Waziri mmoja nchini Uganda amevamia warsha ya wanaharakati wa mapenzi ya jinsia moja na kujaribu kumkamata mwandaaji wa shughuli hiyo, limesema gazeti moja la huko na pia kundi la wanaharakati wa haki za binaadam waishio Uingereza.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya mbunge mmoja kuurejesha muswada wenye utata wa kupinga mapenzi ya jinsia moja.
Muswada huo unapendekeza kuongeza adhabu nchini Uganda kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, ambavyo ni kinyume cha sheria, kutoka kwenda jela miaka 14 hadi kifungo cha maisha.
David Bahati, mbunge aliyewasilisha hoja hiyo binafsi, alisema kipengele kinachopendekeza adhabu ya kifo kitaondolewa.
Muswada huo ulipendekezwa kwa mara ya kwanza mwaka 2009, lakini haukuwahi kujadiliwa.
Warsha hiyo ilikuwa imeandaliwa na shirika liitwalo Freedom and Roam Uganda, shirika ambalo lilianzishwa na mwanaharakati mashuhuri wa wapenzi wa jinsia moja Kasha Jacqueline Nabagesera.
Ilikuwa ikifanyika katika hoteli moja mjini Entebbe, kilomita 40 kutoka mji mkuu Kampala, gazeti la Daily Monitor limeripoti.
"Nimeufunga mkutano huu kwa sababu ni haramu. Hakuruhusu mapenzi ya jinsia moja nchini Uganda. Kwa hiyo rudini nyumbani," gazeti hilo limemkariri Bw Lokodo.
Kwa mujibu wa kundi la haki za binaadam la Uingereza, Amnesty International, Bw Lokodo alisema kama wanaharakati hao hawataondoka mara moja, angetumia nguvu dhidi yao.
Waziri huyo pia aliamrisha kukamatwa kwa Bi Nabagesera, ambaye alitunukiwa tuzo ya Martin Ennals mwaka jana kwa harakati zake za kupigania haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda.
Hata hivyo mwanaharakati huyo alitoroka na kukimbia hotelini hapo.
"Hili ni jaribio la kushangaza la kuzuia shughuli za amani na za kihalali za watetezi wa haki za binaadam nchini Uganda," amesema katibu mkuu wa Amnsety International, Salil Shetty, kupitia taarifa aliyotoa.
Marekani na Uingereza zimetaka nchi zinazoendelea kuheshimu haki za wapenzi wa jinsia moja la sivyo watakuwa katika hatari ya kupiteza misaada wanayopatiwa.
Tangu muswada huo uliporejeshwa bungeni, kumekuwa na taarifa za kuongezeka kunyanyaswa kwa wapenzi wa jinsia moja, limesema kundi la haki za wapenzi hao.
No comments:
Post a Comment