Carlos Tevez, mshambulizi wa Manchester City, ameomba radhi kwa tabia yake isiyofaa hivi majuzi, na iliyoanza tangu alipogombana na meneja Roberto Mancini mwezi Septemba.
Mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 28, alirudi katika klabu ya Man City wiki iliyopita, baada ya kuchukua hatua mikononi mwake, alipoamua kurudi nchini Argentina kwa kipindi cha miezi mitatu.
“Ningelipenda kuomba msamaha kwa dhati na pasipo kikwazo chochote kwa kila mtu, na kwa yoyote yule niliyemkosea kwa vitendo vyangu ikiwa nimemuudhi”, alielezea Tevez kupitia taarifa.
Wakati huohuo Tevez amefutilia mbali malalamiko aliyokuwa amewasilisha rasmi dhidi ya klabu ya Man City.
“Nia yangu sasa ni kuhusika zaidi katika kuichezea soka klabu ya Manchester City”, alisisitiza.
Baada ya kushindwa kujiunga na AC Milan ya Italia kama ilivyotazamiwa wakati wa usajili wa mwezi Januari, Tevez bila shaka alikuwa na uamuzi mgumu wa kuamua iwapo aendelee kupumzika na akicheza golf huko Argentina, ama arudi tena mjini Manchester na kujaribu kupigania nafasi yake katika timu yake.
Kuna uwezekano bado wa Tevez kuhama wakati wa msimu wa joto, lakini angalau inaelekea kwa hivi sasa uwanja wa Etihad umetulia, baada ya sokomoko iliyozushwa na mchezaji huyo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina hajawahi kuichezea City tangu mwezi Novemba, wakati meneja Roberto Mancini anadai alikataa kuingia uwanjani kama mchezaji wa zamu, na hatimaye timu kushindwa na Bayern Munich ugenini magoli 2-0 katika mechi ya klabu bingwa mwezi Septemba.
Tevez anadai kulikuwa na hali ya sintofahamu na mkorogano wa lugha, na akaeleweka vibaya.
Moja kwa moja baada ya ugomvi huo, Mancini alisema Tevez “amekwisha” kama mchezaji wa City, lakini baadaye alielezea kuna uwezekano wa mchezaji huyo kukaribishwa tena katika timu, ikiwa ataomba msamaha
.