TANGAZO


Saturday, January 20, 2018

WAZIRI MPINA: WIZARA HAINA MPANGO WA KUONGEZA TENA MUDA WA KUPIGA CHAPA MIFUGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Joelson Mpina akizungumza na vyombo mbalimbali vya  habari  katika ukumbi wa Ofisi ya Wizara hiyo mjini Dodoma leo. Kushoto ni Naibu Waziri wake Mhe.Abdalah Ulega na mwishoni ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo. Mkutano huo ulikuwa kwa ajili yakutoa tathimini ya zoezi la upigaji chapa mifugo  baada ya kumalizika kwa siku 15 za awali baada ya muda wa nyongeza wa siku 30 uliotolewa na Waziri Mpina.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Joelson Mpina akijibu maswali ya  Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Ofisi ya  Wizara hiyo Mjini Dodoma leo. Mkutano huo ulikuwa kwa ajili ya kutoa tathimini ya zoezi la upigaji chapa mifugo  baada ya kumalizika kwa siku 15 za awali baada ya muda wa nyongeza wa siku 30 uliotolewa na Waziri Mpina.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Joelson Mpina akijibu maswali ya  Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Ofisi ya  Wizara hiyo Mjini Dodoma leo. Mkutano huo ulikuwa kwa ajili ya kutoa tathimini ya zoezi la upigaji chapa mifugo  baada ya kumalizika kwa siku 15 za awali baada ya muda wa nyongeza wa siku 30 uliotolewa na Waziri Mpina. Kulia ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji,  Mashimba Ndaki.
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema wizara yake haina  mpango wa kuongeza tena muda zoezi la utambuzi wa  mifugo na kuwataka wafugaji popote walipo nchini kupaza sauti zao ili kuhakikisha kuwa ng’ombe na punda  wote wamepigwa chapa ifikapo Januari 31 mwaka huu.

Pia Waziri Mpina amechukizwa na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuwakatalia wafugaji kupiga chapa mifugo yao kwa kisingizio kuwa sio wakazi halali wa maeneo husika jambo ambalo amesema halikubaliki na kusisitiza kuwa zoezi lisihusishwe na migogoro ya muda mrefu ya matumizi ya ardhi na hivyo kuagiza kuwa ng’ombe na punda wote nchini wapigwe chapa isipokuwa ya kutoka nchi jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusu tathmini ya utekelezaji wa zoezi upigaji chapa mifugo, Mpina alisema hadi kufikia Januari 16 mwaka huu jumla ya ng’ombe 10,306,359 sawa na asilimia 59.3 ya lengo wameshapigwa chapa ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 ya tathmini ya awali.

Aidha amesema wafugaji wote nchini wataoshindwa kupiga chapa mifugo yao ndani ya muda uliowekwa hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Namba 12 ya mwaka 2010 ibara ya 4 kifungu cha 26 huku akizionya halmashauri ambazo zitashindwa kutekeleza kikamilifu hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi wake.

Alisema hadi sasa halmashauri 100 zimepiga chapa zaidi ya asilimia 50, halmashauri 54 zimepiga kati ya asilimia 10 hadi 50, halmashauri 14 zimepiga chini ya asilimia 10 huku halmashauri 9 zikiwa bado hazijaanza kabisa zoezi hilo.

Waziri Mpina amezitaja Halmashauri hizo ambazo hadi sasa hazijaanza kupiga chapa ni Tandahimba, Nanyumbu, Mafia, Newala, Halmashauri za miji ya Newala, Nanyamba, Masasi na Manispaa za Kigamboni na Ilemela Mwanza ambapo amesema halmashauri 68 ambazo ziko chini ya asilimia 50 na ambazo haijaaanza kabisa tayari  halmashauri hizo ameziwasilisha kwa Waziri Mkuu.

Pia alisema halmashauri 6 zina ng’ombe wengi wa maziwa walio kwenye mpango wa kuvalishwa hereni  pamoja na mikoa mingine ambapo jumla ya ng’ombe wote wa maziwa nchini 782,995 kwa sasa, aidha jumla ya punda 572,353 wanatarajiwa kupigwa chapa, taarifa kutoka mikoani kuhusu utekelezaji wa zoezi hili zinaendelea kukusanywa kila siku.

Alisema kumekuwa na ongezeko la asilimia 20.8 katika muda wa kipindi cha wiki mbili tangu muda wa nyongeza kutolewa ongezeko hili ni kutokana na juhudi za pamoja za uhamasishaji uliofanywa kati ya Wizara na halmashauri pamoja na mchango mkubwa uliotolewa na vyombo vya habari.

“Hivyo juhudi kubwa za pamoja baina ya Wizara, Halmashauri, vyombo vya habari na wafugaji zinahitajika ili kukamilisha zoezi la upigaji chapa kwa asilimia 100, kwa kuwa hadi sasa bado asilimia 40.7 ya ng’ombe hawajapigwa chapa “alisema.

Aidha Waziri Mpina amesema kipimo cha asilimia hakitakuwa kigezo cha mwisho cha uhakiki mifugo iliyopigwa chapa badala yake ni kuhakikisha kila ng’ombe na punda mwenye umri wa kuanzia miezi sita wamepigwa chapa.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji,  Mashimba Ndaki alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na  wizara hiyo katika kusimamia zoezi la upigaji chapa ambalo limeungwa mkono na wafugaji wengi nchini.

No comments:

Post a Comment