Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye akiwaeleza jambo Waandishi wa habari kuhusu dhumuni la kutembelea uwanja wa Taifa 11 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam. |
WAZIRI wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye leo ametembelea Uwanja
wa Taifa Jijini Dar es Salaam ili kukagua shughuli za marekebisho ya
miundombinu inayoendelea uwanjani hapo ikiwemo kukagua ufanisi wa Kamera za kufuatilia matukio
Uwanjani pamoja na marekebisho ya viti vya kwenye majukwaa.
Katika
ziara yake Waziri Nape amekagua namna Kamera za CCTV zinavyokuwa na uwezo wa
kubaini matukio mbalimbali yanayoendelea uwanjani ambapo ameridhika na utendaji
kazi wa kamera hizo na kusisitiza zitumike ipasavyo ili kuwabaini wahusika
wanaoharibu miundombinu ya uwanja.
Amesema
kwamba kazi ya kubaini waharibifu wa miundombinu kwa sura katika uwanja huu kwa kutumia hizi
kamera yataongeza hali ya usalama kwenye uwanja na pia kusaidia kufuatilia
matukio ya kihalifu Uwanjani kama vile kuvunja viti”, alisema Mhe. Nape.
Aidha,
amesema kwamba ukarabati wa uwanja unaoendelea sasa pinid utakapokamilika
utaufanya uwanja huo kuwa salama zaidi na ndiyo maana kamera nyingi zimeweka
ili kuendelea kubaini matukio yanayoendelea ndani na nje ya mipaka ya uwanja
ikiwemo milangoni.
“Kwa
sasa uwanja wetu utaweza kushughulika na mtu mmoja mmoja anayehujumu
miundombinu yetu, kwasababu kamera zetu zina uwezo mkubwa wa kumtambua mtu kwa
sura pindi awapo uwanjani kuanzia magetini”,alisema Mhe. Nape.
Ameagiza
ukarabati wa miundombinu uendelee ikiwemo mageti na viti uendelee kufanyika
kwani yeye anachosubiria ni kukabidhiwa uwanja huo siku ya tarehe 13 Desemba
mwaka huu na siku hiyo ndiyo itafahamika thamani ya ukarabati uliofanyika kwa
ujumla.
Aidha,
amegusia suala la Mkataba ulioingiwa kati ya Serikali na Klabu ya Yanga African
ambapo amesema kwamba, Serikali iliingia Mkataba na Klabu ya Yanga African ya kutumia
uwanja wake wa Taifa pamoja na uwanja wa Uhuru tarehe 1 Desemba, 2016 kwa muda
wa mwaka mmoja yaani mpaka tarehe 30 Novemba,2017.
Amesema
kwamba, kutokana masharti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) pamoja
na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), vilabu vyote vinavyoshiriki
michezo ya Kimataifa vinatakiwa kuonyesha uthibitisho wa umiliki wa uwanja au
viwanja vitakavyotumika katika mechi zao au kuonyesha mkataba walioingia ambapo
mechi hizo zitachezwa.
“Kwa
kuwa klabu ya Yanga haina Uwanja wake, walileta ombi Wizarani, la kuingia
Mkataba na Mmiliki wa Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru yaani Serikali. Serikali
iliona ni busara kuingia mkataba na Klabu ya Yanga African ili pale ambapo
watahitajika kutaja uwanja watakaotumia waweze kutaja Uwanja wa Uhuru au Uwanja
wa Taifa”, alisema Mhe. Nape.
Kwa
muktadha huo, Klabu ya Yanga itaendelea kutumia uwanja wa Uhuru ambao
haukujumuishwa katika maamuzi ya kufungiwa na hauna tatizo la kukarabatiwa.
Amesisitiza
kuwa, Serikali ina nia njema kwa vilabu vyake na wadau wote wa Michezo na Serikali
inafanya shughuli zake kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni, hivyo amevitaka
Vilabu vyote viwe na utamaduni wa kufuata sheria, taratibu na Kanuni katika
kutekelea majukumu yao.
No comments:
Post a Comment