Idadi ya watu waliofariki katika ajali mbaya ya kuteketea kwa lori nchini Kenya, imepanda na kupita watu 30.
Kwa mjibu wa naibu kamanda mkuu wa jimbo la Nakuru Isaaca Masinde, ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia Jumapili katika eneo la Karai kwenye barabara ya kutoka Nairobi kuelekea Naivasha.
Lori moja la kubeba mafuta, lilianguka na kulipuka katika eneo la barabara hiyo yenye shughuli nyingi nchini Kenya na kusababisha mauwaji ya watu 30 papo hapo.
Watu wengine zaidi wamefariki wakitibiwa mjini Naivasha.
Shirika la msalaba mwekundu nchini humo, limesema lori hilo la mafuta, lililokuwa njiani kuelekea nchi jirani la Uganda, lilipoteza usukani na kisha kugonga magari kadhaa kwenye barabara kati ya Nairobi na Naivasha yapata kimomita 100 kutoka mji mkuu Nairobi.
Mtu mmoja kwa jina Moses Nandalwe aliyeshuhudia ajali hiyo, ameiambia BBC kuwa, magari kadhaa yalishika moto na kuanza kuchomeka, huku watu wengi waliofika katika eneo la ajali hiyo ili kushuhudia kilichotokea, wakikumbwa na moto huo na kisha wakachomeka.
Magazeti nchini Kenya yanaripoti kuwa zaidi ya watu 40 wanahofiwa kufa, huku magari 12 yakiteketea. Kuna taarifa pia kuwa maafisa kadhaa wa polisi pia wameangamia.
Miongoni mwa magari yaliyoteketea ni Basi moja la matatu lililokuwa na abiria 14, ambao wanahofiwa wote wamefariki.
Bw. Mwachi Pius Mwachi, naibu mkurugenzi wa shirika la kukabiliana na majanga nchini Kenya, amesema kuwa lori hilo la mafuta lilikuwa likiteremka kwa kasi, kabla ya kuanza kuungua.
Ajali hiyo mbaya imetokea nchini Kenya, wakati ambapo madaktari na wauguzi wakiendelea na mgomo wao, hatua ambayo imelemaza kabisa shughuli za matibabu katika hospitali za umma.Idadi ya watu waliofariki katika ajali mbaya ya kuteketea kwa lori nchini Kenya, imepanda na kufikia 40.
No comments:
Post a Comment