TANGAZO


Thursday, February 9, 2012

Waziri Mkuu Pinda Amaliza Mgomo wa Madaktari

Watoa mwezi mmoja kwa Serikali kutekeleza Makubaliano yao




Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, akizungumza kuhusu madaktari waliogoma.

Na Mwindishi Wetu.
 HATIMAYE madaktari nchini wametangaza rasmi kumaliza mgomo wao ambapo leo wameahidi kurejea kazini ili kutoa huduma za kitabibu kwa wagonjwa.
Uamuzi huo wa madaktari umeleta matumani kwa wagonjwa ambao kwa wiki kadhaa wamekosa huduma hiyo na kujikuta wakikata tamaa kuhusu hatma ya maisha yao.
Juhudi ambazo zimefanywa na Serikali, Bunge na wananchi kwa ujumla zimezaa matunda baada ya madaktari kuamua kukubali ombi la Waziri Mkuu Mizengo Pinda, la kurudi kazini baada ya kuridhika na baadhi ya maeneo ambayo wamekubaliana.
Katika kikao kilichofanyika jana na kuwashirikisha Waziri Mkuu Pinda, madaktari bingwa, madaktari, madaktari walioko kwenye mafunzo kwa vitendo na wauguzi walifikia makubaliano kuwa sasa mgomo umekwisha rasmi.
Lakini madaktari walitoa mwezi mmoja wa kuitaka Serikali kuhakikisha inatekeleza mambo kadhaa waliyokubaliana.
Akizungumza kwa niaba ya madaktari hao, Mwenyekiti wa Umoja wa Madaktari, Dk.Ulimboka Steven alisema wametafakari kwa kina maelezo ya Waziri Mkuu baada ya kukaa kwa zaidi ya saa mbili wakijadili suala hilo kati yao na Serikali na kuona ipo haja ya kusitisha mgomo huo.
Dk.Ulimboka alisema kuwa licha ya kumaliza mgomo huo, wametoa muda wa mwezi mmoja kwa Serikali kufanyia kazi madai yao ili kuondoa malumbano ambayo yanaweza kujitokeza kama wataona hakuna ambacho kimefanyiwa kazi kwa mujibu wa makubaliano yao.
Awali katika kikao kati ya Pinda na madaktari, aliwaambia madaktari hao kuwa Serikali inatambua umuhimu wao kwa kuwa ndiyo wenye dhamana ya kuwa hudumia wananchi, hivyo imeamua kutekeleza madai yao japo si kwa asilimia zote kama walivyotaka.
Pamoja na mambo mengine, Pinda katika kutuliza hasira za madaktari hao aliamua kusikiliza kilio chao cha muda mrefu kuhusu kutokuwa na imani na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambapo alitumia nafasi hiyo kutangaza kumsimamisha kazi Katibu Mkuu Blandina Nyoni, pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Deo Mtasiwa wakati Waziri na Naibu wake wakisubiri uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye aliyewateua.
Aliwahakikishia madaktari hao kuwa kusimimamishwa kwa watendaji hao wa ngazi ya juu katika wizara ni kutaka kupisha uchunguzi wa kubaini tuhuma zinazowakabili kama inavyodaiwa na madakari hao ambao wamekuwa wakisisitiza kutokuwa na imani nao.
"Katibu Mkuu Nyoni na Mganga Mkuu tumeamua kuwasimamisha kazi ili kuchunguza tuhuma ambazo zinawakabili. Kuhusu Waziri na naibu wake hao watachukuliwa hatua na Rais kwani ndiye mwenye jukumu la kuwawajibisha. Pia tutaendelea kusafisha wizara hii," alisema Pinda.

Baadhi ya Madaktari waliokuwa wamegoma, wakiwa kwenye mkutano wao (katikati mbele) ni mwandishi wa Gazeti la The Citizen, Mkinga Mkinga, akifuatilia mkutano huo.

