Mshambuliaji wa klabu ya Uingereza ya Wycombe Wanderers Adebayo Akinfenwa ametoa onyo kali kwa nahodha wa Real Madrid Sergio Ramos.
Ramos amekuwa akishutumiwa baada ya nyota wa Liverpool na Misri Mohamed Salah kuumia begani walipokabiliana wakati wa fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya.
Ramos pia aligongana na kipa wa Liverpool Loris Karius na inadaiwa kwamba huenda tukio hilo lilimduwaza kwa kumsababishia mtikisiko wa ubongo jambo ambalo pengine lilichangia makosa ya kushangaza aliyoyafanya kipa huyo.
Makosa yake mawili yalichangia mabao mawili ya Real Madrid ambao walishinda mechi hizo 3-1.
Akinfenwa ameandika kwenye Twitter kwamba daima atakuwepo kuwasaidia na kuwaunga mkono Liverpool wakitishiwa.
Amepakia video kwenye mtandao huo wa kijamii akionesha nguvu zake kwa kuvuta buti kwa kutumia mikono yake mwenyewe.
Klabu yake inatokea High Wycombe eneo la Buckinghamshire, England na inacheza ligi ya daraja ya tatu kwa sasa.
'Mnyama'
Akinfenwa - ambaye jina lake la utani ni The Beast (Mnyama) - amekiri kwenye video hiyo yake kwamba pengine hatawahi kukutana na Sergio Ramos uwanjani.
"Tazama kama, sitawahi kucheza dhidi yako kwa sababu klabu yangu haitawahi kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, na una bahati."
Mashabiki wa Liverpool wameonekana kumshukuru sana mchezaji huyo.
Ramos mwenyewe amejitetea na kusema hafai kulaumiwa, akisema hatua ya Mohamed Salah kumshika mkono kwanza ndiyo iliyosababisha mchezaji huyo wa Liverpool kuumia.
Ramos, 32, aliambia jarida la michezo la AS la Uhispania: "Upuuzi mtupu, wamemwangazia Salah sana. Sikutaka kuzungumza kwa sababu kila kitu kimeongezwa chumvi."
"Kitu pekee sijasikia ni Roberto Firmino akisema kwamba alipata mafua kwa sababu aliangukiwa na jasho langu," amesema Ramos kwa kutania.
Ramos pia amedai kwamba Salah angeendelea kucheza mechi hiyo "iwapo angedungwa sindano kipindi cha pili".
- Mchezaji wa asili ya Tanzania kucheza Kombe la Dunia
- Kipa wa Liverpool Karius atumwa kwa madaktari Marekani
"Nautazama mchezo vyema, anaushika mkono wangu kwanza na ninaanguka upande mmoja, na jeraha lilitokea kwenye mkono ule mwingine na wanasema kwamba nilishika mkono na kuukatalia kama mchezaji wa judo. Baada ya hapo, kipa wao anasema nilimduwaza kwa kumgonga.
"Niliwasiliana na Salah kupitia ujumbe, alikuwa vyema. Angeendelea kucheza iwapo angedungwa sindano kipindi cha pili. Nimefanya hivyo mara kadha lakini wakati ni Ramos alifanyajambo kama hilo, linakwamilia zaidi.
"Sijui kama ni kwa sababu umekuwa (nimekuwa) Madrid kwa muda mrefu na umeshinda kwa muda mrefu sana kiasi kwamba watu hulitazama tofauti."
Akinfenwa ni nani?
Saheed Adebayo Akinfenwa ni mchezaji aliyezaliwa 10 Mei 1982.
Anafahamika sana kutokana na nguvu zake za mwili na unene na misuli yake.
Kimo chake ni futi tano na inchi 11.
Amewahi kuwachezea Swansea City na Northamptom. Alikuwa anachezea klabu ya AFC Wimbledon kabla ya kuhamia Wycombe.
Utotoni, alikuwa anaishabikia sana Liverpool na mchezaji aliyempenda zaidi alikuwa John Barnes.
Babake ni Mwislamu lakini mamake ni Mkristo. Alikuwa Mwislamu na hata alikuwa akifunga mwezi wa Ramadhan alipokuwa mdogo lakini siku hizi ni Mkristo.
Anafahamika zaidi kwa kuorodheshwa kuwa mchezaji mwenye nguuv zaidi katika mchezo wa video wa FIFA.
Mwaka 2014 alihudhuria uzinduzi wa FIFA 15 akiwa pamoja na wachezaji wengine nyota na watu mashuhuri kama vile Rio Ferdinand, George Groves na Lethal Bizzle.
Akinfewa uzani wake unadaiwa kuwa kilo 101 na anaweza kuinua kilo 200, ambao ni karibu mara mbili uzani wake.
Ana kampuni ya mavazi ya Beast Mode On, ambapo hutumia sifa zake kama mtu mwenye nguvu kama za mnyama.
Salah alianguka vibaya na kuumia kwenye bega wakati wa kipindi cha kwanza dhidi ya Real.
Licha ya kuumia, ametajwa kwenye kikosi cha Misri kitakachocheza Kombe la Dunia nchini Urusi.
Inaaminika kwamba ingawa huenda asichezee Misri mechi yake za kwanza Urusi, huenda akashiriki mechi za baadaye.
Wengi wa mashabiki wa Liverpool wanamlaumu Ramos kutokana na kuumia kwa Salah, tukio ambalo mwamuzi hakutoa adhabu yoyote.
Ombi limeanzishwa kuwataka Fifa na Uefa kumwadhibu mchezaji huyo wa Uhispania.
Wakili mmoja nchini Misri amewasilisha kesi ya kutaka Ramos atakiwe kulipa fidia ya £874m kwa madhara na hasara aliyowasababishia raia wa Misri "kimwili na kiakili."
No comments:
Post a Comment