TANGAZO


Tuesday, October 17, 2017

MAAFISA ARDHI HANNANG WAPEWA SIKU 90 KUJIREKEBISHA KABLA YA KUCHUKULIWA HATUA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabulla

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabulla amefanya ziara ya kushtukiza katika idara ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Hannang mkoani Manyara na kukuta mfumo mbovu wa uhifadhi wa hati za kumiliki ardhi hali ambayo ni rahisi kwa maafisa hao kudanganya na kumilikisha watu wawili wawili.

Mheshimiwa Mabulla ameyagundua hayo baada ya kupekua katika makabati ya uhifadhi wa nyaraka hizo katika ofisi ya Idara ya Ardhi na kuona mapungufu makubwa katika mafaili hayo hali inayoweza kupelekea   maafisa hao wa ardhi kufanya udanganyifu.

Mabulla aliamua kupekua Hati za mwananchi mmojammoja na kugundua baadhi ya hati hazina vielelezo vya kumbukumbu na baadhi ya nyaraka za umuliki wa ardhi hazina mtiririko mzuri wa uhifadhi wa mafaili.

Mara baada ya kugundua mapungufu hayo makubwa Mheshimiwa Mabulla alimpa muda wa miezi mitatu Afisa Ardhi Mteule Bwana Egidius Kashaga kurekebisha mapungufu hayo pamoja na yeye mwenyewe kubadilika na akishindwa kufanya hivyo atamvua cheo chake na kumuadhibu kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Mabulla amekutana na wananchi wa Kata ya Mogitu, Wilaya ya Hanang mkoani Manyara na kusikiliza kero zao za ardhi hasa suala la muwekezaji wa Kiwanda cha Manyara Cement Limited ambae ameomba eneo la ujenzi wa kiwanda la ukubwa wa ekari 370.

Mmiliki huyo Bwana James Mtei alipeleka maombi yake kwa Halmashauri ya Wilaya ya Hannang akiomba ardhi katika kijiji cha Mogitu ili ihawilishwe na imilikishwe kwa Kampuni yake kwa hati miliki chini ya Sheria ya Ardhi (Sura 113) kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji saruji.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo ili mtu au kampuni iweze kumilikishwa ni lazima maombi hayo yaridhiwe na wanakijiji na kumfikia Waziri wa Ardhi na baadae kuidhinishwa na Mheshimiwa Raisi ikiwa ataridhia kutoa kibali chake cha Uhawilishaji.

Mheshimiwa Mabulla alitembelea eneo hilo linalotaraji kujengwa Kiwanda cha uzalishaji saruji ili aweze kujiridhisha kabla ya kummilikisha mwekezaji huyo.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabulla anamalizia ziara yake Mkoani Morogoro ambapo kesho anataraji kutembelea Chuo cha Ardhi cha Morogoro na kutatua changamoto zinazokikabili chuo hicho pamoja kutatua changamoto za walimu, wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho.

No comments:

Post a Comment