TANGAZO


Friday, April 27, 2018

UVUTAJI SIGARA NA UNYWAJI POMBE ULIOKITHIRI HUSABABISHA MAGONJWA YA MISHIPA YA DAMU YA MOYO

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimzibua mgonjwa  mishipa ya damu ya moyo ambayo imeziba kwa kutumia mtambo wa Cathlab  katika kambi maalum ya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo inayofanyika katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 23 wamezibuliwa mishipa ya damu pamoja na kufanyiwa uchunguzi.(Picha zote na Brighton James - JKCI) 
Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Taasisi ya Madaktari Afrika ya nchini Marekani wakimzibua mgonjwa  mishipa ya damu ya moyo ambayo imeziba kwa kutumia mtambo wa Cathlab katika kambi maalum ya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo inayofanyika katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 23 wamezibuliwa mishipa ya damu pamoja na kufanyiwa uchunguzi.

Na Brighton James - JKCI
27/4/2018 
WATANZANIA wameshauriwa kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri kwa kufanya hivyo watajiepusha na magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yanaouwa watu wengi Duniani.
Ushauri huo umetolewa leo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Madaktari Afrika ya nchini Marekani Mazen Albaghded wakati akiongea na waandishi wa habari katika kambi maalum ya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Dkt. Albaghded alisema kuwa ulaji wa vyakula vyenye mafuta na bila kufanya mazoezi ambayo yangesaidia kuyeyusha mafuta hayo kunaweza kusababisha  kupata kirahisi ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo. Wagonjwa wa kisukari  na wenye shinikizo la juu la damu  nao wanaweza kupata ugonjwa huo kirahisi.
“Mishipa ya damu inapozungukwa na mafuta  baadaye huweza kuziba  na hivyo damu kushindwa kwenda katika misuli ya moyo (myocardium) na kusababisha mtu kupata shambulio la moyo”, alisema.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo ya matibabu ya  siku nne Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Tulizo Shemu alisema wagonjwa wanaotibiwa ni wale wanaohitaji matibabu ya kibingwa yenye uhitaji wa uchunguzi yakinifu.
Dkt. Shemu alisema  kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa njia ya kutoboa tundu dogo kwa mgonjwa wanaangalia kama mishipa ya moyo imeziba na ikiwa imeziba wanaizibua kwa kumuwekea mgonjwa  kifaa maalum kinachojulikana kwa jina la “stent” ambacho kinasaidia mshipa wa damu usizibe tena.
Katika kambi hiyo ambayo ilienda sambamba na mafunzo ya kubadilishana ujuzi wa kazi jumla ya wagonjwa 23 wamefanyiwa  vipimo na matibabu ambapo hali zao zinaendelea vizuri na  wengine wameruhusiwa kurudi nyumbani.

No comments:

Post a Comment