Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro kuwasili katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano Cha Kimataifa Arusha (AICC) kwa ajili ya kufungua jukwaa la fursa za biashara mkoani humo jana Alhamisi Mei 24, 2018.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadhamini wa mkutano wa jukwaa la fursa za biashara mkoani humo lililofanyika jana Alhamisi Mei 24, 2018.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (wa tatu kushoto) akifurahia jambo na mmoja wa Wajasiriamali wadogo waliopo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha muda muda baada ya kufungua mkutano wa jukwaa la biashara Mkoani Arusha jana Alhamisi Mei 24, 2018.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyabiashara ndogondogo wa Halmashauri ya Jiji la Arusha muda mfupi baada ya kufungua mkutano wa jukwaa la biashara mkoani Arusha jana Mei 24, 2018.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akiangalia moja ya bidhaa zinazozalishwa na kikundi cha ujasiriamali cha Ideal health care cha Jijini Arusha muda mfupi baada ya kumaliza kwa mkutano wa jukwaa la biashara Mkoani Arusha jana Mei 24, 2018.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akipata maelezo kuhusu uzalishaji wa bidhaa za sabuni kutoka kwa mjasiriamali Bartazal Odull muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa jukwaa la biashara Mkoani Arusha jana Mei 24, 2018. Wengine pichani ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dkt. Jim Yonaz (kushoto) na kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dkt. Hassan Abbasi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akipata maelezo kuhusu uzalishaji wa bidhaa za vikapu kutoka kwa mjasiriamali Hadija Zahoro (kulia) muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa jukwaa la biashara Mkoani Arusha jana Mei 24, 2018.
Na Mwandishi Wetu, Maelezo, Arusha
25.5.2018
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amelitaka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kutanua mtandao wa majukwaa ya biashara ili kufikia ngazi ya kimataifa pamoja na kutangaza fursa za masoko na uwekezaji zilizopo nchini.
Akifungua mkutano wa jukwaa la fursa za biashara jana (alhamisi Mei 24, 2018) Jijini Arusha, Waziri Mwakyembe alisema ili kufikia adhma hiyo TSN haina budi kuboresha ubunifu wake katika uendeshaji wa majukwaa hayo ambayo tayari yameanza kuleta matokeo chanya kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Waziri Mwakyembe alisema Serikali ya Awamu ya Tano ipo katika mkakati mkubwa wa mageuzi ya uchumi, hivyo TSN kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Wafanyabiashara hawana budi kupanua wigo wa fursa za biashara zilizopo nchini kwa kuvutia wawekezaji na wafanyaboiashara mbalimbali nchini.
“Katika ukanda huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania imebahatika kuwa na fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwemo mbuga za wanyama zilizopo kwa wingi hapa mkoani Arusha, hivyo kupitia jukwaa nawaomba wananchi wa Mkoa wa Arusha kuchangamkia fursa za kuibua miradi ya uwekezaji” alisema Dkt Mwakyembe.
Aidha Waziri Mwakyembe aliongeza kuwa ili kufikia nchi ya kipato cha kati ni wajibu wa taasisi za umma na binafsi kuboresha mfumo wa utendaji kazi ikiwemo kuimarisha ubunifu katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kutengeza fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Dkt. Waziri Mwakyembe pia alipongeza ubunifu huo wa TSN kwa kuwa umewasaidia wafanyabiashara katika mikoa mbalimbali kukutana kwa karibu zaidi na taasisi za usimamizi na uratibu wa biashara nchini, kwa kuwa huwawezesha kutoa maoni, ushauri na mapendekezo yao katika namna bora zaidi ya kufanya biashara.
Naye Mhariri Mtendaji wa TSN, Dkt. Jim Yonaz alisema katika kupanua mtandao wa biashara zake kwa umma, ofisi yake imepanga kuongeza wigo wa wateja wake kwa kusambaza nakala za magazeti yake kufika katika nchi za China, India na Marekani ambapo hata hivyo kwa sasa magazeti hayo yanasomwa katika nchi ya Rwanda.
Anaongeza mikutano ya majukwaa ya fursa za biashara yamelenga katika kuibua fursa na hamasa ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuzingatia malengo na shabaha mbalimbali zilizowekwa na Serikali kupitia Dira, Sera, mikakati na program mbalimbali.
Kwa mujibu wa Dkt. Yonaz anasema hadi sasa majukwaa ya fursa za biashara tayari yamefanyika katika mikoa ya Simiyu, Mwanza, Tanga, Shinyanga, Zanzibar na Arusha ambapo wafanyabiashara na wawekezaji wameweza kutumia fursa hizo kwa ajili ya kupata uelewa wa kuhusu fursa za biashara na uwekezaji.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hab Nkwizu alisema Bodi yake imejipanga kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma zake kwa umma ikiwemo kuimarisha mfumo wa uendeshaji wa majukwaa hayo ili kuweza kwenda na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaletea maendeleo wananchi.

No comments:
Post a Comment