TANGAZO


Friday, May 25, 2018

SERIKALI KUHAKIKISHA UBORA WA ZAO LA KOROSHO UNAENDELEA KUZINGATIWA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt. Mary Mwanjwelwa

Na Frank Mvungi- Maelezo
SERIKALI kuendelea  kuhakikisha  kuwa  Korosho zinazozalishwa hapa  nchini zinakuwa na ubora unaotakiwa katika Soko la Kimataifa ili kuendelea kukuza uzalishaji na kuchochea maendeleo hapa nchini.
Akijibu swali  la Mbunge wa Mtwara Vijijini Mhe. Hawa  Ghasia, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt. Mary Mwanjwelwa amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa soko la korosho ghafi linaendelea kukua ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018 ilikuwa zuri hususan kutokana na kupanda kwa bei ya korosho na kuuza kuanzia shilingi 3,500 hadi 4,000 kwa kilo.
" Bei ya Korosho ilipanda kutokana na   Serikali kuimarisha minada ya Korosho na kuwahamasisha wanunuzi kutoka Vietnam kuja kununua korosho moja kwa moja hapa nchini  badala ya kupata korosho hizo kupitia India kama ilivyokuwa imezoeleka kwa muda mrefu"  Alisisitiza Dkt. Mwanjelwa
Akifafanua Mhe. Mwanjelwa amesema kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwafanyia uchunguzi wa kina wale wote walioripotiwa katika taarifa Timu ya uchunguzi iliyoundwa na Serikali ili kuhakikisha kuwa wale waliosababisha korosho makontena mawili yaliyogundulika kuwa yalichanganywa na kokoto huko vietnam  ambapo ilibainika kuwa korosho hizo zimetoka Tanzania.
Aliongeza kuwa Serikali itachukua hatua mbalimbali ikiwemo  kuitaka Bodi ya Korosho Tanzania, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghalani, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Mamlaka za Serikali za Mitaa kushirikiana katika kuimarisha usimamizi wa ubora wa Korosho katika mnyororo wake wote kudhibiti uhalifu huo.
Aidha  Mhe. Mwanjelwa amezitaka  Kampuni za ndani na nje ya nchi kuwasilisha malalamiko ya yao Serikalini pale wanapoona mapungufu katika Biashara hiyo badala ya kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari kwa kuwa kuchafua jina  na biashara ya korosho za Tanzania.
Pia alisema kuwa uchunguzi uliofanywa na vyombo vya dola umepelekea  watuhumiwa wa swala hilo wameshakamatwa kufuatia uchunguzi uliofanywa na vyombo hivyo na watuhumiwa wamekamatwa na kwa manufaa ya uchunguzi huo Serikali itatoa kauli mara itakapokuwa tayari kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment