TANGAZO


Thursday, December 14, 2017

MATOKEO YA UTAFITI WA TWAWEZA: MALIPO KWA WALIMU BAADA YA MATOKEO YAMEWEZESHA KUJIFUNZA KWA UFANISI SAWA NA NYONGEZA YA NUSU MUHULA KATIKA MWAKA WA MASOMO

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze

*Kuwalipa walimu bahshishi kumewanufaisha wanafunzi zaidi ya 48,000 katika kujifunza stadi za Kiswahili na Hisabati

14 Decemba 2017, Dar es Salaam: 
BAADA ya miaka miwili ya majaribio, Twaweza, kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na shirika la Innovations for Poverty Action (IPA), wamedhihirisha kuwa kuwalipa walimu fedha baada ya matokeo ya kujifunza kunaweza kuboresha matokeo ya kujifunza.

Matokeo haya yamethibitisha kwamba wanafunzi wameweza kujifunza na kupata stadi stahiki kwa muda
wa mwaka mmoja kile ambacho wangeweza kujifunza kwa mwaka na nusu muhula.

Matokeo ya utafiti unaojulikana kama KiuFunza, utafiti mkubwa wa aina yake Afrika Mashariki, yaliwasilishwa katika majadiliano na wadau wa elimu jijini Dar es Salaam.

Kwa kipindi cha miaka miwili ya KiuFunza, Twaweza na IPA wamefanya majaribio yafuatayo katika shule 200 kwenye wilaya 21 za Tanzania:
·         Kutoa bahshishi kwa kujifunza stadi mahususi zilizoainishwa kwa darasa kwenye kundi moja la shule (Stadi).
·         Kutoa bahshishi kwa ongezeko la kujifunza kwenye kundi lingine la shule (Mashindano).

Njia zote mbili zilijaribiwa ili kulinganisha matokeo yaliyopatikana na kundi la shule za ulinganisho ambazo walimu wake hawakupewa bahshishi. Japokuwa mfumo wa Mashindano ni mgumu zaidi kueleweka kuliko mfumo wa Stadi, mfumo huu huleta usawa zaidi kwa walimu, kwakuwa wanafunzi hushindana na wenzao walio kwenye makundi yenye uwezo unaofanana. Stadi  hueleweka kwa urahisi zaidi lakini pia huwapendelea walimu wanaofundisha wanafunzi wenye uwezo mkubwa (mara nyingi wa shule za mijini).

Wastani wa bahshishi waliyolipwa walimu wa masomo ni shilingi 266,315.00 sawa na karibu asilimia 42 ya wastani wa mshahara wa kila mwezi (kabla ya kodi) mwaka 2016. Kiwango cha chini cha fedha kilicholipwa kwa walimu ni shilingi 8,100 wakati ambapo ni walimu wachache tu hawakuambulia kitu. Mwalimu aliyelipwa kiasi kikubwa kuliko wote alipata shilingi milioni 3.6.

Mbali na kuboresha matokeo ya kujifunza, mfumo wa kuwalipa walimu bahshishi umeonekana kuungwa mkono na walimu wengi:
  • Walimu tisa kati ya kumi kwenye shule za majaribio wanaunga mkono wazo la malipo kwa matokeo.
  • Walipoulizwa kuhusu utaratibu huu kuwa wa kisera, asilimia 63 ya walimu waliafiki kwamba Serikali iweke mfumo rasmi wa motisha kwa walimu kutokana na matokeo mazuri wakati yatakapofanyika maboresho ya mishahara (lakini asilimia 37 walisema kiwango cha malipo hayo kiongezwe na kiwe sawa kwa wote)

Mwaka 2016
  • Shule 135 kutoka wilaya 21 zilizoshiriki kwenye utafiti na shule 60 zilitumika kwa ajili ya ulinganisho.
  • Jumla ya wanafunzi 65,643 walifanya mtihani maalumu wakiwemo wanafunzi wa shule za ulinganisho.
  • Kwa ujumla, wanafunzi 48,042 walikuwa katika shule ambako motisha ilitolewa na hivyo walifanikiwa kujifunza zaidi kuliko wenzao.

Matokeo haya ni kutoka awamu ya pili ya KiuFunza 2015 -2016. Katika awamu ya kwanza ya KiuFunza 2013 – 2014 Twaweza ilifanya jaribio la kupeleka fedha za ruzuku moja kwa moja shuleni (utaratibu huu sasa unatumiwa na Serikali kuanzia Januari mwaka 2016) na Malipo kwa walimu kwa matokeo ya kujifunza pekee na kwa kuchanganya ruzuku na bahshishi. Awamu hii ya kwanza ya KiuFunza ilionesha matokeo chanya ya kujifunza pale ambapo motisha kwa walimu na shule kupelekewa fedha za ruzuku moja kwa moja vilipochanganywa. Awamu ya pili ya KiuFunza ilijaribu mifumo makini zaidi ya utoaji wa motisha baada ya Serikali kupeleka Ruzuku ya Uendeshaji wa Shule moja kwa moja shuleni 2016.

Twaweza imechagua kujikita kwenye kuwalipa walimu fedha za motisha awamu ya kwanza na ya pili ya KiuFunza kwa sababu ushahidi kutoka maeneo mbalimbali duniani unaonesha kuwa motisha huwahamasisha walimu kuongeza jitihada katika kufundisha na kuleta matokeo chanya ya kujifunza. Kwa kuongezea, KiuFunza (na tafiti nyingine) zinaonesha wazi kuwa motisha kwa mwalimu na uwajibikaji ni mambo ambayo yamekosekana shuleni. Wakati wa ziara za kushtukiza katika shule za msingi mwaka 2016:


  • 41% ya walimu walikuwa darasani wakifundisha.
  • 27% hawakuwepo shuleni.
  • 32% walikuwepo shuleni lakini hawakuwa darasani kufundisha.
  • kutokana na walimu kutohudhuria darasani inakadiriwa kuwa Shillingi bilioni 793 hupotea kila mwaka, yaani hulipwa kama mishahara kwa walimu amba hawakufundisha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze, anasema, “Twaweza, kwa kushirikiana na IPA tumeonesha kuwa utoaji wa motisha kwa mwalimu unaweza kuboresha matokeo ya kujifunza. Japokuwa kujifunza kunachangiwa na mambo mengi, tumeonesha, kupitia utafiti huu wa kisayansi, kuwa kuchanganya motisha na uwajibikaji kunaweza kuleta matokeo mazuri ya kujifunza kwa wanafunzi. Huu ni ushahidi thabiti wa kile kinachoweza kufanyika na kuwa na uhakika kuwa tukifanya hivyo watoto wetu watajifunza.

No comments:

Post a Comment