TANGAZO


Thursday, July 6, 2017

BALOZI SEIF IDDI AZUNGUMZA NA UONGOZI WA TAASISI YA USHAURI WA MASUALA YA UHANDISI YA ENDSIGHT ILIYO CHINI YA USIMAMIZI WA SHIRIKA LA CHANGAMOTO YA MILENIA LA MAREKANI (MCC) MJINI ZANZIBAR

Rais wa Taasisi ya Ushauri wa masuala ya Uhandisi  ya Endsight iliyo chini ya usimamizi wa Shirika la Changamoto ya Milenia la Marekani { MCC } Bwana Matthew McLean (kulia), akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar. 
Balozi Seif Ali Iddi (katikati) akiwa katika pamoja na Rais wa Taasisi ya Ushauri wa masuala ya Uhandisi  ya Endsight  Bwana Matthew  McLean aliyeko upande wa Kulia yake , Waziri Ardhi Mh. Salama Aboud Talib Kushoto  yake, Naibu Waziri Ujenzi Mh. Mohamed Ahmed Salum wa Pili kutoka Kushoto pamoja na baadhi ya Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/7/2017.
TAASISI ya Ushauri wa masuala ya Uhandisi  ya Endsight  iliyo chini ya usimamizi wa Shirika la Changamoto ya Milenia la Marekani { MCC } imeazimia kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha miradi ya Maendeleo kupitia miundombinu ya Mawasiliano na huduma za Kijamii.

Rais wa Taasisi hiyo Bwana Matthew McLean alitoa kauli hiyo wakati alipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Mazungumzo hayo pia yalijumuisha Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Mh. Salama Aboud Talib, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usarifishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahmed Salum pamoja na watendaji wakuu wa baadhi ya Taasisi za Serikali.

Bwana Matthew alisema Endsight imekuwa ikitoa ushauri wa Kitaalamu katika fani ya uhandisi katika kuona kiwango cha miundombinu kinachowekwa kwenye miradi  inayohusika zaidi na masuala ya uhandisi inatekelezwa katika hadhi na daraja inayotakiwa kitaalamu.

Alisema miundombinu ya bara bara na Mawasiliano , kilimo ikiwemo pia miradi ya huduma  za maji safi na salama inahitaji ungalizi sahihi katika uanzishwaji wake ili wakati inapoanza kufanya kazi itoe huduma sahihi iliyokusudiwa kitaalamu.

Naye Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Mh. Salama Aboud Talib pamoja na watendaji wa Serikali walimueleza Bwana Matthew kwamba Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto wa upatikanaji wa maji safi na salama katika baadhi ya maeneo.

Waziri Salama alisema nguvu za washirika wa maendeleo zinahitajika katika kuunga mkono sekta hiyo licha ya juhudi kubwa inayoendelea kuchukuliwa na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika kuongeza nguvu kwenye mindombinu ya Sekta ya  Maji Nchini.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mataifa, Taasisi pamoja na Mashirikia rafiki yana fursa za kusaidia au kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kuwaletea maendeleo Wananchi wake.

Balozi Seif alimuhakikishia Rais huyo wa Taasisi ya Ushauri ya Endesight ya Marekani iliyo chini ya Shirika la Changamoto ya Milenia ya Marekani kwamba Zanzibar iko tayari kushirikiana kwa kina na Taasisi au Nchi yoyote iliyo tayari kusaidia mipango ya Maendeleo.

Rais wa Taasisi ya Ushauri wa masuala ya Uhandisi  ya Endsight  iliyo chini ya usimamizi wa Shirika la Changamoto ya Milenia la Marekani { MCC } Bwana Matthew yupo Zanzibar kuangalia maeneo ambayo Taasisi yake inaweza kushirikiana na Zanzibar katika kutoa Ushauri wa Kitaalamu wa Kiufundi.


No comments:

Post a Comment