Huku akisilizwa na mamia ya wafanyakazi hao, Pinda alisema katika mwezi mmoja uliyopita huduma hospitalini hapo hazikuwa nzuri na kilio cha Watanzania ni kikubwa, hivyo akawasihi walitazame jambo hilo kwa umakini mkubwa.
Pinda alitumia nafasi hiyo kuwasihi madaktari hao kujali uzalendo na kurudi kazini, kwa kuwa wamebeba dhamana ya kuwahudumia Watanzania na kubainisha kuwa hakuwa na dhamira ya kumfukuza yoyote kwani Serikali yenyewe ndiyo imewasomesha, hivyo haoni sababu ya kuwafukuza.
"Nilipokutana nanyi mlinipa maadhimio nane ambayo nilipaswa kuyatolea ufafanuzi, lakini halikufanyika, pamoja na kutopata nafasi nikaona kuna umuhimu wa kulifanyia kazi kila adhimio kwa kuvihusisa vyombo mbalimbali vilivyoko chini ya wizara hii," alisema.
Pinda alisema suala la madaktari walioko katika mafunzo kwa vitendo ambao wanafanya kazi nyingi muhimu kabla ya madaktari bingwa ambao kwa mfumo uliopo wanapata posho ya kila mwezi, lakini hadi kufikia Desemba 22 mwaka jana walikuwa hawajapata posho zao.
Alisema kwa kulipa uzito suala hilo waliwalipa posho hizo, lakini jambo hilo likaibua mambo mengi hivyo akaagiza posho hizo kulipwa sanjari na mishahara na kusisitiza kuwa zilipwe kwa wakati unaotakiwa.
Maazimio mengine yalikuwa ni kupandishiwa posho kutoka sh.3,000 hadi 5,000 kwa walioko mafunzoni, sh.15,000 badala ya 5,000 kwa madaktari wa kawaida na sh. 25, 000 kwa madaktari bingwa badala ya 20,000 ya awali, ambapo aliahidi kulifanyia kazi kulingana na bajeti ijayo na kubainisha kuwa lazima zipatikane zaidi ya sh. bilioni 2.
Kuhusu kufanya kazi katika mazingira hatarishi na ugumu wa kazi Waziri Mkuu aliwataka wapeleke mapendekezo kuhusu maeneo yapi yanayopaswa kuboreshewa maslahi, hivyo akasema kuwa wataangalia namna ya kuwavutia kwenda kufanya kazi katika maeneo kama hayo.
Pia alizungumzia kuhusu madai ya kutaka kupanda kwa mshahara hadi kufikia sh.3,500,000 na kusema kuwa ni vigumu kuamua jambo hilo kwa kuwa ili kutekeleza hili ni lazima idara zote chini ya wizara zipandishiwe mishahara hiyo.


Baadhi ya madaktari hao wakiwa kwenye moja ya mikutano yao ya kujadili maslahi yao.

" Jambo hili ni zito sana kwa kuwa karibu bajeti yote itakuwa imeenda kwa madaktari hivyo suala hil ni gumu na lazima tukae chini tuangalie namna ya kukabiliana nalo," alisema Pinda.
Kuhusu madai ya usafiri, Waziri mkuu Pinda alikiri kuwa ni muhimu na kubainisha kuwa upo utaratibu wa serikali kutoa mikopo kwa madaktari ili waweze kujinunulia magari hayo lakini akatoa angalizo kuwa wasione ufahari kununua magari ya gharama kubwa kubwa na kushindwa kumudu gharama za kuyatunza.
"Madaktari wote watakopeshwa pesa ili waweze kununua magari, ila mnatakiwa kuangalia aina ya gari ili usije kuparamia VX (shangingi), ndugu yangu utapata shida,"alisema Pinda.
Wakati kikao hicho kinaendelea wanaharakati waliotinga hospitalini hapo  walikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko isiyo halali huku wakiwa na mabango kitu ambacho kiliwatia shaka Polisi.
Wanaharakati hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa Habari (Tamwa), Ananilea Nkya, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Helen Bisimba na wengine ambao walidai walifika hapo kwa nia ya kufahamu hali ilivyo na hatima ya kikao cha Waziri Mkuu na madaktari.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi aw Kinondoni, Charles Kenyela alisema wanaharakati hao walikamatwa kwa kuwa hawakuwa katika hali ya kwenda kuangalia hali ya Muhimbili bali walikutwa na viashiri vya vurugu kama mabango ambavyo vingehatarisha amani.
Kenyela alisema kuwa juzi walifanya mkusanyiko katika Barabara ya Ali Hassan mwinyi bila kibali hivyo kuhatarisha amani kwa watumiaji wa barabara hiyo na kusababisha kusimama kwa shughuli katika eneo hilo.
Kamanda huyo alisema kuwa wameendelea kuwashikilia watuhumiwa hao wakati wakiendelea kufanya uchunguzi na huku wakisubiri dhamana endapo wataafnikiwa kupata.
Hata hivyo Nkya alikanusha tuhuma hizo na kudai kuwa walifika Muhimbili baada ya kusikia Waziri Mkuu anazungzumza na madaktari hivyo wakaona wafike kufahamu hatima ya mgomo lakini wakaambulia kukamatwa na kupelekwa kituoni kuandika maelezo.

No comments:

Post a Comment