu Pinda, amesema kuwa amewasimamisha watendaji hao, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa dhidi yao.
Aidha, kuhusu hatua za kumchukulia Waziri wa Wizara hiyo, Hajji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya, kama ilivyokuwemo kwenye madai ya madaktari hao, Waziri Pinda, alisema kuwa hilo ni suala la Rais na kudokeza kuwa kinachofuatia sasa kinaeleweka.
Aliwataka madaktari waliokwenye mgomo huo, kurudi kazini ili kuokoa maisha ya wananchi na kuwahakikishia kuwa hakuna tishio lolote kwao la kuwafukuza kazi.
Awali katika madai yao, madaktari hao, walitaka katika masharti yao ya kurejea kazini kuwa ni pamoja na kuuondoa uongozi mzima wa ngazi za juu wa Wizara hiyo, kutokana na kushindwa kwao kutekeleza majukumu yao ya kiutendaji, pia kuboreshewa maslahi yao, yakiwemo nyongeza ya mshahara kwa madaktari wanaoingia kwenye ajira, mshahara wa kuanzia, uwe sh. milioni 3.5.
Pia nyongeza za posho zao mbalimbali, zikiwemo za kujikimu, hatarishi na nyinginezo.

 Baadhi ya Madaktari, waliokwenye mazoezi kwa vitendo, walio kwenye mgomo, wakiwa katika moja ya vikao vyao, walivyokuwa wakijadili maslahi yao. (Picha na Kassim Mbarouk)


 Mmoja wa Madaktari, walio kwenye mgomo, akichangia hoja zilizokuwa zikitolewa kwenye vikao vyao, ukumbi wa Don Bosco kabla ya kupigwa marufuku kwa mikusanyiko yao na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye mkutano wake na viongozi wa jiji, Karimjee, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.   (Picha na Kassim Mbarouk)


 Mmoja wa viongozi wa mgomo wa madaktari, Steven Ulimboka, akizungumza na waandishi wa habari, hivi karibuni, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam. (Picha na Kassim Mbarouk)


 Katibu Mkuu, aliyesimamishwa kazi na waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Blandina Nyoni, akizungumza na waandishi hivi karibuni katika moja ya mikutano ya viongozi wa Wizara hiyo na waandishi, wizarani hapo. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Serikali, ambaye naye wamesimamishwa pamoja, Deo Mtasiwa. (Picha na Kassim Mbarouk)


 Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hajji Mponda, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam hivi karibuni katika moja ya mikutano yake aliyokuwa akizungumzia juu ya mgomo wa madaktari hao. Kulia ni Naibu wake, Dk. Lucy Nkya. (Picha na Kassim Mbarouk)

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliyesimamishwa kazi, Blandina Nyoni, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari, wakati Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Lucy Nkya (kulia), alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na mgomo wa madaktari hivi karibuni. (Picha na Kassim Mbarouk)

No comments:

Post a Comment