SWAHILIsimu
Rais wa zamani nchini Nigeria Olusegun Obasanjo anatarajiwa kukutana na upande wa upinzani nchini Senegal katika juhudi za kutuliza taharuki za kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu hapo Jumapili.
Takriban watu sita wameuawa katika machafuko ya maandamano kupinga hatua ya rais Abdoulaye Wade kuwania tena urais.Wapinzani wa kiongozi huyo wamesema hatua hiyo ni kinyume cha katiba. Bw. Obasanjo yuko mjini Dakar kama kiongozi wa ujumbe wa Muungano wa Afrika na kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS.
Hapo Jumanne wiki hii polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuvunja maandamano ya upinzani. Viongozi wa upinzani chini ya mrengo wa M23 wamepanga maandamano ya kitaifa kumshinikiza rais Wade kubatilisha hatua ya kuwania urais.
Baadhi ya wanasiasa watakaofanya kikao na Bw Obasanjo ni pamoja na waliokuwa Mawaziri wakuu Moustapha Niasse na Idrissa Seck, pamoja na kiongozi wa chama cha Socialist Tanor Dieng.
Senegal imekuwa na sifa ya mataifa mojawapo ya Afrika ambayo yamekuza demokrasia huku likiwa taifa pekee Afrika Magharibi ambalo halijashuhudia mapinduzi ya kijeshi.
Maandamano yalizuka mapema mwakani baada ya mahakama ya juu nchini Senagal kumkubalia rais Wade kuwania urais huku ikimpiga marufuku msanii mashuhuri Youssou Ndour.
Katiba ya nchi imeweka mihula miwili kwa afisi ya urais, lakini mahakama ya juu ilisema awamu ya kwanza haikushirkishwa kikatiba.
No comments:
Post a Comment