Mabaharia wa meli hiyo kwa jina Costa Allegra iliyo na zaidi ya abiria 1000, walituma ujumbe wa kuomba msaada baada ya moto kuzuka na kuteketeza mitambo ya kuzalisha umeme, ikiwa takriban Kilomita 300 kusini mwa Ushelisheli.

Meli iliopata ajali hapo awali ya Costa Concordia

Chombo kimoja cha uvuvi kutoka Ufaransa tayari kimewasili katika eneo hilo na maafisa wa Italia wamesema meli nyingine na mashua zinatarajiwa kuwasili katika eneo hilo baadaye adhuhuri ya leo.
Kamanda Cosimo Nicastro kutoka jeshi la wanamaji la Italia ndiye anayesimamia shughuli nzima ya uokoaji.
Ameiambia BBC kwamba mashua ya uvuvi iliyowasili katika eneo hilo inawasaidia pakubwa kuwasiliana na mabaharia katika meli Costa Allegra.
Kadhalika kamanda Cosimo Nicastro amesema hakuna mipango ya kuwaondoa abiria katika meli hiyo.
Meli hii inamilikiwa na kampuni ambayo ilishutumiwa vikali baada ya kutokea kwa ajali ya meli nyingine iliozama katika pwani ya Italia na kusababisha vifo kadhaa.